KOCHA wa Simba, Fadlu Davids, ameshtuka kutokana na ugumu aliokumbana nao katika mechi za ugenini hasa kwenye viwanja vigumu na kisha kupanga mikakati mipya ya kuhakikisha wanafanya mambo makubwa kuwapa burudani mashabiki na wapenzi wa timu hiyo sambamba na timu kushinda kiulaini.
Simba juzi ililazimika kusubiri dakika za majeruhi kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mashujaa, lakini Fadlu alisema kwa sasa anaandaa mpango maalum wa mbinu mbadala ili kutafuta matokeo chanya katika viwanja vigumu, ambavyo kwa kawaida vinawanyima uhuru wachezaji wake kucheza soka la pasi za chini na haraka wakati wa kushambulia.
Mbinu hizi mpya zinalenga kuhakikisha kwamba Simba inakuwa na ufanisi, hata katika mazingira yasiyowaruhusu kutandaza soka safi.
Katika mechi hiyo ya juzi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma, Simba ilijikuta katika wakati mgumu mbele ya wenyeji wao kwa kilichoelezwa uwanja kutokuwa rafiki kama ilivyokuwa pia Sokoine Mbeya na Fadlu akasisitiza tayari ameshajua tatizo na analifanyia kazi mapema.
Akizungumza na Mwanaspoti, Fadlu alisema upo umuhimu wa kuwa na mipango ya ziada kwa mechi ambazo zina changamoto za viwanja.
“Tunapocheza kwenye viwanja kama hivi, lazima tuwe tayari kubadili mbinu kulingana na hali halisi ya mazingira,” alisema Fadlu na kuongeza kuwa, Simba inahitaji kuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto yoyote inayojitokeza, bila kujali aina ya uwanja.
Ushindi huo umeiweka Simba kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi, ikiwa na pointi 22 kutokana na mechi tisa ilizocheza. Fadlu anasisitiza kuwa ili kuendelea kufanikiwa, timu yake lazima iendelee kujiandaa vizuri kwa changamoto zinazokuja, hasa wanapocheza kwenye viwanja vya ugenini ambavyo haviwapi uhuru wa kucheza wanavyopendelea.
“Wachezaji wetu wanahitaji kujua kwamba tunaweza kucheza kwa njia tofauti ili kupata matokeo. Hatuwezi kutegemea aina moja ya uchezaji kwa kila uwanja. Ni lazima kuwa na mipango mbalimbali ili kuhakikisha tunapata ushindi, na hilo linatupa faida kubwa ya kimkakati kwenye ligi,” aliongeza Fadlu.
Kwa mujibu wa kocha huyo, mbinu hizo mpya zinalenga kuimarisha ukakamavu wa timu yake kwa kuwaongezea mazoezi ya nguvu na ufundi wa kucheza mipira ya juu pale inapobidi. “Tunatakiwa kuhakikisha kwamba kila mchezaji yuko tayari kupambana na hali yoyote ya uwanja,” alifafanua.
Mbinu hizi zinahusisha pia matumizi ya mipira mirefu na mbinu za kimwili ambazo zitawasaidia wachezaji wa Simba kuhimili mazingira magumu ya viwanja na kuweza kutumia nafasi wanazopata kufunga mabao.
Siku chache zilizopita, kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alionekana akilalamikia Uwanja wa Sheikh Amri Abeid kwamba hauruhusu kucheza aina yao ya soka ila hapakuwa na namna iliwabidi kucheza kulingana na mazingira na kuhakikisha wanapata ushindi.