Wakazi wa Butiama waaga mwili wa Jenerali Musuguri, kuzikwa kesho

Butiama. Balozi wa Tanzania Nchini Zimbabwe,  IGP mstaafu Simon Sirro amewaongoza wakazi wa Butiama na maeneo jirani pamoja na  baadhi ya maofisa wa jeshi la wananchi na familia  kuaga mwili wa mkuu wa majeshi mstaafu, Jenerali David Musuguri katika Kijiji Cha Butiama Wilaya ya Butiama.

Jenerali Musuguri alifariki dunia Oktoba 29, 2024 katika hospitali ya Kanda Bugando jijini Mwanza alipokuwa akipatiwa matibabu, atazikwa nyumbani kwake Butiama kesho  Jumatatu Novemba 4, 2024 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dotto Biteko anatarajiwa kuongoza maziko hayo.

Akizungumza leo Novemba 3, 2024 baada ya kutoa heshima za mwisho, Balozi Sirro amesema Jenerali Musuguri wakati wa uhai wake aliongozwa na mambo makuu matatu ambayo ni ujasiri, uzalendo na mapenzi ya dhati kwa Watanzania.

Amesema maisha ya Musuguri yanapaswa kutumika kama kielelezo na rejea kwa viongozi wa Serikali na jamii kwa ujumla.

“Musuguri kupitia maisha yake ya uongozi anatukumbusha kuwa ukipewa nafasi ya kuwa kiongozi hasa wa Serikali jambo kubwa unalotakiwa kufanya kwanza ni kuwa na mapenzi ya dhati kwa watu unaowaongoza, lakini pia unatakiwa kuwa mzalendo kwa nchi yako kwani hauna nchi nyingine zaidi ya hii Tanzania, ” amesema.

Sirro amesema atamkumbuka kwa mengi marehemu Jenerali Musuguri ikiwepo namna ambavyo alimpigia simu alfajiri ya siku alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Polisi nchini, akimtaka kufanya kazi kwa kuzingatia maadili, uadilifu, uzalendo na kuwapenda Watanzania.

“Alinipigia simu alfajiri akinipongeza lakini alinitaka nihakikishe nafanya kazi kwa uadilifu nizingatie sheria na maadili, aliniambia kabila letu ni dogo hivyo kwa nafasi niliyopata natakiwa kuendelea kutunza heshima ya kabila letu, lakini hilo litawezekana pale nitakapofanya kazi kwa kuzingatia misingi hiyo aliyoniusia,” amesema.

Baadhi ya wakazi wa Butiama na maeneo jirani wakitoa heshima za mwisho kwenye jeneza lenye mwili wa Mkuu wa Majeshi mstaafu, Jenerali David Musuguri kijijini Butiama.  Picha na Beldina Nyakeke

Amesema Taifa limepoteza kiongozi muhimu kwani  wanaojua historia wanajua Musugri  amelifanyia nini Taifa la Tanzania na watu wake, huku akisema ushiriki wake katika vita ya Kagera ni kielelezo cha namna gani alivyokuwa na mapenzi ya kweli kwa Watanzania.

Mkurugenzi wa Mfuko wa Mwalimu Nyerere,  Joseph Butiku amesema Musuguri alifanya kazi kubwa kwa Taifa na watu wake hivyo atakumbukwa daima.

Amesema Jenerali Musuguri alikuwa ni mpenda haki na wakati wa uongozi wake aliwaongoza watu kwa kuzingatia haki jambo ambalo lililomuwezesha  kufanikisha masuala mengi ikiwemo ushindi wakati wa vita ya Kagera.

“Vijana walimpenda kwa sababu alikuwa akiwatendea haki na ndio maana hata kwenye vita walihakikisha wanashinda na ingekuwa tofauti tusingepata ule ushindi, lakini pamoja na yote pia alikuwa mtu wa nidhamu ya hali ya juu na alikuwa na uwezo mkubwa wa kuongoza,” amesema Butiku

Butiku amesema licha ya kutokuwa na elimu kubwa lakini kutokana na ujasiri, uzalendo na mapenzi na watu marehemu aliweza kuongoza vizuri na kupata mafanikio makubwa, hivyo viongozi wanapaswa kujifunza kupitia kwake.

Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Butiama wamesema mbali na kuwa kiongozi mkubwa nchini lakini Musuguri alikuwa ni mtu mwenye mapenzi na kila mtu, hata baada ya kustaafu aliporudi kijijini Butiama aliishi vizuri na wakazi wa kijiji hicho.

“Wingi wa watu hapa leo ni kielelezo kuwa huyu mtu alikuwa mtu wa aina gani hakujali cheo chake alikuwa akimsikiliza kila mtu na alikuwa sehemu ya utatuzi wa shida za watu iwe binafsi au kijamii, wana Butiama tumempoteza mtu wa muhimu sana,” amesema Esther Mahera.

“Hata wasaidizi wake ilibidi wakubaliane na hali halisi kwa sababu yeye alikuwa mpenda watu hivyo alikuwa akipokea watu wengi, na hakutaka mtu yeyote azuiliwe kumuona kwa hiyo wasaidizi wakawa hawana namna zaidi ya kukubaliana naye,” amesema Thomas Kinyonyi.

Related Posts