Dar es Salaam. Malik Hashim (6) aliyesota Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa siku 107 akitibiwa koo, sasa amepona kabisa.
Mtoto huyo anayeishi Goba Kinzudi Dar es Salaam, alifikishwa hospitalini hapo Julai 15, mwaka huu baada ya kushambuliwa na kitu chenye ncha kali na mtumishi wao wa ndani.
Akizungumza na Mwananchi Novemba Mosi, Mkuu wa Idara ya Masikio, pua na koo wa MNH, Dk Aslam Nkya amesema kuwa hospitali imekamilisha matibabu yake na sasa anaishi maisha ya kawaida.
Kufuatia shambulio hilo, Malik alifanyiwa upasuaji wa saa tano na timu ya madaktari 12 na baada ya hapo alilazimika kukaa hospitalini kwa siku 25 kwa matibabu zaidi hadi alipotolewa Agosti 7, 2024, lakini aliendelea na matibabu ya kila wiki hospitalini hadi aliporuhusiwa jana.
“Tulimruhusu Malik akiwa na kifaa maalum kinachoitwa ‘tracheostomy’ kwenye koo lake ili kumsaidia kupumua wakati akiendelea na matibabu mengine. Wakati huo mfumo wake wa kupumua ulikuwa bado unahitaji matibabu, ndiyo maana tulimtoa kifaa hicho,” amesema Dk Nkya.
Amesema wakati akiendelea na matibabu ya kila wiki, walilazimika kubadilisha kifaa hicho na kuweka kingine na kufanya upasuaji mdogo kuondoa nyama ambazo huota wakati kidonda kinapona.
Dk Nkya amesema ilikua ni muhimu kufanyika kwa upasuaji huo mdogo, ili kuondoa vinyama vidogo kuepeka kuziba kwa mfumo wa upumuaji.
Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Mohamed Janabi, amesema Malik alipokelewa hospitalini akiwa katika hali mbaya, kwani koo lake lilikuwa limekatwa vibaya karibu ya kuathiri sanduku la sauti.
“Tunamshukuru (Rais Samia Suluhu Hassan) madaktari wetu wa hapa Tanzania kwa kuokoa maisha ya Malik. Hadi sasa, gharama za matibabu zimefikia Sh15 milioni zilizolipwa na Rais,” amesema Profesa Janabi.
Mama yake Malik, Shani Charles, amemshukuru Rais Samia na madaktari na wafanyakazi wote wa MNH kwa kumhudumia mwanawe siku zote alizokuwa hospitalini hapo kwa matibabu.
“Safari ya matibabu haikua rahis bila msaada kutoka kwa Rais na wafanyakazi wa MNH; tusingeweza kufika hapa,” amesema Shani.
Amesema changamoto aliyokutana nayo wakati Malik anatumia ‘tracheostomy’ ilikua ni namna ya kuhakikisha inabaki kwenye hali ya usafi kuepuka maambukizi.
“Tumekua tukija hospitali kila wiki tangu tuliporuhiusiwa na mara tatu tofauti tulipewa kitanda kwa matibabu zaidi japo tulikua hatukai sana.
“Leo rasmi ni siku yetu ya mwisho kwa matibabu ya Malik kwa tatizo hili la koo,” amesema Shani.
Kufuatia tukio la Malik kukatwa koo maisha ya familia ya Malik yamebadilika kwa sababu walilazimika kwenda kuishi sehemu tofauti na kwao ili iwe rahisi kwa Malik kuondoa kumbukumbu ya tukio hilo kwenye akili yake, amesema Shani.
Pamoja na hayo Malik hakuweza kuendelea tena na masomo yake, huku mama yake akilazimika kuacha kazi iliyokua inamwingizia kipato ili apate muda wa kutosha kumhudumia Malik.
Akizungumza na waandishi wa habari Jumatano, Julai 17, 2024 Kamanda wa Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam, Jumanne Muliro, alisema Julai 17, 2024, msako wa kumkamata mtumishi huyo ulifanyika na alikamatwa Julai 22, 2