KADI nyekundu ya moja kwa moja aliyopewa beki wa kati Ibrahim Bacca dakika ya 21 tu, imeiponza Yanga kupoteza mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara msimu huu mbele ya Azam FC na kutibuliwa rekodi mbalimbali ilizokuwa nazo msimu huu ikiwamo kupoteza uwanja wa nyumbani tangu msimu uliopita.
Yanga iliyokuwa imecheza mechi zaidi ya 50 nyumbani na pia kucheza mechi nane mfululizo za Ligi Kuu msimu huu bila kupoteza wala kuruhusu bao lolote, lakini bao la dakika ya 34 la Gibril Sillah lilitibua kila kitu kwa kocha Miguel Gamondi kwa Azam kuendelea pale ilipoishia msimu uliopita ilipoichapa Yanga 2-1.
Katika mchezo huo uliopigwa kuanzia saa 12:00 jioni kwenye Uwanja wa Azam Complex, Yanga licha ya kupambana kiume kutaka kulinda heshima iliyonayo, ilijikuta katika wakati mgumu mbele ya Wanalambalamba walioamua kutumia mtindo wa kubaki basi hasa kipindi cha pili.
Mapema tu Yanga ilikumbana na pigo baada ya beki wake Ibrahim Hamad ‘Bacca’ kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja dakika ya 21 kufuatia beki huyo kumuangusha mshambuliaji wa Azamm Nassoro Saadun wakati akielekea kufunga.
Mwamuzi Ahmed Arajiga kutoka Manyara ambaye anashikilia tuzo ya mwamuzi bora wa msimu uliopita alisimama imara akimtoa nje Bacca, beki huyo akiifanya timu yake kucheza pungufu.
Wakati mashabiki wa Yanga wakichanganyikiwa na kadi hiyo nyekundu, Bacca mwenyewe aliwaomba radhi mashabiki wa timu yake wakati akitoka nje kuelekea vyumbani huku nao wakimpigia makofi wakiwa na huzuni.
Dakika 12 baadaye alikuwa winga Djibril Silla akiIFUNGIA Azam bao dakika ya 33 kwa shuti kali akifanikiwa kuinasa pasi ya kiungo wake Adolf Mutasingwa.
Hilo ni bao la tatu kwa Silla kuifunga Yanga tangu asajiliwe Azam ambapo aliwaifunga la kwanza mabingwa hao Oktoba 23, 2023 timu yake ikipoteza 3-2 kisha kufunga Machi 17,2024 timu yake ikishinda kwa mabao 2-1.
Azam kwa mara nyingine iliendelea kuzuia rekodi za Yanga ambapo kabla ya mchezo huo mabingwa hao watetezi walikuwa hawajapoteza mchezo wowote wala kuruhusu bao rekodi ambazo zilizuiwa na matajiri hao wa Chamazi.
Yanga kabla ya mchezo huo ilikuwa haijafungwa nyumbani kwa michezo 50 ambapo Azam ikazuia rekodi hiyo ya tatu kwa wenyeji wao. Mapema Aprili 25, 2021 Azam iliizuia Yanga iliyocheza mechi 17 bila kupoteza nyumbani ikishinda mechi 17 lakini mechi ya 18 ikapoteza kwa bao 1-0.
Azam pia ndio ilikuwa timu pekee iliyokuwa imezigusa nyavu za Yanga katika mechi 14 zilizopita za mashindano ambapo wababe hao wa Jangwani ilipobeba Ngao ya Jamii kwa mabao 4-1.
Matokeo hayo yameifanya Yanga kusaliwa na pointi 24 kama ilizokuwa nazo Singida BS iliyokuwa uwanjani usiku wa jana kuumana na Coastal Union, ikiwa na pointi 22 na kama imeibuka na ushindi itakuwa imrejea kieleleni kwa kufikisha pointi 25.