Dar es Salaam. Viongozi wa Serikali za mitaa hushughulikia masuala ya msingi yanayogusa maisha ya kila siku ya raia kama vile usalama, afya, elimu na mazingira.
Pia, wana wajibu wa kuhakikisha maendeleo endelevu, usawa na utulivu katika jamii. Kwa hiyo, umuhimu wao katika kuboresha maisha ya wananchi hauwezi kupuuzwa hasa katika maeneo ya vijijini na mijini.
Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa ameelezwa katika Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977, ibara ya 145 sura ya 8 inayohusu mamlaka ya umma na kazi zake zimeainishwa katika sehemu ya a, b na c
Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Mitaa Mkoa wa Dar es Salaam, Juma Mwingamno anasema wanapofika kwa wananchi wa eneo husika huwa na utaratibu wa kueleza majukumu wanayoyafanya na watakayoyafanya.
“Unapofika kwenye vikao haiwezekani kuanza kutangaza majukumu maana hakuna mtu anayeweza kukuelewa, hivyo inatakiwa tuanze na changamoto zinazowakabili wananchi na ndipo itafikia hatua ya kueleza majukumu wanayoyafanya,” anasema Mwingamno.
Anasema ili wananchi kujua majukumu kikamilifu inatakiwa kukumbushiana mambo yaliyopita yanayofanywa na Serikali iliyopo madarakani kwa kuonyesha kwa vitendo ambavyo vimo ndani ya mtaa husika.
Mwingamno anasema viongozi hawa wanatakiwa kushirikiana na wananchi katika kuhakikisha ulinzi wa maeneo yao kupitia vikundi vya ulinzi shirikishi ambavyo vimekuwa msaada katika kupunguza uhalifu kwenye jamii na kusaidia kuwakamata wahalifu kwa kushirikiana na vyombo vya usalama.
Katika jamii, viongozi wa Serikali za mitaa wana mchango mkubwa kwa kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi na wanasaidia kutatua migogoro, kushughulikia matatizo ya usalama na kuhakikisha wananchi wanapata huduma za msingi.
Katika maeneo mengi kwa sasa kumekuwa na ulinzi shirikisi, mwenyekiti wa Serikali ya mtaa ndiye mwenyekiti wa ulinzi na usalama wa eneo husika kwa kushirikiana na vijana walioteuliwa na wananchi.
Aidha, wanachangia katika kutoa elimu ya kupambana na vitendo vya uhalifu na kuwajengea wananchi uwezo wa kujilinda na mali zao.
Kusimamia huduma za kijamii
Kazi nyingine muhimu ya viongozi wa Serikali za mitaa, ni kusimamia huduma za kijamii kama vile afya, elimu na usafi wa mazingira.
Katika masuala ya afya, viongozi hawa wanataka kuhakikisha zahanati na vituo vya afya vinatoa huduma bora kwa wananchi na kufuatilia kwa karibu upatikanaji wa dawa na vifaatiba na kuhakikisha zahanati zina vifaa vya kutosha.
Viongozi hawa wana jukumu la kuhamasisha kampeni za afya kama chanjo, upimaji wa afya na utoaji wa elimu ya afya kwa wananchi.
Katika elimu, viongozi wa Serikali za mitaa wanahakikisha kuwa shule katika maeneo yao zinatoa elimu bora na wanafunzi wanakuwa kwenye mazingira salama.
Pia, jukumu la kutatua changamoto za miundombinu kama vile madarasa, madawati na vyoo pamoja na kushughulikia changamoto za walimu na upungufu wa vifaa vya kufundishia.
Kwa kufanya hivyo, wanachangia katika kuimarisha sekta ya elimu na kusaidia kizazi kijacho kuwa na maarifa na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.
Usimamizi wa miradi ya maendeleo
Jukumu jingine la viongozi wa Serikali za mitaa ni kusimamia miradi ya maendeleo katika maeneo yao, wanapokea maoni na mapendekezo ya wananchi kuhusu miradi inayohitajika kama vile ujenzi wa barabara, madarasa na visima vya majisafi.
Wanaratibu utekelezaji wa miradi hiyo kwa kushirikiana na mashirika ya maendeleo na Serikali kuu.
Kwa mfano, viongozi hawa hufanya tathmini ya changamoto zinazowakabili wananchi kama upatikanaji wa maji na wanashirikiana na mashirika ya kutoa maji kuhakikisha huduma hii inapatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu.
Kupitia usimamizi wa miradi, viongozi wa Serikali za mitaa wanatakiwa kuhakikisha rasilimali za Serikali zinatumika kwa ufanisi na miradi inakamilika kwa wakati.
Wanatakiwa kushirikiana na wananchi kwa kuwahamasisha kushiriki kwenye miradi ya maendeleo kwa kutoa nguvu kazi, ardhi na rasilimali nyingine za kijamii.
Ushirikiano huu unajenga umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi na kuimarisha uchumi wa eneo husika.
Viongozi wa Serikali za mitaa pia ni watatuzi wa migogoro ndani ya jamii. Mara nyingi, migogoro kuhusu ardhi, majirani na familia huletwa kwa viongozi wa mitaa kwa ajili ya usuluhishi.
Kwa kutumia busara na sheria ndogondogo za kijamii, viongozi hawa husaidia kupatanisha pande zinazohusika na kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa.
Licha ya baadhi yao kuchangia migogoro ya ardhi lakini hilo ni eneo kubwa katika maeneo mengi ya vijijini, inashughulikiwa kwa umakini na viongozi wa Serikali za mitaa.
Wanahakikisha wanafuata sheria na taratibu za ardhi katika kutoa uamuzi ili kuepusha migogoro isiyohitajika.
Pia, wanashirikiana na vyombo vya kisheria na wataalamu wa ardhi ili kutoa uamuzi sahihi na wa haki kwa pande zote.
Kazi ya viongozi wa Serikali za mitaa pia inatakiwa kuhakikisha kuna uwiano katika jamii. Wanahakikisha rasilimali na huduma zinafikia wananchi wote kwa usawa, bila ubaguzi wa kikabila, kidini, au kijinsia.
Hii inasaidia kuleta mshikamano na kuimarisha amani na utulivu katika jamii. Viongozi wa mitaa wanatakiwa kufanya kazi kwa uwazi na uwajibikaji kwa kutoa taarifa kuhusu mapato na matumizi ya fedha za maendeleo kwa wananchi kupitia mikutano ya hadhara.
Kwa kufanya hivyo, wanajenga imani ya wananchi kwa Serikali na wanahamasisha ushirikiano katika kufanikisha malengo ya maendeleo.
Changamoto zinazowakabili
Licha ya mchango wao mkubwa, viongozi wa Serikali za mitaa wanakabiliwa na changamoto kadhaa katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akielezea changamoto zinazokuwa zinawakabili, Mwingamno ametaja upungufu wa rasilimali, kama vile fedha na vifaa ili kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Ukosefu wa elimu na ujuzi wa kutosha kwa baadhi ya viongozi huzuia ufanisi katika utendaji wao.
Changamoto nyingine ni upungufu wa ushirikiano kutoka kwa wananchi, hasa wakati wananchi wanapokosa imani na Serikali.
Pia, viongozi wa mitaa mara nyingi hukutana na changamoto za kisiasa zinazoweza kuathiri utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma.
Suala hili linahitaji kuwa na viongozi wenye busara na wenye uwezo wa kuhimili changamoto za kisiasa ili kuhakikisha kuwa wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwa maslahi ya wananchi wote.
Kwa msaada wa viongozi hawa, wananchi wanapata nafasi ya kushiriki moja kwa moja katika uamuzi unaowahusu na kuhakikisha kuwa rasilimali za umma zinatumika kwa faida ya wote.
Hivyo, ni muhimu kwa Serikali kuhakikisha kuwa viongozi hao wanapatiwa mafunzo, rasilimali na msaada wa kutosha ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Mtafiti Mradi wa Ubora wa Maudhui wa Vyombo vya Habari Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Abdallah Katunzi anasema wananchi wanatakiwa kutambua umuhimu wa viongozi wa Serikali za mitaa kwa sera zao na wanachokwenda kufanyia kazi.
“Wananchi hawajui majukumu ya kazi za Serikali za mitaa, watu wengi wamekuwa wakipokea taarifa za mtu na si majukumu na kazi ambazo zinakwenda kufanyika kama sera za wagombea katika utekelezaji wa majukumu yao,” anasema Katunzi.
Anasema kunatakiwa kuwe na uwezo wa kuhoji namna gani wagombea wanakwenda kufanyia kazi majukumu yao ambayo wananchi wanaweza kunufaika katika jamii.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917