BAADA ya kuambulia pointi tatu ugenini, Kocha Mkuu wa KMC, Abdihamid Moalin amesema ana siku tatu kuendelea kuboresha ubora wa kikosi kabla ya kuivaa Simba, Novemba 4.
KMC iliyopo nafasi ya sita ikikusanya pointi 14 katika mechi 10, itakuwa ugenini kuvaana na Simba iliyo nafasi ya tatu kabla ya mchezo wa jana. Mechi hiyo itapigwa baada ya KMC kumalizana na Namungo FC juzi ikishinda kwa bao 1-0 ugenini.
Akizungumza na Mwanaspoti, Moallin alisema wanatambua ubora wa Simba, lakini hilo haliwatishi kwani hata wao wana malengo makubwa ya kuhakikisha wanakusanya pointi kwenye kila mchezo ili kufikia malengo ya kumaliza tano bora.
“Nina kazi kubwa ya kufanya ndani ya siku tatu hizi kwa kuongeza ubora wa wachezaji wangu waweze kutumia nafasi wanazotengeneza na kuongeza umakini kwenye eneo la ulinzi ili kujiweka kwenye mzani mzuri wa kutoruhusu mabao kwenye kila mchezo,” alisema Moallin aliyewahi kuinoa Azam FC.
“Tumesharudi na timu inaendelea vizuri ipo kwenye morali nzuri kuhakikisha inakusanya pointi kwenye kila mchezo ulio mbele yetu mbinu sahihi na maandalizi mazuri yatatupa nafasi ya kuwa bora zaidi ya mpinzani wetu.
“Simba ina kocha mzuri na ana mbinu bora za kumkabili mpinzani tumewasoma na tunaendelea kuwafuatilia kujua upungufu na ubora wao kabla ya kuvaana nao kwenye mchezo ujao. Yimu yao imebadilika aina ya uchezaji na imekuwa bora maeneo mengi hilo tayari tumeanza kulifanyia kazi.”
Alisema ana imani na kikosi chake, licha ya mechi za karibuni kushindwa kupata matokeo mazuri, amefanyia kazi makosa aliyoyaona na sasa anapambana kusuka mbinu.
KMC kwenye mechi 10 ilizocheza imeshinda mechi nne, sare mbili na vipigo viwili na kwenye mechi tano za karibuni imeambulia sare mbili na vichapo vitatu.