Arusha. Mahakama Kuu Masjala ndogo ya Dodoma imewaachia huru washtakiwa saba ambao ni sungusungu, waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya mwanakijiji aliyedaiwa kuwa mchawi.
Katika kesi hiyo ya mauaji namba 78 ya mwaka 2023, washtakiwa walikuwa ni Maria Chigwile, Magreth Steven, Agusta Reuben, Janeth Hoya, Mariam Zacharia, Tatu Mkomochi na Pendo Lucas.
Mbele ya Jaji Evaristo Longopa, washtakiwa hao walisomewa shitaka moja la mauaji kinyume na vifungu vya 196 na 197 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Mauaji hayo yalitokea Desemba 17, 2022, katika Kijiji cha Mwitikila, Wilaya ya Bahi, mkoani Dodoma, washtakiwa walidaiwa kumuua Beritha Chalo kwa kumpiga wakimtuhumu kuwa mchawi.
Upande wa mashitaka katika kesi hiyo, uliwasilisha mashahidi 11 na vielelezo viwili, wakati upande wa utetezi ulileta mashahidi saba ambao ni washitakiwa wenyewe.
Hata hivyo, hukumu hiyo ya rufaa iliyotolewa Oktoba 28, 2024, baada ya Jaji Longopa kusikiliza hoja za pande zote mbili, iliwaachia huru washtakiwa wote.
Jaji Longopa alibainisha kuwa upande wa mashitaka haukutimiza wajibu wake wa kuthibitisha shitaka bila kuacha shaka yoyote, hivyo hawakustahili kifungo.
Katika kesi hiyo, upande wa mashitaka uliwakilishwa na mawakili watatu wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Geofrey Mlagala huku mawakili saba, wakiongozwa na Anselin Mwampoma wakiwatetea washtakiwa.
Shahidi wa kwanza, Neema Mpanda alidai Desemba 17, 2022 saa nne asubuhi yeye na dada yake (Grace Mpanda), walikamatwa na Theresia ambaye ni mmoja wa sungusungu wa Kijiji cha Mwitikila ambaye alikuwa mshtakiwa wa pili.
Alidai walifungiwa kwenye moja ya darasa la Shule ya Msingi Lupeta, huku yeye akituhumiwa kutumia bangi na marehemu Beritha akituhumiwa kwa uchawi.
“Na ilipofika mchana tulichukuliwa na kupelekwa kwenye kikao kilichoongozwa na Mwenyekiti wa Kijiji (Albert Mlulu).
Alidai watatu kati yao walivuliwa nguo na kubaki watupu na kuanza kupigwa na sungusungu hao.
“Beritha yeye alilazwa juu ya mchanga wa moto wakawa wanamchapa viboko,” alidai Neema.
Akitoa ushahidi wake, Grace Mpanda ambaye ni shahidi wa pili naye alidai mahakamani hapo kuwa baada ya kutolewa shuleni walikokuwa wamefungiwa, sungusungu hao waliwaamuru kuvua nguo zote, wakawafunga na kamba kwenye mti wa mbuyu uliopo shuleni hapo na kuanza kuwacharaza bakora, huku wenzao wengine wakilazwa mchangani huku wakitandikwa bakora pia.
“Beritha yeye alikuwa anachapwa fimbo huku akivutwa na walikuwa wanamwambia aondoke pale kijijini, ilipofika saa nane mimi waliniachia, lakini wakati huo Beritha alikuwa ameshakufa,” alidai shahidi huyo.
Alidai wakati wakipatiwa adhabu hiyo, kulikuwa na watu wengi kutoka vijiji vitano waliodaiwa kuja kushuhudia Beritha akiadhibiwa kwa kuwa ni mchawi.
“Manyanyaso hayo yaliyoongozwa na Mwenyekiti wa Kijiji Albert Mlulu na kiongozi wa sungusungu, Peter Tosh,” alidai shahidi huyo.
Sabina Madeje, shahidi wa nne alidai kushuhudia sungusungu wakimvua nguo marehemu Beritha na kumuacha na ‘tight’ pekee.
“Ila kwa sababu na mimi nilikuwa nimeumziwa sana, sikumtambua sungusungu yeyote na jioni nikapata taarifa kuwa Beritha amekufa,” alidai.
Shahidi wa tano, Salivina Chalo alidai alisikia kifo cha Beritha na kilichodaiwa kusababishwa na kizunguzungu na hajui mtu yeyote aliyeshiriki kusababisha kifo hicho.
Mwenyekiti wa kijiji alidai mahakamani hapo alisema kuwa alimwona Beritha akianguka chini mara tatu na alimkimbilia kwenda kumsaidia.
Akihojiwa na mawakili wa utetezi, mwenyekiti huyo alidai kuwa alielezwa chanzo cha kifo ni shinikizo la damu na mpaka saa 12: 45 jioni alipoondoka eneo hilo, Beritha alikuwa hai.
Akitoa ushahidi wake, Evaristo Mbiche, Mganga Mfawidhi Msaidizi wa Kituo cha afya Mwitikila alidai kuwa Desemba 18, 2022 asubuhi, aliufanyia uchunguzi mwili wa Beritha na kukuta una michubuko sehemu mbalimbali.
Wakijitetea mahakamani hapo, Maria alidai kuwa ni mkulima na alijiunga na sungusungu Juni 2022. Desemba 17, 2022, alifika kijiji cha Mwitikila kwa mkutano wa ujirani mwema uliowajumuisha wanakijiji kutoka vijiji vitano; Chibelela, Mwitikila, Hangwe, Nchimila na Mtitaa.
Alidai kuwa mkutano huo uliitishwa na viongozi, wakiwemo Mwenyekiti Mtendaji wa Kijiji na Mwenyekiti wa Mgambo.
Alikanusha kumpiga marehemu au kumwona, akieleza kuwa alikamatwa Januari 21, 2023 na maofisa wa Polisi na alipoulizwa kuhusu tukio hilo, alikana kuhusika.
Magreth alidai ingawa alihudhuria mkutano huo, jukumu lake lilikuwa ni kupika. “Na hata sungusungu niliokuwa nao hawapo mahakamani lakini anaweza kuwatambua kwa nyuso zao.”
Mshtakiwa wa tatu, Augusta alidai kuwa alihudhuria mkutano huo na aliporudi Chibelela, Januari 21, 2023 saa nne asubuhi, alikamatwa na Polisi akiwa na mwenyekiti wa kijiji.
Alikana kuhusika na tukio hilo, akieleza kuwa hakufahamu viongozi wa sungusungu waliokuwa kwenye mkutano kwani alikuwa amejiunga miezi michache iliyopita. Jukumu lake lilikuwa kuchota maji ya kupika chakula cha washiriki na alikuwa amevaa mavazi ya kawaida kwani bado hakuwa na sare za sungusungu.
Mshtakiwa wa nne, Janeth ambaye ni mkulima, alisema alijiunga na sungusungu miezi miwili kabla ya tukio na siku hiyo alikuwa na jukumu la kutayarisha kuni na vyombo vya kupikia.
Alidai kuwa aliondoka kwenda kumhudumia mjukuu wake aliyekuwa mgonjwa na hivyo hakushuhudia lolote kuhusiana na mauaji hayo. Wakati wa kuhojiwa, hakumtaja mtu yeyote.
Naye mshtakiwa wa tano, Mariam kwa upande wake alidai kuwa alikuwa na wiki mbili tangu ajiunge na sungusungu, na jukumu lake siku hiyo lilikuwa kupika kwani alikuwa na mtoto mchanga wa mwaka mmoja na miezi minne. Alidai baada ya kula chakula cha mchana, aliondoka kuelekea kijiji cha Chibelela.
Mshtakiwa wa sita ambaye ni Tatu, alisema alienda kwenye mkutano huo kwa ajili ya kupika. Alikana kumtaja mtu yeyote kushiriki katika tukio hilo alipokuwa akihojiwa.
Naye Pendo ambaye ni mshtakiwa wa saba, alikana kushiriki katika tukio hilo. Alieleza kuwa alikuwa sungusungu mpya na alikuwa na siku 11 tu tangu ajiunge, hivyo hakushiriki jukumu lolote wakati wa mkutano huo wa Desemba 17, 2022.
Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili Jaji Longopa alianza kwa kueleza kuwa kanuni zinazoongoza kesi za jinai,zinaeleza ni jukumu
la upande wa mashitaka kuthibitisha kesi pasipo kuacha shaka yoyote.
Huku akinukuu kesi iliyotolewa uamuzi na Mahakama ya Rufani nchini, Jaji alieleza kuwa imewekwa sheria kwamba pale watuhumiwa wakifanya kosa kwa pamoja ili kutimiza nia husika kila mmoja atawajibika kwa kosa hilo kama litathibitishwa.
Jaji alieleza kuwa baada ya kuchunguza kwa makini ushahidi kwa ujumla, Mahakama imeona ushahidi wa upande wa mashitaka uliotolewa haujathibitisha kosa dhidi ya watuhumiwa hao, ikiwemo utofauti wa muda aliofariki Beritha pamoja na uchunguzi wa mwili huo.
“Hakuna hata mmoja wao aliye na hatia ya kosa la mauaji kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu, kama ilivyoshtakiwa, Mahakama inawaachia huru washtakiwa wote saba,” alihitimisha Jaji.