Dar es Salaam. Kutoweka katika mazingira ya kutatanisha kwa Mkurugenzi wa Dar24 Media, Maclean Mwaijonga kumeongeza kilio cha kuongezwa kazi ya uchunguzi wa matukio ya watu kupotea au kutekwa nchini.
Mwaijonga alitoweka Alhamisi Oktoba 31, 2024 alipotoka ofisi za Datavision International Ltd, zilizopo Mikocheni jirani na Rose Garden saa 11:00 jioni na hadi leo hajaonekana.
Taarifa iliyotolewa Novemba 2, 2024 na mmoja wa viongozi wa Datavision International Ltd, William Kihula kupitia mitandao ya kijamii, imesema Mwaijonga ambaye pia ni mtendaji mkuu wa kampuni hiyo, hana kawaida ya kutorudi nyumbani lakini mpaka sasa hajapatikana.
“Wakati akitoka ofisini alikuwa na gari aina ya Toyota Prado nyeusi yenye namba za usajili T 645 DEE,” amesema Kihula katika taarifa.
Moses Mwaijonga, aliyejitambulisha kwa Mwananchi ni mdogo wa Maclean, amesema tangu kaka yao alipotoweka walianza ufuatiliaji na hadi leo hawajapata mafanikio.
“Juzi (Oktoba 31) baada ya kutoka ofisini kwa sababu huwa ni mtu wa diet (anayejinyima chakula), alikwenda kwa wakala wa fedha, akatoa Sh10, 000 kisha akanunua karanga. Tumeuliza, pale wakasema baada ya kununua karanga akampa kijana mmoja pale, lakini yule kijana alisema anakula biskuti, basi jamaa akaondoka zake.
“Alipotoka pale tunaambiwa alikwenda kwenye ofisi inayoitwa Windhoek hapohapo Mikocheni karibu na shule ya Feza, huenda alikwenda tu kwa biashara zake, lakini tumefuatilia pale wanasema hawajui lolote,” amesema.
“Tumeomba kuangalia picha za CCTV wanasema mhusika hayupo, mpaka Jumatatu,” amesema.
Moses amesema baadaye walikwenda kufungua jalada Kituo ha Polisi Oysterbay.
“Leo siku nzima tuko hapa Polisi Oysterbay wametuhoji tumewapa taarifa na bado tuko hapa,” amesema alipozungumza na Mwananchi saa 9:36 alasiri.
Akizungumzia tukio hilo leo Novemba 2, 2024, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema wamepata taarifa ya tukio hilo na wameanza uchunguzi.
“Hiyo taarifa na mimi nimeiona, kwa hiyo na mimi nafuatilia. Ndugu walikuja wakatwambia nini na nini, lakini tukimwangalia sisi hatuna rekodi naye za criminality (uhalifu), kwa hiyo na sisi tunafuatilia,” amesema.
Tukio hilo linaongeza idadi ya matukio ya watu kupotea na wengine kudaiwa kutekwa nchini, huku Jeshi la Polisi likilaumiwa kuchelewa kukamilisha uchunguzi.
Tukio hilo, limekujwa ikiwa imepita miezi miwili tangu kutoweka msanii wa uchoraji, Shadrack Chaula (24) ambaye baba yake mzazi, Yusuph Chaula (56) ameiomba Serikali kufanya uchunguzi wa kina kujua aliko mwanaye.
Shadrack alitoweka baada ya kuchukuliwa na watu wasiojulikana Agosti 2, 2024 saa 2:30 asubuhi akiwa katika eneo la biashara zake kwenye Kijiji cha Ntokela wilayani Rungwe, Mkoa wa Mbeya.
Kabla ya tukio hilo, Julai 3, 2024 Shadrack alishikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kosa la kuchoma picha ya kuchora ya Rais Samia Suluhu Hassan, kutokana na video iliyosambaa mitandaoni ikionyesha tukio hilo.
Julai 5, 2024, alishtakiwa na kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela au kulipa faini ya Sh5 milioni katika Mahakama ya Wilaya ya Rungwe.
Wanaharakati na watumiaji wa mitandao ya jamii walimchangia na kulipa faini hiyo, hivyo kumwezesha kutoka jela Julai 8, 2024.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu Oktoba 31, 2024, Yusuph amesema familia wanakiri kijana wao alitenda kosa lakini alishalipiwa faini ya Sh5 milioni na wasamaria wema na siku kadhaa baada ya kutoka gerezani alikabidhiwa kwake kupitia mwanasheria wake, Michael Mwangasa.
“Zilipita wiki mbili watu wasiojulikana wakiwa kwenye gari yenye vioo vyeusi walimchukua mzobemzobe wakamwingiza ndani na kuondoka naye kwa mwendo wa kasi kuelekea barabara ya Mbeya,” amesema.
Amesema tangu tukio hilo litokee amekuwa anaishi maisha ya kuugua shinikizo la damu kutokana na msongo wa mawazo, kwani alimpenda mwanaye na kijana huyo alikuwa msaada kwake.
“Ombi langu Serikali inisaidie nijue yuko wapi? Kama ameuawa nijue kaburi lake liko wapi? Kama amefungwa nijue yuko gereza lipi kuliko maisha haya ninayoishi bila kujua hatima ya kijana wangu,” amesema.
Hayo yanatokea wakati ambao tayari Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (TBUB), inayoongozwa na Jaji Mathew Mwaimu imetangaza kuzunguka mikoa 15 ya Tanzania Bara yalikotajwa matukio yapatayo 80 ya watu kupotea ili kutafuta ukweli wake.
Pia, Agosti 9, 2024 Baraza la Uongozi la Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) lilitoa tamko likilalamikia ongezeko la vitendo hivyo na kutoa orodha watu 83 waliotoweka.
Alipoulizwa swali kuhusu uchunguzi wa matukio ya watu kutoweka na wengine kudaiwa kutekwa leo Novemba 2, 2024, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime amemtaka mwandihsi kumwandikia ujumbe, ambao hata hivyo hakujibiwa.
Lakini Kamanda Muliro alipoulizwa amesema majibu yote alishayatoa kwenye kongamano la Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) lililofanyika Dar es Salaam Oktoba 5, 2024.
Katika kongamano hilo, Muliro alisema Jeshi la Polisi linatumia kifungu cha 5(2) cha Sheria ya Polisi na Polisi Wasaidizi kupambana na matukio hayo.
“Moja ya jukumu la majukumu ya polisi ni kuhakikisha usalama wa watu; watu wanakuwepo, wanaishi, wanafanya shughuli zao kwa mujibu wa Katiba na kama yatatokea matukio ya watu kupotea na utekaji ndiyo jukumu la polisi linapokuja katika kifungu hicho.
“Kwanza kwa nini wamepotea, wako wapi sababu zipi zimefanya wapotee, kwa hiyo jukumu la upelelezi,” amesema.
Alipoulizwa katika kongamano hilo kuhusu kutoweka kwa makada wa Chadema, Deudedith Soka na wenzake, Muliro alisema kwa rekodi alizonazo yapo matukio 37 ya watu kutekwa na kupotea.
“Nataka kukueleza, zaidi ya watu 37 ambao wamekumbwa na kadhia hii kuanzia mwaka 2018 tumeshapata majibu yake, baadhi ya watu walikamatwa na kupelekwa mahakamani na baadhi ya watu waliodaiwa kutekwa na wengine kupotea tulikuta wamekufa na tulipata sababu za wao kufa, na mara kadhaa ilipotokea tumekuwa tukiyatolea taarifa kwenye vyombo vya habari,” alisema.
Alipoulizwa sababu ya matukio hayo kuwalenga watu wa vyama vya upinzani, alikanusha.
“Sisi wachunguzi kwanza hatukubaliani na mtazamo huo, kuna visa 46 tulivyochunguza si watu wa Chadema, bali ni wa vyama mbalimbali wametekwa,” alisema.
Miongoni mwa matukio ya hivi karibuni yanayodaiwa kuwa ni ya utekaji ni pamoja na la kiongozi wa Chadema, Ally Kibao, ambaye alishushwa na watu kwenye basi la Tashrif eneo la Tegeta Kibo, Dar es Salaam saa 12.00 jioni ya Septemba 6, mwaka huu akiwa safarini kwenda Tanga.
Siku iliyofuata Septemba 7, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alizungumza na waandishi wa habari kuhusu taarifa alizozipata za kada huyo kutekwa, kabla ya mwili wake kupatikana katika Hospitali ya Mwananyamala na Septemba 8, ikielezwa uliokotwa maeneo ya Ununio.
Kutokana na tukio hilo, Rais Samia Suluhu Hassan kupitia ukurasa wake wa X (zamani twitter), aliviagiza vyombo vya usalama kufanya uchunguzi wa kina na kumpatia taarifa.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Misime akizungumzia tukio hilo Jumapili Septemba 8, 2024, alisema uchunguzi unaendelea.
“Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi mkali na timu kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai imetumwa kuongeza nguvu ili kuhakikisha waliofanya mauaji hayo wanapatikana na kufikishwa mahakamani,” alisema.
Hata hivyo, hadi leo hakuna taarifa yoyote iliyotolewa kuhusu uchunguzi huo.
Oktoba 20, 2024 Katibu Mwenezi wa Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bawacha) Taifa, Aisha Machano naye alidaiwa alitekwa, kupigwa na kutupwa porini wilayani Kibiti, mkoani Pwani.
Misime pia alikiri jeshi hilo kupokea taarifa ya tukio hilo na tayari uchunguzi wa jambo hilo umeanza mara moja kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.
Tukio jingine ni Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) Wilaya ya Temeke, Deusdedit Soka na Katibu wake, Jacob Mlay na Frank Mbise ambaye ni dereva wa bodaboda walitoweka tangu Agosti mwaka huu.
Wakili Paul Kisabo alifungua shauri mahakamani akiomba vijana hao waachiwe au wapelekwe mahakamani.
Mahakama Agosti 29, 2024 ilisema maombi yaliyowasilishwa mahakamani kuomba Soka, Mlay na Mbise hayajathibitishwa kupitia kiapo kama ushahidi kwamba wanashikiliwa na jeshi hilo.
Mahakama iliitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi ili kujua waliko vijana hao.
Akiuzngumzia masuala hayo, Wakili Kisabo ameshauri kuundwa kwa tume huru ya kuchunguza matukio ya watu kupotea au kutekwa kwa kuwa baadhi ya matukio yanalihusisha Jeshi la Polisi.
“Serikali inapaswa kuunda tume huru ambayo itafanya uchunguzi wa haya matukio ya watu kutekwa na kupotea, kwa sababu kuna baadhi ya matukio polisi wametuhumiwa na kwa hiyo hawawezi kujichunguza, kwa sababu kuna uwezekano mkubwa wa kujipendelea.
“Kwa hiyo Rais aunde tume huru au awaalike wachunguzi huru, kwa mfano Scotland Yard ya Uingereza. Hapo ndipo taarifa zinaweza kuwa za uhakika,” amesema.
Amesema licha ya kuwepo kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, bado kunaweza kusiwe na uhuru wa kutosha.
“Tunachosema sisi ni tume ya kijaji ambayo haiwezi kuingiliwa na mtu yeyote. Tatizo la polisi wanatuhumiwa kwa baadhi ya matukio, hata ukiwa wewe unatuhumiwa kwa tukio halafu unajichunguza lazima utajipendelea.
“Ndio maana unaona haya mambo yanasuasua na ripoti hazitoki kwa wakati,” amesema.