Dar es Salaam. Wakati shughuli za kiuchumi zikitajwa kuwa sababu ya wakazi wa jijini hapa kuongoza kwa kuchukua mikopo, wachumi wametaka kuangaliwa namna kanda nyingine zinavyoweza kunufaika na fursa hiyo.
Hiyo ni baada ya takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuonyesha asilimia 56.7 ya mikopo ya Sh32.089 trilioni iliyotolewa mwaka 2023/2024 ilichukuliwa na wakazi wa Jiji la Dar es Salaam pekee.
Ripoti hiyo ya uchumi wa kikanda ya mwaka 2023/2024 inaonyesha kanda nyingine tano zinazobakia zimekuwa na uchukuaji hafifu wa mikopo hiyo, ambapo Dar es Salaam ilifuatiwa na Kanda ya Ziwa iliyokuwa na asilimia 13.3 pekee.
Kanda nyingine ni ya kati yenye asilimia 11.4, ya kaskazini asilimia 10, kusini mashariki ikiwa na asilimia 4.8 huku nyanda za juu kusini ikiwa na asilimia 3.8.
“Dar es Salaam inabebwa na shughuli za kiuchumi lakini uchumi wake unategemea sana kuingiza bidhaa na kuuza, kanda nyingine zinaweza kunufaika na mikopo hii ikiwa shughuli nyingi za kiuchumi zitaanzishwa katika maeneo yao kuendana na aina ya uzalishaji wa mazao wanayofanya,” amesema Profesa Aurelia Kamuzora, mtaalamu wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe.
Amesema kinachopaswa kufanyika ni kubainisha bidhaa katika kila mkoa kwa kugundua vitu vya asili vilivyopo na vilivyo na utofauti viinuliwe ili mkoa uweze kuwa maarufu kwa kitu fulani.
Akitolea mfano wa mkoa kama Kigoma ambao ni wazalishaji wa samaki kutoka Ziwa Tanganyika wajulikanao kama migebuka, alitamani kichukuliwe kama kitu kinachoweza kuwa utambulisho maalumu wa mkoa huo na kubebwa kwa uzito wake kupitia uongezaji wa thamani na zikauzwa nje ya nchi kutokea mkoani humo.
“Tukibadilika na kujikita katika uzalishaji, mikoa inayozalisha itakua haraka, tutumie mapinduzi ya viwanda kwa kila mkoa kuwa na kiwanda kuendana na mazao wanayozalishwa, ili kuongeza thamani ya bidhaa hizo na kuuza kwenda nje ya nchi katika masoko yanayohitaji siyo kuuza bidhaa ghafi.”
“Kufanya hivyo kutachochea uwekezaji wa viwanda vingi, uzalishaji wa ajira kwa vijana wanaozunguka eneo husika, kukua kwa shughuli nyingine za kiuchumi zinazohitaji mikopo,”amesema.
Kwa upande wake, Dk Timothy Lyanga kutoka Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), amesema baadhi ya kanda zinaonekana kuwa na kiwango kidogo cha uchukuaji wa mikopo kwa sababu shughuli kubwa zilizotawala ni kilimo.
Jambo hilo linafanya wao kuhitaji zaidi pembejeo badala ya fedha kwa ajili ya kutimiza majukumu yao ya kila siku.
Pia uwepo wa wafanyabiashara wengi ambao shughuli zao hazijarasimishwa inatajwa kuwa sababu nyingine ya ufikiaji wa mikopo inayotolewa na taasisi mbalimbali, jambo ambalo ni moja ya kigezo kinachoangaliwa sana na wakopeshaji.
“Tunachoweza kufanya ni kurasimisha biashara au shughuli za kimkakati katika kanda husika, kila kanda ina shughuli au mazao, biashara za kimkakati. Mfano kanda ya magharibi mkoa wa Kigoma kuna zao la chikichi hivyo ni vyema kuhakikisha Serikali inahamasisha uwepo wa vikundi vinavyolima na vinavyokamua mafuta,” amesema Dk Lyanga.
Amesema hilo linaweza kufanywa na Serikali kupitia wizara na taasisi zake zinazohusiana na biashara za kimkakati ili kuhakikisha biashara zinafanywa na vikundi rasmi ili waweze kukopesheka na taasisi za kifedha.
“Mikopo ni kitu kinachochangamsha uchumi wa mtu, Taifa kwa ujumla na inapunguza umasikini katika ngazi ya kaya. Hili linaenda sambamba na kuongeza mchango katika pato la Taifa inapotumika sahihi hivyo ni vyema kuangalia namna ambavyo fursa hiyo inaweza kuwafikia wote,” amesema Dk Lyanga.