USHINDI mtamu hasa unaposhinda kwa timu kubwa kama Yanga na hii imethibitishwa na kocha wa Azam FC, Rachid Taoussi aliyesema pointi tatu ilizopata timu hiyo mbele ya Yanga ni kielelezo cha mipango imara na nidhamu ya hali ya juu kutoka kwa wachezaji, huku akiweka wazi lengo ni kujiimarisha na kuwa klabu tishio zaidi nchini.
Mkwara wa Taoussi umekuja baada ya kuifyatua Yanga bao 1-0 katika pambano kali la Ligi Kuu juzi kwenye Uwanja wa Azam Complex na Mmorocco huyo licha ya kuwashukuru mashabiki wa Azam FC kwa kuwaunga mkono, alisema kiu yake ni kuendeleza ubabe Bara.
Ushindi huo ni wa pili mfululizo kwa Azam dhidi ya Yanga Ligi Kuu Bara ikiwamo wa msimu uliopita na kutibua rekodi kadhaa ilizokuwanazo vinara na watetezi hao wa ligi hiyo, umeifanya Azam ishike nafasi ya nne kwa kufikisha pointi 21 baada ya mechi 10.
“Nawashukuru mashabiki wetu kwa kutuunga mkono, tunahitaji zaidi ya hapo kwa sababu sisi ni klabu kubwa. Kuanza kushinda dhidi ya klabu yenye nguvu kama Yanga ni hatua nzuri sana kwetu,” alisema.
Akizungumzia maandalizi ya mechi hiyo, alisema walihakikisha wanadhibiti kasi ya washambuliaji wa Yanga kwa kupanga safu ya ulinzi iliyokuwa imara. Alisema walitengeneza “block compact” kwa lengo la kuziba mianya ya Yanga kutumia kasi na ufundi wao, hasa kwa washambuliaji wao hatari. “Tulifanya mpango mzuri wa kuweka uwiano kati ya mashambulizi na ulinzi, na hilo liliweza kutusaidia sana. Wachezaji walikuwa na nidhamu kubwa, kila mmoja alitoa asilimia mia moja yake,” alisema kwa furaha na kuongeza; “Kila mchezaji alifanya kazi yake vizuri na napenda kuwashukuru kwa hilo.”
Taoussi alieleza ameanza kuona maendeleo makubwa kwa Azam tangu ajiunge na timu hiyo miezi miwili iliyopita na hatua kwa hatua wamekuwa wakiongeza ubora wao.
Alisema kazi aliyofanya hadi sasa inaonekana uwanjani na wanaendelea kujijenga kuwa timu yenye ushindani mkubwa.
Katika kuonyesha umakini wake kwenye mchezo huo, alisema walijitahidi kuepuka kupoteza pointi kwenye mchezo huo na kuwapongeza wachezaji wake kwa kutekeleza maagizo yake kikamilifu. “Tulijua umuhimu wa kutoiacha Yanga kupata nafasi, na wachezaji walifanya vizuri sana,” alieleza.
Alipoulizwa kuhusu uamuzi wake wa kumrejesha mshambuliaji wake, Nassor Hamoud, kutoka kwenye timu ya taifa kwa ajili ya mchezo huo, alifafanua, ilikuwa ni hatua ya kimkakati kutokana na umuhimu wa mchezaji huyo katika mipango yake ya ushindi.
“Tuliheshimu timu ya taifa, lakini tulihitaji huduma yake kwa ajili ya mchezo huu na naishukuru bodi kwa kufanikisha hilo,” alisema.
Taoussi pia alionyesha furaha yake kwa namna timu yake ilivyochukua jukumu la kujilinda kwa umakini. Alisema washambuliaji wake si tu walikuwa wakishambulia bali pia walikuwa mstari wa mbele kwenye ulinzi.