KIPA wa Dodoma Jiji Mkongomani Alain Ngeleka amesema anategemea mapokezi mazuri wakati kikosi hicho kitakapopambana na Kagera Sugar katika mchezo mkali wa kusisimua wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa kesho, kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
Kauli ya kipa huyo inatokana na kuwahi kuichezea timu hiyo kabla ya kujiunga na Dodoma Jiji msimu huu ambapo anaamini atapata mapokezi mazuri wakati atakaporejea Kaitaba, kwa sababu aliondoka kwa amani na hakuwa na shida na mtu yeyote.
“Niliondoka kwa amani na walinipa baraka zao baada ya kuwambia nimepata sehemu nyingine, nashukuru walinielewa na kuniambia wameridhia ombi langu, tulikuwa pia katika mazungumzo ya mkataba mpya hivyo Kagera ni zaidi ya familia,” alisema.
Ngeleka aliongeza kuwa licha ya wapinzani wao kutokuwa na mwenendo mzuri tangu msimu huu umeanza, lakini wanawaheshimu kutokana na aina ya ubora wa wachezaji waliopo, huku akiwataka nyota wenzake kuhakikisha wanapambana zaidi ili wapate ushindi.
“Kuanza kwao vibaya haina maana hawana wachezaji wazuri, msimu huu umekuwa mgumu sana kwa sababu kila timu imejipanga kwa ushindani, tunaenda ugenini huku tukitarajia kukutana na mechi ngumu kama zilivyokuwa nyingine tulizocheza pia.”
Kipa huyo aliyejiunga na Dodoma Jiji msimu huu akitokea Kagera Sugar, anakumbukwa zaidi ule wa 2022-2023 wakati akiwa na kikosi cha Tabora United zamani Kitayosce, ambapo aliwekea rekodi nzuri ya kufunga bao katika Ligi ya Championship.
Ngeleka alifunga bao pekee la kufutia machozi kwa upande wa Tabora United katika mchezo mkali na wa kusisimua uliopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Mbweni, ambao timu hiyo ilichapwa mabao 3-1, dhidi ya JKT Tanzania Desemba 3, 2022.
Nyota huyo kwa mara ya kwanza alitua nchini na kujiunga na Tabora United wakati inashiriki Ligi ya Championship msimu wa 2022-2023 akitokea klabu ya Lumwana Radiant ya Zambia, ambapo amekuwa ni muhimili mkubwa katika kikosi cha Dodoma Jiji.