MFUNGAJI wa bao pekee lililoitubulia Yanga katika Ligi Kuu, Gibril Sillah amefunguka namna bao hilo lilivyompa heshima, lakini akizidi kumfukuzia Stephane Aziz Ki katika mechi za Dabi ya Dar es Salaam.
Mashabiki wa Yanga wamekosa raha baada ya Sillah kuitungua timu yao kwenye Uwanja wa Azam Complex, kwani lilivunja rekodi kibao ilizokuwa nazo, lakini hilo lilikuwa bao la tatu kwa staa huyo wa Azam kuitungua Yanga akimtafuta Aziz KI mwenye kismati ya kuitungua pia Azam kila zinapokutana.
Sillah aliifungia Azam bao hilo la tatu kwake tangu asajiliwe na timu hiyo na yote akiyafunga kipindi cha kwanza.
Ndani ya mabao matatu hayo Sillah amelifunga mabao mawili katika dakika moja kwenye mechi mbili tofauti zilizofuatana.
Sillah aliifungia Azam bao la kwanza dhidi ya Yanga Oktoba 23,2023, akiisawazishia dakika ya 18 kwa asisti ya beki Lusajo Mwaikenda japo mechi iliisha kwa Azam kulala 3-3,Aziz KI akifunga hat trick.
Winga huyo Mgambia bao la pili akiifunga Yanga ilipolala 2-1 Machi 17,2024, akisawazisha pia dakika ya 18 bao la Clement Mzize na juzi tena akafunga la taty kwa shuti kali dakika ya 33 akipokea asisti ya kiungo wake Adolf Mtasingwa na kuizamisha Yanga.
Mbali na kufunga Sillah pia ameshatoa Asisti mbili akitengeneza mabao kwenye mechi dhidi ya Yanga Mgambia huyo akiwa na moto anapokutana na mabingwa hao.
Hata hivyo, Sillah ni kama anaifukuza rekodi ya kiungo wa Yanga Aziz KI anayeongoza kwa kuifunga Azam jumla ya mabao sita katika mashindano tofauti akiwa ndiye staa aliyewafunga zaidi matajiri hao wa Chamazi.
Akizungumza bao hilo la juzi, Sillah alisema limeipa heshima timu hiyo kwa kuitibulia Yanga iliyokuwa haijafungwa wala kuruhusu nyavu zao kuguswa katika ligi msimu huu.
“Mechi ilikuwa na presha kubwa, kutokana na mashabiki kubeba matarajio makubwa, ila yote katika yote sisi tumemaliza dakika 90 kwa kutimiza malengo yetu ambayo ilikuwa ni kupata pointi tatu, kwa sasa tunaangalia mechi zilizopo mbele yatu,” alisema Sillah na kuongeza;
“Msimu huu natamani uwe wa mafanikio makubwa zaidi kwetu, najua ligi ni ngumu , ila tutaendelea na mapambano hadi dakika ya mwisho za kutimiza malengo ya klabu. Binafsi natamani kufunga zaidi ya mabao niliyokuwa nayo msimu uliopita, kama itashindikana basi nihusike katika pasi za mwisho nyingi, kwani timu kwanza malengo binafsi baadaye.”