Bosi wa Dar24 apatikana Kigamboni akiwa hai, Polisi wafafanua

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Kampuni ya Dar24, Maclean Mwaijonga amepatikana akiwa hai eneo la Buyuni, Kigamboni jijini Dar es Salaam baada ya kudaiwa kutoweka tangu Oktoba 31, 2024.

Taarifa ya kupatikana kwake imethibitishwa na Jeshi la Polisi Kanda maalumu ya Dar es Salaam leo Jumamosi Novemba 2, 2024 ambalo pia lilikuwa likimtafuta kwa kushirikiana na ndugu na wafanyakazi wenzake.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa kanda hiyo, Jumanne Muliro amesema ndugu yake akiwa na polisi ndio walimuona mfanyakazi huyo Kigamboni.

“Polisi wakiwa na ndugu zake walienda mpaka maeneo ya Kigamboni, Buyuni na kumkuta mtu huyo akiwa barabarani. Alikuwa anapepesuka, walimpeleka hospitali na baada ya vipimo ilionekana ana afya njema,” amesema Muliro

Kamanda huyo amesema katika maelezo yake, mtu huyo anadai kuwa alichukuliwa na watu aliokuwa na mazunguzo nao ya kibiashara kwa muda mrefu.

“Kitu anachokumbuka walimpa kinywaji kilichomfanya apoteze fahamu mpaka alipopata fahamu na kujikuta eneo alipopatikana,”amesema Muliro.

Mwaijonga inadaiwa alipotea Agosti 31, 2024 wakati anatoka ofisini kwao eneo la Rose Garden, Mikocheni jijini Dar es Salaam akiwa na gari yake aina ya Toyota Prado.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi

Related Posts