Diarra, Camara mwanzo mpya | Mwanaspoti

KWA miaka mingi iliyopita katika soka, makipa walichukuliwa kuwa na kazi moja tu, nayo ni kuzuia mpira usiingie wavuni.

Kipa alikuwa ni mchezaji pekee anayeweza kutumia viungo vyake vyote katika soka ikiwemo mikono, akiwa amevaa jezi tofauti na wenzake na alionekana kuwa tofauti kabisa na wengine uwanjani.

Kwa miaka ya hivi karibuni, maisha ya makipa yamebadilika na mabadiliko hayo yamekuwa na faida kubwa kwenye soka ila athari zake pia ni kubwa.

Mifumo hiyo mipya ndiyo imeletwa nchini, kuanzia usajili wa Djigui Diarra, Ayoub Lakred pamoja na Moussa Camara tumeona mabadiliko makubwa ya makipa katika soka letu, lakini kumbuka mabadiliko haya ya makipa ndiyo yamewaondoa relinii makipa wengi Ulaya na kuingiza sura mpya ndani ya timu zao.

Diarra na Camara ndio wanaongoza kwa clean sheet kwa sasa kila mmoja akiwa na saba huku timu zao zikicheza meschi tisa wakipoteza moja moja.

Mwanzoni mwa karne ya 20 makipa walikuwa wanaruhusiwa kudaka mpira sehemu yoyote kwenye eneo la nusu ya timu yake, yaani kutoka katikati kwenda langoni kwake.

Kanuni hiyo ilibadilishwa mwaka 1912, na kuwalazimisha makipa kudaka mpira kwenye eneo lake la ndani ya 18 tu.

Mwaka 1992, kanuni ya kurudisha mpira kwa kipa ilibadilishwa na sasa alikuwa hana ruhusa tena ya kuudaka ule uliorudishwa kwake kwa mguu makusudi, bali aliruhusiwa kudaka kama umerudishwa kwa kichwa, kifua au bega.

Kutokana na hali hii iliwalazimisha makipa kuongeza uwezo mkubwa kwenye miguu yao, mipira ilipokwenda kwao wakati mwingine walituliza, walipiga chenga na kutoa pasi. Kanuni hii ndiyo ilimaliza utegemezi wa mikono kwa makipa duniani.

Makipa ambao wameshindwa kubadilika wamekuwa wakiruhusu mabao ya hovyo na wakati mwingine walipiga mpira na kumpasia adui au walitoa pasi mbovu kwa mabeki wao na kulazimisha madhara langoni, rejea bao alilofungwa Juma Kaseja kwenye mchezo kati ya Yanga na Simba michuano ya Mtani Jembe, likiwekwa wavuni na Awadhi Juma.

Lakini kwa heshima kubwa ni sahihi kuamini kuwa mfumo huu wa makipa wa kisasa hapa nchini ulianzishwa na Juma Kaseja, alikuwa na uwezo mkubwa mguuni, alikuwa anaweza kumpiga mshambuliaji chenga, na hata mechi za mabonanza au mazoezini Kaseja alikuwa anacheza kama kiungo au mshambuliaji.

Labda kwa wazawa ndiye kipa aliyekuwa na uwezo wa juu zaidi wa kutumia miguu yake yote vizuri na kwa mafanikio makubwa.

Kwa sasa ni dhahiri msingi wa makipa siyo kuzuia tu mpira kwenda wavuni bali kucheza kulingana na mfumo wa timu unavyotaka, kila kitu kuhusu timu kinaanzia kwao.

Sharti kubwa ya mfumo huu ni lazima kipa awe na uwezo mzuri wa kutumia miguu, kifua na wakati mwingine kichwa bila presha yoyote kwa kuwa mipira mingi zaidi hurudi kwake badala ya kwenda mbele.

Kipa wa kisasa ni lazima awe na uwezo wa juu wa kutuliza mpira, kupiga chenga ikibidi na kutoa pasi ya uhakika kwa mchezaji wake, badala ya mfumo wa zamani wa kupiga mpira mbele ili utoke langoni kwake.

Mazoezi mengi ya makipa kwa sasa siyo kuruka kama nyani, bali ni kuwa na uwezo wa kudaka lakini zaidi kuisaidia timu kumiliki mpira, ndiyo maana wakati mwingine Diarra anaweza kugusa mpira mara nyingi mguuni kwake zaidi ya Clement Mzize ndani ya dakika 90 za mchezo.

Mashambulizi sasa yanaanzia kwa makipa, awali kulikuwa hakuna sheria inayombana kipa kudaka mpira akirudishiwa na beki wake, lakini baada ya kanuni mpya ya kuudaka mpira kutoka kwa beki, au mchezaji mwenzake yoyote iliwalazimisha makipa kujifunza kitu kipya.

Kipa wa kisasa ni lazima awe anaweza kupiga pasi fupi, ndefu na wakati mwingine shuti kali ambalo litamfikia mchezaji wake ili kutengeneza shambulizi, mfano ni jinsi anavyofanya kipa wa Manchester City, Ederson kwa kipindi cha misimu minane ambayo amekaa kwenye timu hiyo, tayari ametengeneza mabao manne, yaani asisti nne.

Madhara makubwa ya mfumo huu wa makipa ni kuruhusu mabao yasiyotarajiwa, kwa kuwa makipa wamekuwa wakitakiwa kupiga pasi fupi, kupokea mipira mingi na kuiachia mara nyingi wamekuwa wakishindwa kuufikisha mpira kwa mlengwa na kujikuta wanafungwa mabao ambayo huzua gumzo.

Lakini kwa kuwa mfumo huu mpya unawafanya kuwa kama viungo zaidi kuliko makipa, wanalazimika kusogea na mpira mpaka hatua 10, kabla ya eneo la katikati ya uwanja, madhara yake makipa wa mfumo huu wamekuwa wakifungwa mabao mengi ya mbali.

Rejea bao alilofungwa kipa wa Simba, Camara dhidi ya Coastal Union na lile alilowahi kufungwa Diarra msimu uliopita na Seif Karihe wa Mtibwa Sugar yote yanatokana na mfumo huu.

Pia mabao mawili ambayo alifungwa kipa wa Manchester United, Andre Onana msimu uliopita wakati anatua kwenye timu hiyo ni moja ya madhara ya mabadiliko haya.

Mara nyingi wamekuwa wakianzisha mashambulizi au umiliki wa mpira kuanzia kwa mabeki wa kati, pembeni au wakati mwingine kiungo mkabaji ambaye anakuja na kuingia kwenye eneo la 18 la timu yake.

Baada ya kupiga pasi ya kwanza kipa anatakiwa kutoka kwenye eneo alipo na kutafuta nafasi ya kupasiwa tena mpira kama anavyofanya mchezaji mwingine wa ndani ya uwanja, mfumo huu unajulikana kama ‘sweeper keeper’.

Kama wapinzani wanaweza kuacha upenyo kidogo basi kipa anaweza kupiga pasi ndefu ambayo mara nyingi imekuwa na madhara makubwa sana kwa kuwa kinakuwa ni kitu ambacho wanakuwa hawajajiandaa nacho kwa wakati ule.

Kwa timu ambazo zinatumia makipa kuandaa mashambulizi zinaelezwa kuwa zimekuwa na nyongeze ya namba ya kutengeneza uwanjani kitu ambacho kinajulikana kama 11v10.

Hata hivyo, tofauti na mfumo wa zamani ambao makipa walikuwa wanapiga mpira juu unakwenda kushuka katikati au mbele ya katikati, wakati huu wamekuwa wakipiga mipira mingi usawa wa kati na inakuwa ni pasi sahihi badala ya kubahatisha.

Marc-André Ter Stegen: Barcelona

Hakuna shaka yoyote kuwa kipa huyu amekuwa zaidi ya makipa wengine duniani, amekuwa akitumika kama kiungo au mlinzi wa kati kutokana na ubora wake wa kuitumia miguu yake. Amekuwa na uwezo mkubwa sana wa kucheza one- two.

Ederson hakuna shaka kuwa anaenda na mfumo huu, lakini akiwa anaongeza jambo lingine kuwa na kiwango cha juu cha kupiga pasi ya mwisho ndiyo maana kwa sasa anaongoza akiwa na pasi nne za mabao ndani ya misimu nane Premier.

Alionyesha kiwango cha juu sana akiwa na Inter Milan akitumia mfumo huu wa kucheza nyuma, shida kubwa kwake akiwa na Man United ni aina ya walinzi alio nao ambao wameshindwa zaidi kuendana na kasi ya kipa huyo.

Alisson Becker, Liverpool

Huyu ni kipa bora kwenye mfumo huu wa kisasa, lakini tofauti yake na Ederson ni kwamba hapendi sana kuingia kwenye mashaka na mara nyingi mipira yake amekuwa akiitupa mbele.

Thibaut Courtois, Real Madrid

Courtois ni zaidi ya mfumo huu kumuona akiwa amevuka mstari wa katikati siyo jambo la ajabu kwake. Amekuwa akitoa pasi kwa kutumia viungo vyote kichwa, miguu na hata kifua chake kimekuwa na ubora wa juu kufikisha mpira kwa mlengwa, labda ndiye namba moja hapa.

Moja ya makipa wa kisasa kwa sasa duniani, ana ufundi mwingi mguu kwake na hilo lilimfanya kocha wa Arsenal Mikel Arteta aachane na Aaron Ramsadale na kumchukua huyo kutokana na uwezo wake wa juu wa kutumia miguu kwa kuwa mfumo wa timu yake wa mabeki wa kati kupitia kwa Gabriel Magalhães na William Saliba wanauwezo mkubwa wa kutumia mfuno.

Related Posts