Marekani. Zikiwa zimebaki siku mbili kufanyika uchaguzi wa Marekani, Novemba 5, 2024, wagombea urais, Donald Trump wa Republican na Kamala Harris wa Democrats, wameendelea na kampeni za lala salama katika majimbo yasiyo ngome ya chama chochote.
Viongozi hao wa vyama vya Democrats na Republican walielekea jimbo la North Carolina jana Jumamosi Novemba 2, 2024 Kamala na Rais wa zamani, Trump wote walikuwepo katika jimbo hilo siku hiyo.
Wagombea hao wanatembelea majimbo hayo ya kusini yanayobadilikabadilika kisiasa wakijaribu kuwaomba wapigakura wa maeneo hayo wawaunge mkono, huku joto la uchaguzi likizidi kupanda nchi humo.
Jumatano walikuwa North Carolina, Alhamisi Nevada na Ijumaa Wisconsin, huku wakati mwingine wakifanya mikutano karibu karibu.
Hii inaonyesha jinsi kura zitakavyoamua matokeo ya uchaguzi katika majimbo machache ambayo uchunguzi umeonyesha kuwa na ushindani mkali.
“Tushinde jimbo hili, tutashinda mchezo mzima,” amesema Trump katika hotuba yake mjini Gastonia, North Carolina. “Tumeshinda mara mbili hapo awali na tutashinda kwa urahisi,” amesisitiza Trump.
Kwa upande wake, Kamala alisema Trump si mtu anayezungumzia jinsi ya kufanya maisha kuwa bora huko Atlanta, Georgia huku akisema yeye anapanga kuboresha hali ya maisha kwa Wamarekani.
Wakati hayo yakiendelea, watu mbalimbali mashuhuri wameendelea kumuunga mkono Kamala wakiwemo Eminem, Beyoncé, Taylor Swift, huku wanaomuunga mkono Trump wakiwa ni Jason Aldean, Amber Rose na bilionea Elon Musk.
Vijembe vyatawala kampeni
Katika kampeni zao, Kamala na Trump wamekuwa wakirushiana vijembe huko Wisconsin. Awali, Kamala wakati akitoa hotuba yake akiwa kwenye Chuo Kikuu cha Wisconsin mjini Madison, amesema ni wakati wa uongozi wa kizazi kipya kuingia madarakani nchini humo.
Kwa mujibu wa DW, mgombea huyo ameongeza kwamba wapigakura katika uchaguzi huo wana nafasi ya kufunga ukurasa wa muongo mmoja wa Trump anayetaka kurudi madarakani.
Kamala amesema ni wakati wa kizazi kipya kuiongoza Marekani na yuko tayari kuwapa aina hiyo ya uongozi kama Rais ajaye wa nchi hiyo.
Kamala amewaahidi pia wafuasi wake kuwa iwapo atachaguliwa, atafanya juhudi za kutafuta suluhisho kwa matatizo yanayowakabili na kwamba anataka maendeleo.
Kwa upande, Trump alipokuwa katika jimbo hilohilo, alionekana kwenye kampeni akiwa amepanda gari la taka, hatua inayotafsiriwa kuwa ni jibu kwa kauli ya Rais Joe Biden iliyotolewa hivi karibuni, iliyoashiria kuwaita wafuasi wa Trump kuwa sawa na takataka.
Akizungumza katika mkutano huo wa kampeni katika eneo la Green Bay, Trump amefafanua kuwa alichokisema Biden kinaakisi namna wawili hao wanavyowachukulia wafuasi wake.
Ameeleza kwamba maoni ya Rais Biden ni matokeo ya moja kwa moja ya uamuzi wa mpinzani wake, Kamala wa kumuona yeyote asiyempigia kura si binadamu kamili.
Katika kampeni hiyo, Trump ameongeza kuwa Biden na makamu wake wamekuwa wakiichukulia nchi nzima kuwa takataka kwa kufungua mipaka na kuruhusu mfumuko wa bei na yanayoendelea Russia na Ukraine.
Katika mkutano wake wa kampeni mjini Las Vegas, Kamala amekuwa akimkosoa vikali Trump kwa madai ya udhalilishaji wa wanawake.
Vilevile, amemshtumu Rais huyo wa zamani ikiwa atachaguliwa kuongoza tena, atapiga marufuku utoaji mimba kote nchini humo, atazuia upatikanaji wa njia za uzazi wa mpango atahatarisha huduma za usaidizi zinazofahamika kama IVF.
Trump, akiwa mjini Henderson, amelizungumzia suala la uhamiaji na kuwaahidi wapigakura kulikomboa taifa. Amesema Marekani ni Taifa linalotawaliwa na kuwa maelfu ya wahamiaji huingia nchini humo wakiwa na vifaa vyenye hadhi ya kijeshi. Amewaambia wapigakura wake kuwa Novemba 5 itakuwa “siku ya ukombozi wa Marekani”.
Trump ameeleza kuwa kutokana na mipaka ya Marekani kuwa wazi, mpinzani wake ambaye ni Makamu wa Rais, anasaidia kufanikisha ulanguzi wa binadamu, uingizwaji wa dawa za kulevya na kuingia kwa wanaofanya biashara hiyo haramu Marekani.
Tim Walz ni mgombea mwenza wa chama cha Democrats ambaye alichaguliwa mihula miwili kuhudumu kama Gavana wa Jimbo la Magharibi kati la Minnesota kabla ya kuteuliwa na Kamala kuwa mgombea mwenza.
James David (JD) Vance mgombea mwenza wa chama cha Republican yeye aliteuliwa na Trump. Vance ambaye alikuwa Seneta wa Ohio, ni kijana mwenye umri wa miaka 39.
Imeandikwa na Sute Kamwelwe kwa msaada wa mashirika ya habari.