MWENYEKITI wa Chama cha Soka Mkoa wa Mwanza (MZFA), Vedastus Lufano ametetea nafasi hiyo, baada ya kupita bila kupingwa akipigiwa kura za ndio na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho, huku Khalid Bitebo akipitishwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti.
Lufano ameshinda nafasi hiyo katika mkutano mkuu wa uchaguzi wa chama hicho uliofanyika juzi, jijini Mwanza baada ya aliyekuwa mpinzani wake, Frank Deogratias kujiengua siku moja kabla ya uchaguzi huo na safu hiyo itakiongoza chama hicho hadi mwaka 2028.
Katika uchaguzi huo ambao umesimamiwa na Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi MZFA, Alhaji Majogoro, wagombea katika nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Kelvin Chela na wajumbe wa kamati tendaji MZFA, Bernad Jackson na Almasi Moshi nao wameshinda nafasi hizo kwa kupita bila kupingwa.
Baada ya ushindi huo, Lufano alimpendekeza Khalid Bitebo kuwa Makamu Mwenyekiti, Domit Chisena kuwa mjumbe wa mkutano mkuu na Leonard Malongo kuendelea na ukatibu mkuu wa chama hicho na wajumbe wa mkutano huo waliyapitisha majina hayo bila kupingwa.
Akizungumza ushindi huo, Lufano alisema kazi iliyopo ni kufungua ukurasa mpya, kuvunja makundi na kufanya kazi kwa pamoja kwa manufaa ya soka la Mwanza huku akiwaomba wanachama kusimamia dira ya chama hicho na kutimiza majukumu yao.
“Tunaosimamia mpira lazima tuonyeshe nidhamu ya kweli mpira wa sasa hauhitaji mizengwe zama za huko nyuma tunaachana nazo. Wajumbe tuwe waadilifu na tuheshimiane karibuni kwangu milango iko wazi ukiwa na shida ya mpira ili tuendeshe mpira kisasa kuwe na utulivu na nidhamu,” alisema Lufano.
Ofisa Michezo Mkoa wa Mwanza, William James ameutaka uongozi mpya wa chama hicho kuwa na dira itakayowaongoza na kufanya kazi kwa kufuata katiba ili kuepuka migogoro kwani wadau wana matarajio makubwa kuona soka linapiga hatua kama ilivyo kwenye majiji mengine nchini.
Mwenyekiti wa Kamati ya uchaguzi huo, Alhaji Majogoro amewashauri viongozi wapya kuwa tayari kukosolewa na kutibu majeraha na vidonda ambavyo vimejitokeza katika uchaguzi ili kutengeneza Mwanza moja na kuendeleze soka.
“Mjifunze katika uongozi wenu uliopita muone mliyoyafanya yana tija kiasi gani na mnajifunza kitu gazi.”