Arusha. Mahakama ya Rufani imemuachia huru, Yustine Robert aliyehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kutiwa hatiani kwa kumuua mkewe na watoto wake wawili.
Robert alihukumiwa adhabu hiyo na Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, Julai 13, 2020 kutokana na kesi ya mauaji iliyokuwa ikimkabili akidaiwa kumuua mkewe, Jackline Yustine na watoto wao Frank (6) na Elizabeth (4).
Hukumu ya rufaa namba 299 ya 2020 iliyomuachia huru imetolewa Oktoba 29, 2024 na jopo la majaji wa Mahakama ya Rufani Barke Seleh, Dk Paulo Kihwelo na Gerson Mdemu.
Majaji walifikia uamuzi huo baada ya kupitia mwenendo wa kesi na kusikiliza hoja za mawakili na kubaini ushahidi wa kimazingira uliozingatiwa katika hukumu ya Mahakama Kuu haukuweza kumuunganisha mrufani na tukio la mauaji ya familia yake.
Katika ushahidi mahakamani, ilidaiwa Aprili 6, 2013 saa saba mchana Jackline alikutwa amezama kisimani akiwa hai lakini dhaifu sana na aliopolewa pamoja na maiti mbili za watoto.
Kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa mashtaka, Robert aligombana na mkewe akamfukuza akimtaka aondoke na vitu vyake vyote.
Inadaiwa alipokuwa akiondoka alivunja jagi la mumewe, jambo lililompa hasira Yustine aliyemtisha kuwa jambo atakalofanya litakuwa historia katika eneo hilo.
Katika Kijiji cha Majimoto, Jackiline inadaiwa kwa kutumia ishara alieleza kuna watu zaidi kisimani ndipo walipogundulika watoto wakiwa wameshafariki dunia.
Inadaiwa siku ya tukio saa moja asubuhi, mtoto wa kike mwenye umri wa miezi minne alikutwa ametelekezwa kwenye makutano ya barabara, hivyo balozi wa nyumba kumi eneo la Majimoto ambaye alikuwa shahidi wa pili, Edwin Nkolo alifika eneo hilo ambako pia kulikuwa na karatasi zilizokunjwa, kanga, na kipande cha pazia.
Mtoto huyo alitambuliwa kuwa wa mrufani na Jackline hivyo kuashiria kulikuwa na tatizo.
Shahidi wa kwanza alidai Aprili 5, 2013, mrufani na familia yake walikuwa wakiishi katika nyumba yake walikopanga.
Alidai siku ya tukio alisikia wakigombana na mume akimfukuza mkewe akimtaka achukue vitu vyake arudi kwa wazazi wake na aache jagi ambalo mke alilivunja.
Alidai mume huyo alimpiga teke na kumwambia kuwa: “Kwa kunivunjia jagi langu, tukio nitakalolifanya Majimoto ni historia.”
Shahidi alidai aliingilia kati na kuwatuliza kisha akaondoka kwenda kumsindikiza mgeni wake na aliporejea hakuwakuta. Baadaye alimuona mume akirudi nyumbani peke yake na alipomuuliza mkewe alipo alimjibu hajui.
Alidai asubuhi ya siku iliyofuata alifahamishwa na balozi kuhusu mtoto mchanga aliyeachwa barabarani, hivyo walienda kumchukua na jioni walikuta maiti za watoto kisimani na mama yao alipelekwa Kituo cha Afya Mamba na alifariki dunia Aprili 7, 2013.
Robert alikamatwa na kufikishwa mahakamani akishitakiwa kwa makosa matatu ya mauaji ambayo aliyakana.
Alidai Aprili 5, 2013 aliporejea kutoka kazini, aligundua kuwa baadhi ya samani za nyumbani hazipo.
Robert alidai alikuta kitanda na godoro pekee na alipomuuliza mkewe nini kimetokea alimweleza vitu vimehifadhiwa nyumbani kwa shahidi wa kwanza.
Alidai alimtaka arudishe vitu hivyo na akafanya hivyo, pia aliandaa chakula cha jioni wakala na kulala. Alieleza asubuhi alipoamka mke hakuwepo nyumbani.
Alidai hakumuulizia akaenda kwenye shughuli zake za kuuza maji hadi alipokamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi Majimoto.
Baada ya ushahidi wa pande zote, jaji wa Mahakama Kuu alimtia hatiani kwa ushahidi wa mazingira na kumuhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
Ushahidi wa kimazingira uliotumika ni kushuhudiwa ugomvi kati ya wanandoa hao, maneno yaliyotamkwa baada ya Jackline kuvunja jagi na mwenendo wa mrufani kutomfuatilia mkewe baada ya kubaini hayupo
Katika rufaa, Robert aliyetetewa na Wakili Baltazar Chambi, alikuwa na sababu tatu akidai mahakama ilikosea kisheria kumtia hatiani wakati upande wa mashtaka hauthibitisha kosa kwa kiwango kinachotakiwa.
Nyingine ni mahakama ilifanya makosa kisheria kumtia hatiani kwa kosa aliloshtakiwa nalo bila kuzingatia utata na kutofautiana ushahidi wa mashtaka, na mahakama kukosea kumtia hatiani kwa kutegemea ushahidi wa kimazingira bila kuzingatia masharti.
Jaji Sehel katika uamuzi wa rufaa amesema ni msingi wa kisheria kuwa upande wa mashtaka una wajibu wa kuthibitisha kosa linalomkabili mshitakiwa ambapo katika kesi hiyo upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi wanne na vielelezo vitatu ambavyo ni ripoti za kifo za Frank na Elizabeth.
Ripoti ya kifo cha Jackiline na ramani ya mchoro wa eneo la tukio havi kutolewa na Jamhuri mahakamani.
Jaji alieleza kwa kuzingatia mawasilisho ya pande zote na kupitia kumbukumbu za kesi hiyo ikiwa hiyo ni rufaa ya kwanza, Mahakama ina haki ya kutathmini upya na kupitia upya ushahidi uliotolewa mbele ya mahakama ya awali.
Akinukuu mashauri kadhaa alieleza katika rufaa hiyo
wataangalia masuala matatu ambayo ni ugomvi unaodaiwa kuibuka baina ya wanandoa hao, maneno yaliyotamkwa na mwenendo wa mrufani baada ya kukuta familia yake haipo nyumbani.
“Kwanza, tulikusanya kutoka kwenye rekodi ya rufaa kwamba kwa hakika kulikuwa na ugomvi kati ya mrufani na mke wake ambao ulishuhudiwa na shahidi wa kwanza na kuungwa mkono na mrufani ila ugomvi huo
ulitatuliwa usiku huohuo.
“Baada ya ugomvi kutatuliwa kwa amani hakukuwa na kitu kinachounganisha kifo na mapigano, kwa hiyo tunaona kwamba Jaji alielewa kwa makosa aliposhikilia kwamba kulikuwa na mlolongo wa matukio ambao haukuweza kuthibitisha hatia kwa mrufani,” amesema.
Jopo hilo limesema katika hali hiyohiyo, hawaoni uhusiano wowote na maneno yanayodaiwa kutamkwa na mrufani, ikiwa ni maneno ya aina hiyo na mke kukutwa amezama kwenye kisima cha maji.
Amesema mrufani hakukimbia, ikiwa ni yeye aliyemuua mkewe na familia yake, ushahidi unaonyesha alikamatwa katika kituo chake cha biashara cha kawaida.
“Yote kwa yote, tumeridhika kwamba ukweli hauelekei kwenye mrengo wa hatia kwa upande wa mrufani bali kuna mashaka tu,” amesema.
“Kwa kuzingatia kwamba sababu hizi mbili za kukata rufaa zinatosha kuondoa rufaa yote, tunaona kwamba mrufani alitiwa hatiani kimakosa kwa kosa la mauaji, huku kukiwa hakuna mnyororo unaomhusisha na mauaji ya familia yake,” amesema.