Utitiri wa bodaboda, bajaji vurugu tupu

Dar es Salaam. Licha ya usafiri wa pikipiki na bajaji kuonekana mkombozi kwa abiria, vyombo hivyo vimelalamikiwa kwa uvunjifu wa sheria za barabarani na kuwa kero kwa watumiaji wengine.

Malalamiko hayo ni pamoja na madereva wa vyombo hivyo kutojali watumiaji wengine huku wakijiona kuwa na haraka kiasi cha kutozingatia sheria za usalama barabarani na hata kusababisha ajali.

Makosa mengine ni kutokuzingatia taa za barabarani, kubeba mizigo mikubwa na abiria wengi kupita uwezo wa chombo (mishikaki) na kuhatarisha usalama wa abiria na watumiaji wengine wa barabara.

Malalamiko hayo yanakuja wakati ikibainika Sheria ya Usalama Barabarani kuwa na upungufu unaoshindwa kudhibiti vyombo hivyo.

Pia, imebainika vyombo vya udhibiti likiwamo Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Usafiri wa Ardhini (Latra) kuelemewa na idadi kubwa ya vyombo hivyo.

Kutokana na malalamiko hayo, kumekuwa na mivutano kati ya madereva wa bajaji na magari ya abiria katika majiji ya Arusha na Mbeya, huku Dar es Salaam vurugu zikitamalaki barabarani.

Baadhi ya watumiaji wa barabara wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti wamesema ili kupunguza ajali barabarani zinazoendelea kuleta hasara katika jamii, kundi hilo linapaswa lidhibitiwe.

“Bodaboda na bajaji wanajiona watoto pendwa hawafanywi lolote na wakati mwingine wakikamatwa adhabu wanapewa ndogo, huku barabarani ni vurugu usipokuwa makini wanakusababishia ajali au hasara kubwa,” amesema Zabron Mwasapile ambaye ni dereva wa gari.

 Amesema madereva wa pikipiki na bajaji hujiona wana haraka muda wote kuliko wengine na ndio sababu ya kuwakosesha utulivu na umakini watumiaji wengine.

Gaudensia Mlawa amesema, “niliwahi kupata ajali nikiwa kwenye usafiri wa bodaboda maeneo ya Stop Over Kimara, baada ya dereva kulipita lori, nilishamwambia tutembee mwendo wa wastani lakini alidai ana haraka.”

Mtumiaji wa usafiri huo, Mtulia Joseph amesema vyombo hivyo vimekuwa msaada kwake hasa pale anapohitaji kuwahi kazini.

“Pikipiki zimekuwa msaada mkubwa kwa sababu nikitaka kuwahi kazini lazima nitumie bodaboda na inanisaidia hata nisigombane na mabosi zangu,” amesema Joseph.

Mwenyekiti wa Chama cha Bodaboda jijini Dar es Salaam, Charles Massawe amesema kabla ya kuwalaumu ni muhimu kwa mamlaka na jamii kuangalia kwanza mzizi wa tatizo.

 “Si wote wanaovunja sheria au kubeba mizigo inayochukua sehemu kubwa ya barabara, ni baadhi; na hao wanaobeba ni kulingana na ugumu wa maisha wanayopitia, unaweza kukaa kijiweni toka asubuhi hadi jioni hujapata mteja, ukipata kazi, inakuwa ngumu kukataa,” amesema Massawe.

Massawe amesema kundi hilo kuwa na idadi kuwa ya watu waliojiajiri kupitia kazi hiyo, inasababishwa na wengi kukosa ajira na wanakimbilia katika sekta hiyo.

 “Watu wakihitimu kidato cha sita na chuo wanakimbilia udereva boda boda na kuna watu wanapunguzwa kazi wanakimbilia huku kwenye sekta yetu, kwa hiyo inatokana na uhalisia wa maisha ya sasa na kila siku idadi inaongezeka,”amesema Massawe.

Alipoulizwa kuhusu kundi hilo kuongoza kwa kuvunja sheria za barabarani, katika majibu yake Massawe amesema uvunjaji wa sheria ni hulka ya mtu binafsi.

 “Kundi letu linahukumiwa kwa sababu ya vyombo tunavyotumia na labda tunaonekana sana, ni wangapi wapita barabarani tena kwenye mataa wakiwa na magari ya kifahari bila kusimama ni wengi,” amesema

Katibu wa Shirikisho la Bodaboda Ukonga, Huruma Lugala amesema katika kutafuta riziki kuna mambo mengi yanajitokeza, ili kuwadhibiti inahitajika watengenezewe mazingira ya ufanyaji kazi.

Amesema kwa hali ilivyo sasa hata polisi ni vigumu kuwakamata, kwa kuwa mbinu ya kutumia askari kanzu sasa imeshindikana.

Amesema katika shirikisho lao huwa wanakumbushana kwa kupeana elimu na anayekiuka sheria, huwa wanamuwekea vikao na ikishindikana wanamtimua.

“Chama chetu kina wanachama 300 na kimekuwa kikikua kila siku kulingana na uhalisia wa maisha na sekta nzima imekuwa ikikua lakini baadhi, sio bodaboda ni wezi,” amesema.

Dereva wa bajaji, Mathayo Amos amesema usafiri wao unapendwa na wengi kwa sababu haubebi abiria wengi, huku akieleza ni chanzo cha wenye magari kuwaona kama wanafaidi.

“Sheria tunafuata lakini shida iliyopo barabara zetu ni ndogo hasa hapa Dar es Salaam foleni muda mwingi ndiyo maana kuna kuwa na vurugu barabarani,” amesema Amos.

Polisi kuja na mkakati mpya

Akizungumzia malalamiko hayo, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Ramadhani Ng’azi amekiri kuwepo kwa changamoto ya kuwadhibiti madereva wa bodaboda na bajaji.

Hivyo, amesema kuna makakati mpya wa kudumu wanaouandaa wa kuja na sheria ya kuwadhibiti kwa mfumo wa mtandao.

“Katika vyombo vya usalama barabarani, pikipiki na bajaji ni vyombo vya moto vya usafiri vinavyoongoza kwa uwingi hapa nchini kuliko vyombo vingine vyote, ni zaidi ya asilimia 75 ya vyombo vyote vya moto,” amesema.

Ng’azi  amesema uwingi wake unaleta usumbufu, kwa kuwa Sheria ya Usalama Barabarani wakati inaanzishwa hawakuweka pikipiki kama chombo cha kusafirisha abiria, lakini Serikali ilifungua milango kuruhusu vijana wajiajiri kupitia eneo la usafirishaji.

“Mkakati mkubwa tunaokuja nao tunakusudia kubadilisha sheria zetu ili usajili wa kusafirisha abiria kupitia pikipiki usimamiwe kuanzia kuwatambua, nani amenunua na kuwapa vituo maalumu kama Kinondoni zitakaa kumi, kama hawatoshi tutaongeza,” amesema Ng’azi.

Amesema lengo la kufanya hivyo ni kutengeneza urahisi wa kuwasimamia na kuwafuatilia huku akiongeza wanataka usimamizi wao uwe katika mfumo wa kimtandao.

“Tumeshapata mashirikisho yao na wanajisajili na wanapewa namba kama barcode na mwisho wa siku polisi tukija kufunga vifaa vya ufuatiliaji barabarani kama kamera tutaweza kuwafuatilia kirahisi,” amesema.

Ng’azi amesema wakifanya hivyo itakuwa rahisi kuwakamata hasa pale wanapovunja sheria kama kwenye taa na kuvuka kwenye alama za pundamilia.

“Ni lazima tulidhibiti kundi hili kwa sababu ni kundi linaloongoza kwa kupata ajali mara kwa mara kuliko watu wengine wowote, lazima tuje na mkakati wa kudumu,” amesema.

Ng’azi amesema wanachokifanya sasa Polisi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) na mamlaka zingine za halmashauri wanapanga kuja na mpango wa kudhibiti kundi hilo.

 “Tutatengeneza mfumo mzuri wa kudumu wa kudhibiti biashara yote ya bodaboda na bajaji, kwa sababu barabara zetu ni zilezile, watu wameongezeka na tunaongeza vyombo vya moto na matokeo yake kuna uvunjifu mkubwa wa sheria,”amesema Ng’azi. 

Amesema katika sheria hiyo wanayokuja nayo itawagusa hadi kampuni zinazoingiza pikipiki kutoka nje ya nchi kwa kuwa hakuna sheria inayowasimamia kujua kama zinatosha.

“Itagusa mtu yeyote anayetaka kuanzisha biashara ya bodaboda hata iwe kwa kumpatia kijana kuendesha bila kujua ana mafunzo au vipi,” amesema Ng’azi

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri Ardhini (Latra) Habibu Suluo amesema ukiukwaji wa sheria ni mkubwa na taasisi hiyo haiwezi kuwa kila mahali.

“Idadi ya pikipiki ni kubwa na watumiaji ni wengi na tupo kwenye juhudi ya kuanzisha vyama na kuweka mawakala katika eneo hili, ili watusaidie utoaji leseni na sehemu kubwa kwa pikipiki zinatolewa na halmashauri,” amesema.

Suluo amesema hata ukusanywaji wa takwimu ni lazima wawasiliane na halmashauri zinazotoa kwa mfumo wa kawaida na kuingizwa kwenye mfumo mtandao wa Latra.

Mkuu wa Idara ya Usafirishaji na Biashara wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji, Dk Prosper Nyaki, amependekeza mambo manne ya kuwadhibiti ikiwamo kuundwa kwa sheria na adhabu wanazopewa zinapaswa kuwa kubwa.

“Pia, tunapaswa kuboresha miundombinu ya barabara iwe vizuri na kuwataka wanasiasa kuacha kuingilia masuala ya kisheria, kufanya hivyo kutajenga nidhamu,” amesema.

Akijenga msingi wake Dk Nyaki amesema bodaboda na bajaji wako huru kwa kuwa hawasimamiwi na walitakiwa kuwa na sheria na wapangiwe njia kama ilivyo upande wa daladala.

“Kama haiwezekani kuwapa njia wangefanya ufuatilia kama wanavyofanya kwenye mabasi yanayoenda mikoani, bodaboda namba fulani ametembea kwa mwendo kasi na iko sehemu fulani,” amesema Dk Nyaki.

 Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917

Related Posts