KIUNGO mshambuliaji wa Alliance Girls, Elizabeth John amesema licha ya kudondosha pointi tano anaona mwanzo ni mzuri kwao.
Alliance ilianza kupoteza mechi ya kwanza 3-1 mbele ya JKT Queens kisha kutoa suluhu na Yanga Princess, Nyamagana mkoani Mwanza.
Kinda huyo alisema msimu uliopita walipoteza mechi mbili za kwanza jambo lililowafanya wapige hesabu za vidole katika mechi za mwisho walipokuwa katika hatari ya kushuka daraja.
Aliongeza kuwa msimu jana walipandishwa vijana 10 kutoka kwenye akademi ambao hawakuwa na uzoefu kwenye ligi akiamini sasa ni muda wao wa kuonyesha vipaji.
“Msimu jana tulikuwa tunapata dakika chache za kucheza naona sasa tumeanza kuzoea ligi kutokana na mwanzo hatukuwa tunapata nafasi kubwa ya kucheza,” alisema na kuongeza:
“Kwa upande wangu kitu kikubwa ambacho kocha amekuwa akinisisitiza sana ni namna ya ku-press wapinzani na kupitisha pasi kwa washambuliaji, jambo ambalo awali sikuwa nafanya na sasa nimeanza kubadilika tofauti na msimu uliopita.”