DKT. BITEKO AHIMIZA UPENDO, AMANI NA USHIRIKIANO SENGEREMA

*Asisitiza wananchi kushiriki Uchaguzi Wa Serikali za Mitaa kwa amani, Sengerema inahitaji maendeleo na si maneno

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amehimiza upendo, amani na ushirikiano miongoni mwa wananchi wa Sengerema ili waweze kujiletea maendeleo.

Dkt. Biteko ameyasema hayo Novemba 1, 2024 wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara katika eneo la soko la zamani, wilayani Sengerema mkoani Mwanza.

“ Tumekutana hapa kwa kuwa nchi ina amani, watu wa Sengerema tupendane, tushirikiane, tuthaminiane na tujaliane ili tuweze kuwa na fursa ya kujishughulisha na shughuli zitakazotuletea maendeleo,” amesema Dkt. Biteko.

Ameongeza “ Mhe. Rais amefanya mambo mengi na alipopita hapa alieza, tunapotaja miradi aliyotekeleza tunamtaja sana yeye Mhe. Rais kwa sababu dhamana ya maendeleo ya Watanzania na wananchi wa hapa Sengerema ipo mikononi mwake,”

Dkt. Biteko ameendelea kwa kusema Sengerema haikuwahi kuwa na hospitali ya wilaya isipokuwa katika kipindi cha Rais Samia imepata hospitali hiyo. Amefafanua zaidi kwa kusema alipoitembelea hospitali hiyo amebaini upungufu wa majengo ambayo ni jengo la upasuaji na kuwa fedha kwa ajili ya ujenzi wake zimeshatolewa tayari, fedha za jengo la wagonjwa mahututi nazo zimefika wilayani hapo na kusema kuwa ujenzi wa uzio wa hospitali utafanyika kwa kutumia mapato ya ndani ya wilaya.

Akizungumzia umeme katika Wilaya ya Sengerema, amesema kuwa vijiji vyote 71 vimepata umeme na kuwa katika vitongoji 425 ni vitongoji vicheche havina umeme na vinafanyiwa kazi ili wilaya hiyo ipate umeme wa uhakika, Dkt. Biteko amesema Serikali inajenga njia nyingine ya umeme kutoka Nyakanazi hadi Igaka na kutoka Igaka hadi Sengerema na kuwa jitihada hizo za Serikali zinatafsiri maendeleo ambayo yanahitajika na watu wa Sengerema na sio maneno pekee.

Aidha, amewapongeza wananchi wa Sengerema kwa kuwa na jitihada katika kuzalisha chakula cha kutosha ambapo wamezalisha zaidi ya tani 500,00 huku mahitaji yakiwa tani 333,000 pekee.

Fauka ya hayo, Dkt. Biteko amesema kuwa wananchi wa Sengerema wamempata mbunge mchapakazi Mhe. Hamisi Tabasamu na kumtaka aendeleze juhudi za kuwaletea maendeleo wananchi wake sambamba na kuwahimiza wananchi kuendelea kumpa ushirikiano zaidi mbunge huyo.

Pia, Dkt. Biteko amewaasa wananchi wa Sengerema kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa amani na kufuata taratibu na sheria na kuwa uchaguzi huo usiwe sababu ya kuwagawa.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda amesema kuwa Mkoa wake umejiandaa vizuri kwa ajili ya kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuwa umeshika nafasi ya tatu katika zoezi la kuandikisha wapiga kura kwa idadi kubwa katika Daftari la Wapiga Kura.

Kwa upande wake, Diwani Kata ya Ibisawageni, Mhe. Jumanne Masunga ameipongeza Serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwemo kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari katika kata yake.

“ Hata katika miradi ya maji katika wilaya yetu inaendelea vizuri sasa tumetandaza mabomba kama kilomita 75 ili maji yaweze kuwafikia wananchi wetu. Mwaka jana tumejenga tanki la maji kwa kiasi cha shilingi milioni 554 na tunajenga barabara ya lami, tunaomba utufikishie shukrani zetu kwa Rais Samia na tunamuomba atuongezee bajeti ya ujenzi wa barabara za lami,” amesisitiza Bw. Masunga.
 

Naibu Waziri Mkuu na Waziri Nishati Dkt.Doto Biteko akizungumza na wananchi wa Sengerema kwenye mkutano wa hadhara.

 

Picha za wananchi wa Wilaya ya Sengerema wakimsikiliza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt.Doto Biteko hayupo pichani.

Related Posts