Mbeya. Ikiwa imepita miezi miwili tangu kutoweka kwa msanii wa uchoraji, Shadrack Chaula (24), baba yake mzazi, Yusuph Chaula (56) ameiomba Serikali kufanya uchunguzi wa kina kujua aliko mwanaye.
Mzee Chaula amesema tangu kutoweka kwa kijana wake kama familia wanaishi matumbo moto, huku jitihada za za kumtafuta zikiendelea bila mafanikio.
Shadrack alitoweka baada ya kuchukuliwa na watu wasiojulikana Agosti 2, 2024 majira ya saa 2:30 asubuhi akiwa katika eneo la biashara zake kwenye Kijiji cha Ntokela Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya.
Kabla ya tukio hilo, Julai 3, 2024 Shadrack alishikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kosa la kuchoma picha ya kuchora ya Rais Samia Suluhu Hassan, kufuatia video iliyosambaa mitandaoni ikionyesha tukio hilo.
Julai 5, 2024, alishtakiwa na kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela au kulipa faini ya Sh5 milioni katika Mahakama ya Wilaya ya Rungwe.
Hata hivyo, wanaharakati na watumiaji wa mitandao ya jamii walimchangia na kulipa faini hiyo na kumwezesha kutoka jela Julai 8, 2024.
Akizungumza katika mahojiano kwa simu Oktoba 31, 2024, baba mzazi wa Shadrack, amesema kama familia wanakiri kuwa kijana wao alitenda kosa la kumkashfu kiongozi mkuu wa nchi, lakini alishalipiwa faini ya Sh5 milioni na wasamaria wema.
Amesema siku kadhaa baada ya kutoka gerezani alikabidhiwa kwake kupitia Mwanasheria wake, Michael Mwangasa.
“Zilipita wiki mbili watu wasiojulikana wakiwa kwenye gari yenye vioo vyeusi walimchukua mzombemzobe na kumwingiza ndani na kuondoka kwa mwendo wa kasi kuelekea barabara ya Mbeya,” amesema.
Chaula anasema kimsingi tangu tukio hilo litokee amekuwa anaishi maisha ya kuugua shinikizo la damu kutokana na msongo wa mawazo, kwani alimpenda mwanaye na alikuwa msaada kwake.
“Ombi langu Serikali inisaidie nijue yuko wapi? Kama ameuawa nijue kaburi lake liko wapi? Kama amefungwa nijue yuko gereza lipi kuliko maisha haya ninayoishi bila kujua hatima ya kijana wangu,” amesema.
Akieleza juhudi walizofanya kifamilia, Chaula amesema wamefuatilia ofisi za upelelezi za Jeshi la Polisi na maeneo mengine bila mafanikio yoyote.
“Kuna wakati nawaza huenda hawakuridhishwa na hukumu iliyotolewa au watu wasiojulikana wamefanya yao, ni vyema likawekwa wazi, kama amefariki au amehukumiwa nielezwe yuko gereza gani nikamuone mwanangu,” amesema mzee huyo.
Mbali na mzazi huyo, ndugu wa karibu wa Shadrack ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, amesema walijaribu kumshauri Mzee Chaula kutumia njia za jadi kumtafuta, lakini amekataa na akieleza anamwamchia Mungu.
Akizungumza na Mwananchi leo Novemba mosi 2024 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema bado wanafuatilia suala hilo.
“Unajua sikuwepo ndio nimefika ofisini, naomba nifuatilie kujua wenzangu wamefikia wapi ili nitoe majibu sahihi,” amesema Kuzaga.