Serikali inaendelea kuboresha sekta ya afya -Dk. Biteko

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amepongeza juhudi za Serikali katika kuboresha sekta ya afya, akibainisha kuwa miradi mingi imeanzishwa ili kuongeza ufanisi wa huduma na kuboresha maisha ya Watanzania.

Dk. Biteko alitoa kauli hiyo Novemba 1, 2024, akiwa Sengerema mkoani Mwanza, alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kwenye uzinduzi wa jengo la kisasa la upasuaji na mradi wa umeme wa jua katika hospitali ya Sengerema DDH, inayosimamiwa na Jimbo Katoliki la Geita.

Katika hotuba yake, Dk. Biteko aliipongeza Kanisa Katoliki kwa juhudi zake katika utoaji wa huduma za afya na kuonyesha namna Serikali inavyoshirikiana na sekta ya dini katika kuhudumia wananchi.

Alisema, “Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Samia imefanya kazi nyingi ikiwemo kujenga hospitali mpya 129, kukarabati hospitali kongwe 50, kujenga hospitali za wilaya 677 na zahanati 425. Nawaomba watu Sengerema na sisi wote kujua kwamba wafadhili wametoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo hili na mradi wa umeme wa jua kwa kujinyima kwa ajili yetu. Tutunze miundombinu hii.”

Dk. Biteko aliwaasa wananchi kulinda vifaa na majengo hayo ili yaweze kuwahudumia kwa muda mrefu. “Tutatibiwa sisi kutoka Kigoma na Kagera na wakati wa Covid-19 hapa palikuwa na msaada mkubwa. Haitakuwa sawa wakija wakakuta tumebadilisha na kuwa tofauti na lengo lao. Tutunze vifaa hivi na majengo haya na tuwape moyo ili waweze kutusaidia katika maeneo mengine yenye uhitaji,” alisema.

Aliendelea kwa kuwashukuru wafadhili waliofanikisha miradi hiyo na kueleza umuhimu wa msaada wa kimisionari unaotolewa na Kanisa Katoliki, ambao umesaidia kuondoa umaskini kwa kuhubiri mema, kutoa huduma za afya, na kusaidia wahitaji.

Aliongeza, “Tunasherehekea mafanikio haya kwa sababu umisionari umelenga kuhudumia watu kiroho na kimwili. Niwapongeze sana Kanisa Katoliki kwa kuunga mkono juhudi ambazo Serikali ingefanya.”

Aidha, Dk. Biteko aliwaomba viongozi wa dini kuendelea kuhubiri amani, akiunganisha dira ya maendeleo ya taifa ya 2050 na amani, huku akiwataka Watanzania kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa amani bila kuleta mgawanyiko.

Mbunge wa Sengerema, Hamis Mwagawa, naye alitoa shukrani zake kwa Mtawa Dk. Marie Jose na wafadhili wa mradi, akieleza jinsi msaada huo ulivyosaidia hata wakati wa janga la Covid-19.

Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita, Flavian Kassala, aliunga mkono kauli hizo akisema kwamba ujenzi wa hospitali hiyo ulianzishwa na watawa sita waliotaka kusaidia jamii. “Tuna juhudi za kutoa huduma kwa gharama nafuu na tuna mfuko wa kusaidia wahitaji. Misaada kutoka kwa Shirika la Marafiki wa Sengerema na Simba Health imetuwezesha kujenga chumba cha upasuaji chenye vifaa vya kisasa,” alisema Askofu Kassala.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Sengerema, Sr. Dk. Marie Jose, alisema hospitali hiyo ina uwezo wa kulaza wagonjwa 22,000 na sasa inatoa huduma bora za kibingwa kwa akina mama na watoto.

Aliendelea kusema: “Leo ni siku ya furaha kwani tumepata jengo hili la kisasa la upasuaji lililogharimu shilingi bilioni 2.7 na mradi wa umeme wa jua wenye thamani ya shilingi bilioni 1.7.”

Mfadhili wa mradi wa jengo la upasuaji, Doris Mars, alisema yeye na familia yake waliguswa kusaidia mradi huo kwa kuwa lengo lake ni kuboresha maisha ya watu. “Mungu ametupa uwezo wa kusaidia wengine na Biblia Takatifu inatuambia kila binadamu ameumbwa kwa sura na mfano wake, hivyo tunaamini tutasaidia kuokoa maisha ya watu wa Sengerema,” alisema Mars.

Misa takatifu kwa ajili ya uzinduzi huo iliongozwa na Mhashamu Askofu Mkuu wa Jimbo la Songea, Damiani Denis Dalu, ambaye alikumbusha umuhimu wa kudumisha misaada ya kanisa katika sekta ya afya, elimu, na huduma za kijamii. Alihitimisha kwa kumshukuru Mwasisi wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na Serikali kwa kuendelea kuthamini mchango wa kanisa katika maendeleo ya watu.

Related Posts