Dar es Salaam. Kuna usemi unaosema ‘haki siku zote haiombwi bali inadaiwa,’ hivi ndivyo unaweza kuelezea safari ya siku 2,500 za aliyekuwa Hakimu Mkazi Pangani mkoani Tanga, Hamis Bally kupigania haki yake katika mhimili alioufanyia kazi.
Bally aliachishwa kazi Januari 31, 2016 baada ya Kamati ya Maadili ya Maofisa wa Mahakama kumuona ana hatia katika makosa mawili ya madai ya utovu wa nidhamu na uzembe katika utekelezaji wa kazi za mahakama.
Hakuridhishwa na uamuzi huo, akamua kupinga kufukuzwa kwake kwa njia ya mapitio ya mahakama (judicial review), ambayo kisheria ni lazima kwanza afungue maombi ya kupatiwa kibali cha kufungua maombi ya mapitio hayo.
Hivyo, akafungua maombi namba 11 ya 2017 katika Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala ya Dar es Salaam, lakini Septemba 22, 2017 yakatupwa na Jaji Wilfred Dyansobera akisema hakuwa amejenga vizuri msingi wa kupewa kibali hicho.
Hakuridhika na uamuzi huo akaamua kukata rufaa Mahakama ya Rufani Tanzania ambapo rufaa hiyo ikasikilizwa na majaji watatu, Rehema Mkuye, Abraham Mwampashi na Paul Ngwembe akiegemea sababu kuu tatu.
Alifungua rufaa namba 448 ya 2021 dhidi ya Kamati ya Maadili ya Maofisa wa Mahakama, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Tume ya Utumishi wa Mahakama na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama wajibu rufaa wa kwanza, wa pili, wa tatu na wanne.
Moja ni kwamba Mahakama haikutafsiri vizuri sheria inayosimamia maombi ya kibali cha kufungua maombi ya mapitio ya Mahakama na pili Mahakama ilikosea kisheria pale ilipochukulia maombi yake kama ya mapitio.
Katika hoja ya tatu, Bally aliyekuwa amewakilishwa mahakamani na wakili Dk Lucas Kamanija, alisema Mahakama Kuu ilikosea iliposhindwa kutumia mamlaka yake kutoa uamuzi kuwa yale anayoyalalamikia yalifaa kupingwa kwa mapitio.
Jopo la majaji katika hukumu yao ya Oktoba 31, 2024 walisema hakukuwa na haja ya kushughulikia sababu zote tatu, kwani ya pili pekee ilitosha kuifanya mahakama ifikie maamuzi ya kufuta amri ya Mahakama Kuu.
Majaji hao wamekubaliana na hoja ya Bally kuwa Jaji aliyesikiliza maombi yake ya kuomba kibali cha kuruhusiwa kufungua maombi ya mapitio ya mahakama, alichukulia maombi yake na kuyaamua kama ni maombi ya mapitio ya mahakama.
“Katika mazingira haya huwezi kukataa kuwa mahakama kukataa maombi ya kutoa kibali ilishawishiwa na utafiti wake kwamba mrufani alishindwa kuthibitisha upendeleo, ukandamizaji na kunyimwa haki ya kusikilizwa.
“Katika mazingira haya ambapo Mahakama Kuu ilijiingiza katika kutoa uamuzi kama vile inaamua kuhusu maombi ya mapitio ya mahakama ambayo hayakuwa mbele yake ndio maana tunasema sababu ya pili inatosha kuamua shauri,” alisema.
Walisema Mahakama Kuu haikupaswa kuhitimisha kwamba muombaji alikuwa ameshindwa kuthibitisha madai ya upendeleo, ukandamizaji, ukiukwaji wa haki ya kusikilizwa na maombi yasiyo na mashiko kisheria.
Katika hukumu yao, majaji hao walisema wanakubaliana na rufaa hiyo na kubatilisha uamuzi wa Mahakama Kuu na kuamuru jalada la maombi hayo lirudishwe Mahakama Kuu mbele ya Jaji mwingine ili lisikilizwe upya.
Hii inafanya Bally awe amefikisha siku zaidi ya 2,550 tangu mwaka 2017 alipoanza kupigania haki yake katika mhimili wa mahakama ambao alikuwa akihudumu kabla ya kufukuzwa kazi mwaka 2016.
Kwa uamuzi huu wa jopo la majaji, ina maana bado ana safari ndefu ya kupigania haki yake, kwanza kusubiri kama maombi yake ya kuomba kibali cha kufungua mapitio ya mahakama yatakubaliwa, halafu ndio afungue maombi ya mapitio ya mahakama.