ZRA yakusanya asilimia 102 ya mapato

Pemba. Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), imesema ongezeko la ukusanyaji wa mapato umekuwa ukiimarika sababu kubwa ikitajwa matumizi ya mifumo na kutatua changamoto za walipa kodi.

Akitoa taarifa ya makusanyo kwa waandishi wa habari leo Jumapili Novemba 3, 2024, Kaimu Kamishna Mkuu wa ZRA, Said Ali Mohamed amesema ongezeko hilo pia limetokana na kuimarishwa kwa miundombinu ya kiuchumi nchini.

Amesema kwa Oktoba 2024, ZRA ilikadiriwa kukusanya Sh74.549 bilioni lakini imevuka lengo kwa kufanikiwa kukusanya Sh76.528 bilioni sawa asilimia 102.65.

Mohamed amesema makusanyo hayo ni ongezeko la Sh15.326 bilioni ikilinganishwa na makusanyo ya Oktoba 2023 na ongezeko hilo limechangiwa na usimamizi na miongozo kutoka kwa viongozi wao.

“Mamlaka ya Mapato Oktoba mwaka huu tumefanikiwa kukusanya bilioni 76.528 ikiwa mamlaka hiyo ilikadiriwa kukusanya bilioni 74.549 sawa na ongezeko la asilimia 102.65,” amesema.

Aidha, amesema kwa kipindi cha mwaka wa fedha ulioanza Julai hadi Oktoba 2024/25, mamlaka imekusanya Sh277.46 bilioni ikiwa ni ongezeko la Sh69.365 bilioni ukilinganisha na makusanyo ya mwisho wa mwaka wa fedha wa 2023/24, walikusanya wastani wa Sh59.90 bilioni kwa mwezi.

Akizungumzia mwenendo huo, Mkurugenzi wa ZRA Pemba, Jamal Hassan Jamal amewashukuru wananchi wa Zanzibar hasa kwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa mamlaka hiyo katika kazi yake ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Amewasisitiza waendelee kushirikiana zaidi kwa kudai risiti za kielektroniki kila wanapokwenda kununua bidhaa zao.

‘’Tunawashukuru wananchi kwa kutupa ushirikiano katika ukusanyaji wa mapato kwa hiari, kwani ndiyo yanayotumiwa na Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini na nawaomba muendelee kushirikiana nasi kwa kudai risiti za kielektroniki wakati mnapofanya manunuzi,’’ amesema Jamal.

Related Posts