Badenoch achaguliwa kuongoza chama cha Conservative Uingereza

London. Mwanamke mweusi, Kemi Badenoch ameshinda kinyang’anyiro cha kuwa kiongozi mpya wa chama cha Conservative cha Uingereza, akiahidi kukirejesha katika misingi yake ya uanzilishi na kuwarejesha wapigakura baada ya kushindwa vibaya katika uchaguzi wa Julai 2024.

Badenoch (44), aliibuka kidedea kwenye kinyang’anyiro hicho dhidi ya mshindani wake wa karibu, waziri wa zamani wa uhamiaji, Robert Jenrick, akipata asilimia 57 ya kura za wanachama wa chama hicho.

Alipata kura 53,806, huku Jenrick akipata kura 41,388 kutoka kwa wanachama wenye sifa za kupiga kura 131,680. Chama kilitangaza kuwa waliojitokeza kwenye uchaguzi huo wa Conservative walikuwa asilimia 72.8.

Badenoch anachukua nafasi ya Waziri Mkuu wa zamani, Rishi Sunak na ameahidi kukiongoza chama hicho katika kipindi cha mabadiliko, akisema kimegeukia kituo cha kisiasa kwa “kutawala kutoka kushoto” na lazima kurudi kwenye itikadi zake za jadi.

Mwanamke huyo wa kwanza mweusi kiongozi wa chama kikuu cha kisiasa nchini Uingereza, Badenoch amesema kuwa kiongozi ni heshima kubwa.

Waziri huyo wa zamani wa masuala ya usawa anakabiliwa na kibarua kigumu cha kukiunganisha tena chama kilichogawanyika na kilichodhoofika ambacho kiliondolewa madarakani Julai 2024 baada ya kuongoza kwa miaka 14.

“Kazi iliyo mbele yetu ni ngumu, lakini rahisi,” amewaambia wanachama wa chama hicho katika hotuba yake ya kukubali kuchaguliwa. “Jukumu letu la kwanza kama upinzani mwaminifu kwa mfalme, ni kuiwajibisha serikali hii ya Labour.”

“Wakati umefika wa kusema ukweli,” amesema. “Lazima tuwe waaminifu kuhusu ukweli kwamba tulifanya makosa”.

Akiwa mzaliwa wa London kwa wazazi wa Nigeria, Badenoch alitumia miaka yake ya utoto huko Lagos. Alikuwa mbunge mwaka 2017 na mwaka 2022, alitangaza nia yake kwa mara ya kwanza ya kuwa kiongozi wa Conservative.

Atakuwa kiongozi rasmi wa upinzani na atakabiliana na Keir Starmer wa chama cha Labour katika Bunge la Kitaifa kila Jumatano katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu.

Wakati Serikali ya Labour ikiwa na mwanzo mgumu kufuatia ushindi wake wa kishindo, baadhi ya Wahafidhina wanazidi kuwa na matumaini kwamba wanaweza kurejea madarakani katika uchaguzi ujao, ambao unapaswa kufanyika mwaka 2029.

Lakini baadhi ya Wahafidhina wenye msimamo mkali wana wasiwasi kwamba Badenoch anaweza kuwatenga sio tu watu wa mrengo wa wastani zaidi ndani ya chama, lakini pia baadhi ya wapigakura ambao walishindwa na chama cha Liberal Democrats katika uchaguzi uliopita.

Related Posts