Utoro mawaziri bungeni, mpira warejeshwa kwa spika

Dodoma. Sakata la utoro wa mawaziri, naibu mawaziri na wabunge bungeni limewaibua wachambuzi wa masuala ya siasa baadhi wakirudisha mpira kwa Spika wa Bunge kutumia kanuni kukomesha hali hiyo.

Baadhi ya waliozungumzia suala hilo wamesema linachangiwa na homa ya uchaguzi majimboni mwao.

Oktoba 31, 2024, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alisema kutokuwapo mawaziri bungeni ni suala ambalo wamelizungumza mara nyingi na kutaka viongozi hao kutoa kipaumbele kwa Bunge.

“Waziri uko hapa (hakumtaja) na haya mambo yameshazungumzwa mara kadhaa. Sasa tusifike mahali ambapo waziri atakuwa hayupo (bungeni) halafu tukaahirisha tumsubiri yeye aje ili Bunge liweze kuendelea.

“Tusifike huko, tunatamani ile heshima ambayo tunaheshimiana hii mihimili iendelee kuwepo,” alisema Dk Tulia.

Suala hilo pia limewahi kukemewa na aliyekuwa Spika, Job Ndugai aliyewataja mawaziri na naibu mawaziri ambao hawahudhurii shughuli za kamati za Bunge.

Changamoto hiyo pia ipo kwa wabunge kutohudhuria vikao. Miongoni mwa athari zilizowahi kujitokeza ni kushindwa kupigwa kura ya uamuzi kwa Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali namba 2 wa mwaka 2018.

Muswada huo ulishindwa kupigiwa kura kutokana na akidi ya wabunge kutotimia. Kati ya wabunge 397,  waliokuwepo bungeni walikuwa 65.

Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia aliyekuwa Katibu Mkuu wake, Dk Bashiru Ally kiliwahi kuzungumzia hilo kwa kuwaandikia barua wabunge kuwataka kujieleza kwa nini hawakuhudhuria vikao vya Bunge.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Dk Revocatus Kabobe amesema mawaziri wanapokosa kuwepo bungeni inamaanisha hakuna kinachoendelea kwa sababu hakuna mtu anayesisikiliza hoja za wabunge.

“Kutokuwepo kwao kunakwamisha shughuli za Bunge. Wabunge ndio wawakilishi wa wananchi, wana maswali, wana hoja mbalimbali ambazo Serikali inapaswa kuzijibu na hujibiwa kupitia mawaziri,” amesema.

Amesema ni wakati sahihi wa Spika kutumia kanuni zinazotoa mwongozo wa jinsi ya kushughulikia changamoto hiyo iwapo suala hilo limekuwa sugu ili kuwabana wabunge.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie amesema Spika anaweza kudhibiti tatizo hilo.

“Arudi tu kwenye kanuni za Bunge, kwa sababu kila kikao kina kanuni zake. Lakini kabla ya kwenda huko, ajiulize kwa nini hawahudhurii? Akishajua kwa nini hawahudhurii ndipo aje kwenye kanuni.

“Kwa nini hawahudhurii? Je, wapo kwenye mambo binafsi au wapo kwenye miradi, na kama wapo kwenye miradi ni muda sahihi ambao badala ya kuwepo bungeni kutengeneza sera za wananchi waende huko?” amesema.

Amesema Spika anaweza kuwasiliana na Waziri Mkuu kujua walipo mawaziri.

“Kwa sababu mawaziri wanamuaga Waziri Mkuu na kama hawamuagi ni tatizo lingine kubwa zaidi,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi Novemba 2, 2024 Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT), Dk Ntuli Ponsian amesema ni mwaka wa uchaguzi wa serikali za mitaa, mawaziri ni wabunge, hivyo muda mwingi huwa majimboni kuhakikisha viongozi watakaopatikana ni watu wenye mrengo wao au ni watu wao.

“Wako jimboni wanatafuta wajumbe (kwa ajili ya uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani), na ukiachilia hili mwakani pia ni uchaguzi mkuu sasa hivi huko majimboni kumeshakuwa kwa moto kwa hiyo kila mmoja analinda jimbo lake,” amesema.

Amesema hafahamu watadhibiti vipi lakini wabunge wengi hawana utulivu bungeni kutokana na hali inayoendelea majimboni kwao.

Ameeleza mawaziri kutofika bungeni kunakifanya chombo hicho kukosa umuhimu, kwa sababu mambo yanayojadiliwa ni ya kisera na yanahitaji mabadiliko ya haraka.

“Sasa kama wabunge wako bungeni wanafoka tu, hakuna waziri ambaye anasikiliza unakuwa ni upotezaji wa muda tu. Kwa maana huo muda wanaoutumia wabunge ambao kimsingi ni gharama za walipakodi unakuwa unapotea tu,” amesema.

Dk Ponsian amesema athari nyingi zinazosababishwa na changamoto hiyo ni kutotekelezwa kikamilifu kwa masuala mengi yanayozungumzwa bungeni.

Amesema mawaziri kutegemea wasaidizi wasikilize kinachozungumzwa bungeni, hakuondoi umuhimu wa uwepo wao katika chombo hicho.

Amesema changamoto hiyo haipo Tanzania tu bali duniani kote na kuongeza kuwa ndiyo maana hata unapofuatilia mwenendo wa uchumi wa thamani wa fedha katika nchi yenye uchaguzi,  huanza kuporomoka mwaka mmoja kabla uchaguzi na kisha kupanda mwaka mmoja baadaye.

“Tunapoelekea katika uchaguzi si utoro tu wa kuhudhuria bungeni kwa mawaziri na wabunge bali na utekelezaji wa sera. Ni vitu vingi vitatokea katikati kwa sababu usimamizi wa mawaziri unakuwa ni mdogo, hata upotevu wa fedha utakuwa ni mwingi mwaka mmoja kabla na wakati wa uchaguzi wenyewe,” amesema.

Dk Ponsian amesema kimsingi jambo la utoro wakati wa uchaguzi au mwaka mmoja baada ya uchaguzi, linategemewa kujitokeza katika mabunge mengi duniani, hivyo hafahamu wataweka mkakati gani kukabiliana na changamoto hiyo.

“Anachopaswa kufahamu (Spika) sababu kubwa ya utoro wa wabunge wakati huu ni homa ya uchaguzi unaoendelea nchi nzima. Labda kama watadhibiti wale wanaoleta chokochoko majimboni labda wabunge watatulia,” amesema.

Mbunge wa Mvumi, Livingstone Lusinde amesema kutokuwepo kwa mawaziri na naibu mawaziri wakati wa vikao vya Bunge, kuna athari kwa sababu wao ndio wawakilishi wa Serikali katika chombo hicho.

Amesema viongozi hao ndio wanaotakiwa kutafsiri na kuchambua hoja za wabunge ili waridhike kwamba zina uhusiano kati ya Serikali na wawakilishi wananchi.

“Wasipokuwepo bungeni ina maana wabunge wanasema pekee yao, hakuna mtu wa kuchukua hoja zao. Pia mtu wa kutafsiri hayupo,” amesema.

Amesema hoja za kamati ni hoja za Bunge kwa kuwa wanaifanya kazi hiyo kwa niaba ya Bunge na wanapoazimia,  inamaanisha wanatoa maelekezo au maagizo kwa Serikali.

Amesema baada ya Bunge kuazimia, Serikali inapaswa kuleta mrejesho wa masuala yaliyotekelezwa, hivyo kama haijasikia vizuri ina maana kwenye utekelezaji kutakuwa na upungufu.

Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya amesema mawaziri na naibu mawaziri wanatakiwa kusikiliza michango ya wabunge na maazimio ya Bunge, ili kufahamu ni jambo gani na kwa kipindi gani wanakwenda kulifanyia kazi.

“Si jambo zuri kabisa. Naona jinsi wanavyochukulia kawaida yaani ile nidhamu ya Bunge haipo kwa upande wao. Sawa tunajua kuwa kuna dharura lakini haiwezekani ikawa kila siku mtu huyohuyo ana dharura,” amesema.

Amesema mara nyingine unakuta mawaziri wako wachache bungeni na muda mwingine unakuta hakuna mawaziri isipokuwa chief whip (mnadhimu wa Bunge).

Kuhusu wabunge kutokuwepo bungeni, Bulaya amesema hilo linasababishwa na baadhi yao kutojua wajibu wao kuwa wamechaguliwa na wananchi ili wawakilishe bungeni.

Amesema haiwezekani kila mara mbunge kuwa na dharura na kuwa miongoni mwa majukumu yake makubwa ni kuwakilisha bungeni waliomchagua, hivyo wanapaswa kulitekeleza jukumu hilo kikamilifu.

Related Posts