Uchaguzi Serikali za Mitaa: ACT-Wazalendo wamtumia ujumbe Rais Samia

Dar es Salaam. Wakati mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa ukiwa katika hatua ya uteuzi wa wagombea, Chama cha ACT Wazalendo kimemtaka Rais Samia Suluhu Hassan kusimamia mambo matatu ikiwemo kuhakikisha uteuzi huo unafanyika kwa kuzingatia haki.

Pia, wanamtaka azuie vitendo vya makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na wasimamizi wa uchaguzi kuwatisha na kuwashawishi wagombea wa upinzani kujiondoa kuwania nafasi hizo.

Pia  kuhakikisha sheria na kanuni zinazingatiwa katika hatua zilizosalia kwenye uchaguzi huo hasa uapishwaji wa mawakala, upigaji kura, kuhesabu kura na utangazaji wa matokeo.

Msingi wa wito huo kwa Rais dhidi ya uchaguzi huo utakaofanyika Novemba 27, 2024 yanasadifu kile kilichokuwa kinalalamikiwa na vyama vya upinzani nchini vikidai vinafanyiwa vurugu na rafu na wasimamizi wa uchaguzi huo.

 Hayo yamesemwa na Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu leo Jumapili, Novemba 3, 2024 kupitia taarifa yake kwa umma baada ya kamati ya uongozi ya chama hicho kukutana kwenye kikao chake cha kawaida kujadili masuala mbalimbali ikiwamo uchaguzi huo.

Chama hicho kimemkumbusha Rais Samia kusimamia vyema falsafa yake ya 4R anazozitumia kwenye utawala wake ambazo ni  maridhiano (Reconciliation), mabadiliko (Reforms), ustahimilivu (Resilience) na kujenga upya (Rebuilding).

“Uchaguzi wa serikali za mitaa utatumika kupima iwapo ana nia ya dhati ya kujenga misingi imara ya kidemokrasia nchini kupitia falsafa yake ya 4R. Chaguo lipo mikononi mwake na wakati sahihi wa kuamua ni sasa,” amesema Semu.

Shughuli ya uchukuaji na urejeshaji fomu za kuomba kuteuliwa kuwania nafasi kwenye vijiji 12333, vitongoji 64274 na mitaa 4269 vitakavyoshiriki uchaguzi huo ilianza Oktoba 26 hadi Novemba 1, 2024 na kwa sasa uteuzi wa wagombea unaendelea.

Kampeni ya kura ya hapana

Semu amesema kamati hiyo imetoa maelekezo kwa Ofisi ya Katibu Mkuu wa chama hicho kuwasiliana na vyama vingine vya siasa na wadau wa demokrasia, ili kuandaa kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha umma kupiga kura ya hapana kwa  wagombea wa CCM waliobaki peke yao.

“Chama kiendelee na mpango kabambe wa kampeni na kulinda kura kwenye maeneo yote ambayo ACT Wazalendo kina wagombea ili kuwapa nafasi wananchi kupata uwakilishi bora katika vijiji, mitaa na vitongoji vyao,” amesema

Semu amesema kamati hiyo inamtaka Katibu mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu kumwandikia msimamizi wa uchaguzi orodha ya wagombea wote wa ACT Wazalendo walioshindwa kuchukua na kurejesha fomu, kwa sababu ya wasimamizi wa uchaguzi kutofungua ofisi.

“Tunafanya hivi ili wagombea husika warejeshwe kwenye orodha ya wagombea. Ilani ya uchaguzi izinduliwe wiki moja kabla ya tarehe ya kampeni kuanza,” amesema.

Related Posts