Mjumbe aeleza jinsi Sinodi ilivyoridhia, Askofu Sepeku apewe zawadi

Dar es Salaam. Aliyekuwa mjumbe wa kikao cha Sinodi cha Kanisa la Anglikana Tanzania, kilichoketi Machi 1980, Ernest Mwenewanda(79), amedai kuwa aliyekuwa Askofu Mkuu wa kwanza wa kanisa la Anglikana Tanzania, marehemu John Sepeku, alikuwa na upendo kwa waumini wa wake,  hali iliyosababisha hata kanisa lilipopendekeza apewe zawadi, hakuna mjumbe yeyote aliyepinga uamuzi huo.

Mwenewanda ambaye kwa sasa ni mfanyabiashara na mkazi wa Mikocheni, ametoa maelezo hayo jana Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi, wakati akitoa ushahidi katika kesi ya ardhi iliyofunguliwa na mtoto wa Sepeku, Bernardo Sepeku dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Anglikana Tanzania,  Askofu Jackson Sostenes wa kanisa hilo pamoja na Kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd.

Bernado, alifungua kesi hiyo ya ardhi namba 378/2023, akipinga kunyang’anywa zawadi ya kiwanja alichopewa baba yake mwaka 1978 na kanisa hilo.

Sepeku alipewa zawadi na kanisa hilo ambayo ni  nyumba iliyopo Buguruni na kiwanja chenye ukubwa wa ekari 20 kilichopo Buza, wilayani Temeke kama zawadi kwa kutambua mchango wake katika kanisa hilo, kama Askofu wa Mkuu wa kwanza kanisa hilo.

Bernardo katika kesi hiyo, anadai alipwe Sh3.72bilioni ambayo ni fidia ya hasara ya kifedha iliyopatikana kutokana na uvamizi wa mali ya ardhi katika kiwanja hicho.

Pia anaiomba alipwe fidia ya Sh493.65 milioni ambayo ingepatikana baada ya kukomaa kwa  mavuno ya mazao yaliyokuwepo kwenye shamba hilo.

Hata hivyo, wakati kesi hiyo ikiendelea na usikilizwaji, mdaiwa wa  tatu katika shauri hilo, kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd, hajawahi kufika mahakamani hapo tangu kesi hiyo ilipofunguliwa licha ya kupokea wito wa kuitwa mahakamani.

Akiongozwa kutoa ushahidi wake na wakili Deogratias Butawantemi, mbele ya Jaji Arafa Msafiri, Mwenewanda alidai kuwa Machi 8 na Machi 9, 1980 kulifanyika mkutano mkuu wa Sinodi ambapo pamoja mambo mengine ulipendekeza Askofu Sepetu apewe zawadi, baada ya kustaafu utumishi wake.

Mwenewanda ambaye ni shahidi wa nne wa upande wa mlalamikaji, alidai kuwa mkutano huo ulikuwa ni mahususi kwa ajili ya mapendekezo ya kutoa zawadi kwa askofu Sepetu ambaye alikuwa askofu wa kwanza mkuu tangu kuanzishwa kwa kanisa hilo mwaka 1970.

“Katika mkutano huo, mimi nilikuwa ni mjumbe namba tano kwenye nyumba ya walei na kikao kilipitisha askofu Sepeku apewe zawadi ya ekari 20 za shamba ili aende kujiendeleza kwa kuwa alikuwa anaelekea kustaafu,” amedai Mwenewanda na kuongeza

“Pia kikao hicho kilielekeza Sepeku ajengewe nyumba Buguruni na baada ya mapendekezo hayo kutolewa na kikao hicho, hakuna mtu aliyepinga au kuweka zuio juu ya mapendekezo hayo” alidai

Amedai kuwa baada ya mapendekezo hayo kufanyika, kanisa lilitekeleza mapendekezo hayo na askofu Sepeku alijengewa nyumba Buguruni na kupewa ekari 20, ambazo familia yake ilikuwa inalima mazao mbalimbali.

“Mheshimiwa Jaji, askofu Sepeku alifanya kazi kubwa sana na alikuwa na upendo kwa waumini wake na ndio maana hata sinodi ilipopendekeza apewe zawadi, hakuna mtu yeyote aliyepinga” alidai.

Shahidi huyo aliomba maelezo yake yapokelelewa na mahakama yawe sehemu ya kielelezo katika kesi hiyo, ombi ambalo halikupingwa na upande wa mdaiwa wala mahakama.

Baada ya kumaliza kutoa ushahidi, wakili wa mdaiwa wa kwanza na wa pili katika kesi hiyo, Dennis Malamba alimuuliza maswali ya dodoso Mwenewanda na haya ni baadhi ya maswali aliyohojiwa.

Wakili: Shahidi ni kweli wewe ulikuwa mmoja wa watu waliohudhuria mkutano Mkuu wa Sinodi?

Wakili: Mkutano Mkuu uliitwaje?

Wakili: Huo mkutano wa Sinodi una uwezo wa kutoa zawadi kwa mali ambayo sio yake?

Wakili: Shamba ambalo tunabishania leo hapa mahakamani, lipo eneo gani

Wakili: Shahidi, kwa sababu ulihudhuria huo mkutano, hilo shamba lina hati ya nani?

Shahidi: Dayosisi ya Dar es Salaam.

Wakili: Na kwenye hii kesi, Dayosisi ya Dar es Salaam, imeshtakiwa?

Shahidi: Sijaona Dayosisi ya Dar es Salaam.

Wakili: Unafahamu kanisa la Anglikana Tanzania lina Dayosisi 28? unaweza kuzitaja?

Shahidi: Nazifahamu zipo nyingi ila silazimishwi kuzikariri kama amri 10 za Mungu.

Wakili: Unafahamu kazi hizo 28, ni Dayosisi mbili tu ndio zina bodi ya wadhamini?

Wakili: Hicho kikao cha Sinodi, nani alikuwa mwenyekiti?

Shahidi: Mwenyewe askofu Sepeku

Wakili: Na aliyepewa zawadi alikuwa ni nani?

Wakili: Kwa hiyo Sepeku alisimamia kikao kilichompa zawadi, ni sahili?

Wakili: Kwa hiyo kusema waumini wa Dar es Salaam walikaa na kumpa zawadi, hayo maneno tuyaache kuyasema hapa mahakamani.

Baada ya kumaliza kutoa ushahidi huo, jaji Msafiri aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 16, 2024 saa 4: 00 asubuhi itakapoendelea.

Tayari mashahidi wanne wameshatoa ushahidi wao dhidi ya Kanisa hilo na miongoni mwao ni Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Newala, Oscar Mnung’a, ambaye alidai kuwa bodi ya Wadhamini ya Kanisa hilo, haina Mamlaka ya kutengua au kubadilisha maamuzi yoyote yaliyofanywa na kikao cha Sinodi.

Sinodi ni mkutano mtakatifu ambao unajumuisha askofu, mapadri, waumini kwa ajili ya kutoa maamuzi mbalimbali yanayohusu kanisa na maamuzi yanayotolewa katika mkutano huo, hayapingwi sehemu yoyote.

Pia, alidai Katiba ya mwaka 1970 ya Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Dar es Salaam ilibariki Askofu Mkuu wa kwanza wa kanisa hilo, marehemu John Sepeku, apewe ekari  20 kama zawadi, lakini ameshangaa kuona mali hiyo imemegwa na amepewa Mchina.

Shahidi huyo ambaye ni mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Anglikana, alidai maamuzi ya kikao cha Sinodi  yaliyofanyika mwaka 1978 na Kamati ya Kudumu ya Dayosisi ya Dar es Salaam, yalipendekeza John Sepeku apewe ekari 20 kama zawadi na pia kamati hiyo ilipendekeza kanisa hilo litoe ekari sita kwa Chama cha Viziwi Tanzania, mapendekezo ambayo yalifanyiwa kazi.

Mnung’a ambaye ni shahidi wa pili wa upande wa mlalamikaji, alidai kuwa kikao cha Sinodi kina uwezo wa kutoa mali na kumpa mtu kwa mujibu katiba.

“Hapa nimekuja mahakama kutoa ushahidi wa upande wa familia ya Sepeku na sio kwa niaba ya Bodi ya Wadhamini” alidai Askofu Mnung’a, ambaye ni askofu kwa muda wa miaka 17 sasa.

“Mheshimiwa Jaji na kwa faida ya Mahakama, maamuzi ya Sinodi hayawezi kupingwa na Askofu yoyote, kwa kuwa yalikuwa ni maamuzi halali” alidai Mnung’a na kuongeza

“Na kwamba, Bodi ya Wadhamini ya Kanisa la Anglikana haina Mamlaka ya kutoa mali yoyote iliyopo katika Dayosisi ya Dar es Salaam” alidai

Alifafanua kuwa kazi ya Bodi ya Wadhamini ya kanisa hilo ni kulinda na kusimamia mali zote za Dayosisi pamoja na kuheshimu maamuzi yote ya vikao vilivyofanyika.

Related Posts