Atahadharisha usawa wa kijinsia kwenye ndoa

Dodoma. Wanawake nchini wametakiwa kutafsiri vizuri kuhusu usawa wa kijinsia kwamba haina maana mke kumdharau mume akitaka usawa ndani ya ndoa.

Hayo yamesemwa jana na Mkuu wa dawati la jinsia na watoto Mkoa wa Dodoma Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Christer Kayombo, alipokuwa akitoa mada wakati wa uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia katika jamii.

“Ndoa zisipokuwa vizuri zinaibua mgogoro katika ndoa na kusababisha ukatili hadi kwa watoto. Wanawake wawaheshimu waume zao, vitabu vyote vya dini vinasema mwanaume ni kichwa cha familia, tuwe wapole,” amesema Kayombo.

Amesema suala la nafasi za uongozi 50 kwa 50 kwa wanawake lisiingizwe kwenye ndoa, kwamba mwanamke akipeleka suala la usawa wa kijinsia ndani ya ndoa anasababisha mgogoro unaozaa ukatili, hivyo waume wapewe nafasi zao kwenye ndoa kama hawafanyi ukatili.

Pia, Kayombo amesema wanandoa wanatakiwa kuwa na malezi bora kwa watoto wao ili watoto wawe na maadili mema.

“Changamoto iliyopo wazazi badala ya kutoa maelezi wao wanatoa matunzo na matokeo yake watoto wanaharibika kwa sababu ya kukosa malezi bora,” amesema.

 Kwa upande wake Mkurugenzi wa taasisi ya Bule Crooss Soociety of Tanzania,  Revocatus Nginila amemuomba Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalimu, Mwanaidi Ali Khamis asaidie kushughulikia ukatili aliofanyiwa mtoto mwenye umri wa miaka 13 huko Kyela mkoani Mbeya.

Nginila amedai mtoto huyo alikakatwa koromeo na shangazi yake lakini alipata msaada wa Kanisa la Moravian kwa kupatiwa matibabu na amerejea shuleni kwa ushirikiano na Serikali.

“Kwa pamoja tunajiandaa kwa siku 16 za kupinga ukatili ambazo huanza kila mwaka tarehe 25 Novemba. Mwaka huu, maandalizi haya yamefanywa mapema ili kutoa nafasi kwa uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika tarehe 17 Novemba,” amesema Nginila.

Pia, amesema changamoto zilizopo ni mitizamo hai ya jamii kuhusu usawa wa kijinsia imeathiri juhudi za mabadiliko, waathirika wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu haki zao na taratibu za kisheria na uwepo wa hofu ya usalama nayo imezuia baadhi ya waathirika na mashahidi kutoa taarifa za matukio ya ukatili.

Kwa upande wake,  Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalimu, Mwanaidi Ali Khamis amesema Serikali imeanzisha kamati za kupambana na vitendo vya ukatili wa jinisia kwenye halmashauri, vyuoni na kwenye masoko.

Alizitaka taasisi zisizo za kiserikali kusaidiana na Serikali katika kusambaza elimu ya kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia vijijini.

Naye Yohana Shekimweri ofisa maendeleo ya jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalimu amesema wizara imeanzisha madawati ya kupinga ukatili vyuoni na kwenye maeneo ya umma ambapo jumla ya masoko 187 nchini yana madawati hayo.

Kwa upande wake ofisa kutoka taasisi ya Bule Crooss Soociety of Tanzania, Anna Panga amewataka wanaotoa  elimu ya masuala ya jinsia kutumia maneno yanayoleta  nguvu na  hamasa kwa wanaume, badala ya kuwakatisha tamaa kwa kuwatuhumu zaidi.

Related Posts