KOCHA wa Akademi ya AZOS ya nchini Sweden, Salim Soud amesema ingawa anafundisha nchi hiyo hayo, malengo yake ya baadaye ni kuzisaidia timu za Tanzania.
Kocha huyo ni msimu wa pili sasa tangu aanze kufundisha Sweden ikiwa ni akademi yake mwenyewe kaianzisha.
Akizungumza na safu ya Nje ya Bongo ya Mwanaspoti, Soud alisema akademi hiyo lengo lake kubwa ni kufanyisha mazoezi binafsi wachezaji na kufundisha makocha wa timu za watoto.
Mtanzania huyo alisema program hiyo wanatoa kwa wachezaji kutoka mataifa mbalimbali ikiwa kwa wanaume na wanawake na anatamani kuileta Tanzania kutokana na maendeleo ya soka hilo.
“Bado naendelea kusoma, naamini mchakato utakavyokwenda haraka naweza mwakani kuja kusaidia nchi yangu, hivyo natakiwa kujifunza vingi, isitoshe Tanzania sasa imeendelea sana,” alisema Soud.
Kocha huyo ana leseni D ya UEFA na yuko kwenye mchakato wa kufanya UEFA C mwaka huu.