Maftah aipa Pamba watatu | Mwanaspoti

BEKI wa zamani wa Yanga na Simba, Amir Maftah amesema Pamba Jiji ilikosea hesabu zake kwenye usajili wa dirisha kubwa ambao anaamini haukuzingatia mahitaji ya kiufundi, bali msukumo wa kisiasa na haishangazi kwa matokeo wanayoendelea kuyapata kwenye Ligi Kuu Bara.

Maftah alishauri klabu hiyo kufanya maboresho kwenye dirisha dogo kwa kusajili wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kufanya uamuzi katika eneo la ushambuliaji ambalo limekuwa butu, kiungo na ulinzi ambako kunavuja na kuruhusu mabao katika michezo mingi.

Pamba Jiji ambayo iliachana na benchi lake la ufundi na kubakiza wachezaji saba walioipandisha daraja, haijashinda mchezo wowote wa Ligi Kuu Bara kati ya 10 iliyocheza ikipoteza mitano na sare tano, huku ikiruhusu mabao 12 na kufunga matatu.

Tayari timu hiyo imeshafanya mabadiliko ya benchi  la ufundi ililoanza nalo msimu kwa kuachana na kocha Mkuu, Goran Kopunovic na wasaidizi wake, Salvatory Edward, Razack Siwa (kocha wa makipa) na Cirus Kakooza (kocha wa viungo) huku nafasi zao zikizibwa na Fredy Felix ‘Minziro’ na Mathias Wandiba.

“Sishangai kuona Pamba hawafanyi vizuri, nililiona litakuja kutokea mbeleni kwa sababu walisajili kienyeji na kimaficho bila kushirikisha watu wenye uzoefu na taaluma. Kwa hiyo hawakupata wachezaji wazuri wa kuisaidia timu yetu,” alisema Maftah.

“Wajaribu kuangalia usajili mzuri ambao utaleta nguvu katika kikosi kwa sababu raundi ya kwanza inakwenda ukingoni, tuwe na wachezaji wenye uwezo zaidi ya waliopo kuipigania timu itoke kwenye janga la kushuka daraja kwa sababu tunakoelekea ni kugumu zaidi kuliko tulipotoka,” alisema.

Maftah mwenye leseni ya ukocha, alisema akipatikana mshambuliaji mwenye matumizi mazuri ya nafasi, kiungo wa kusambaza vyema mipira na beki kiongozi kwenye safu ya ulinzi, timu hiyo itashindana na kujinusuru isishuke daraja katika mzunguko wa pili.

“Maeneo hayo yameonyesha mapungufu tufanye usajili mzuri utakaoleta chachu na hamasa ya kupata ushindi. Mwalimu na benchi la ufundi wako vizuri tupate wachezaji ukomavu na wazoefu wa ligi yetu, hapo tutainusuru timu,” alisema Maftah.

Related Posts