Chad yafanya uchaguzi wa rais kuhitimisha utawala wa kijeshi – DW – 06.05.2024

Uchaguzi huo ulipangwa kwa dhamira ya kuhitimisha miaka mitatu ya utawala wa mpito wa kijeshi chini Mahamat Idriss Deby. 

Alichukua madaraka mwezi Aprili mwaka 2021 baada ya waasi kumuua baba yake Idriss Deby, aliyekuwa kiongozi wa muda mrefu wa Chad.

Hata hivyo kura ya leo yumkini itaimarisha zaidi nafasi ya Mahamat kama mtawala wa taifa hilo na kuzima ndoto ya kufunguliwa milango ya demokrasia.

Kiongozi huyo anatarajiwa kupata ushindi ingawa mpinzani wake mkuu Succes Masra amekuwa akivutia wingi wa wafuasi kwenye mikutano ya kampeni kuliko ilivyotarajiwa.

Vituo vitafunguliwa mnamo saa moja asubuhi na kufungwa saa kumi na moja jioni. Raia milioni 8.5 wana haki ya kupiga kura kwenye uchaguzi huo wa leo.

Wanajeshi tayari walianza kupiga kura mapema siku ya Jumapili. Matokea ya awali yanatarajiwa kutangazwa Mei 21 na matokeo kamili yatatolewa Juni 5.

Iwapo hakuna mgombea atakayepata zaidi ya asilimia 50 ya kura, kutakuwa na duru ya pili ya uchaguzi mnamo Juni, 22.

Deby aahidi usalama wakati Marekani ikiondoa kwa muda wanajeshi wake 

Kiongozi wa mpito wa Chad, Mahamat Idriss Deby.
Kiongozi wa mpito wa Chad, Mahamat Idriss Deby.Picha: Gilles Chris Namia Rimbarne/REUTERS

Tangu alipomrithi baba yake kama kiongozi kwenye taifa hilo la Afrika ya Kati linalochimba mafuta, Deby ameendeleza uhusiano mzuri na Ufaransa ambayo ni mkoloni wa zamani wa Chad na mshirika wa muda mrefu. 

Wakati tawala nyingine za kijeshi kwenye kanda ya Sahel ikiwemo Mali, Burkina na Niger zimeitaka Ufaransa na mataifa mengine ya magharibi kuondoa vikosi vyao kwenye mataifa yao, Chad imesalia taifa pekee la Sahel lenye idadi kubwa ya wanajeshi wa Ufaransa.

Uchaguzi huo unafanyika sambamba na hatua ya Marekani kuondoa vikosi vyake nchini Chad. Taifa hilo la Sahel ndiyo mshirika wa karibu zaidi wa Marekani kwenye kanda nzima ya magharibi na katikati mwa Afrika.

Hata hivyo Marekani ilitangaza kuondoa kwa muda wanajeshi wake mwezi uliopita ikisema itafanya tathmini ya operesheni zake za usalama kwenye taifa hilo baada ya uchaguzi.

Kwenye kampeni yake, Deby ameahidi kuimarisha usalama, utawala wa sheria na kuongeza uzalishaji wa nishati ya umeme.

Mashaka ya baadhi upande wa upinzani yaleta wasiwasi wa kuzuka machafuko 

Uchaguzi wa leo unampambanisha Deby dhidi ya waziri mkuu wake Succes Masra, ambaye kabla alikuwa mpinzani wake wa kisiasa aliyeikimbia nchi hiyo mwaka 2022 lakini akaruhusiwa kurejea mwaka mmoja baadaye.

Mitaa ya mji mkuu wa Chad, N´Djamena.
Mitaa ya mji mkuu wa Chad, N´Djamena.Picha: Denis Sassou Gueipeur/AFP

Mwengine anayewania ni waziri mkuu wa zamani Albert Pahimi Padacke na wagombea wengine saba.

Yaya Dillo, mwanasiasa wa upinzani ambaye alitarajiwa kugombea dhidi ya Deby licha ya kuwa anatoka ukoo mmoja na kiongozi huyo, alipigwa risasi na kuuwa mnamo Februari 28 kwenye mji mkuu wa Chad, N´Djamena. Mauaji yake yalitokea siku moja baada ya tarehe ya uchaguzi kutangazwa.

Padacke amemtuhumu Masra kushirikiana na Deby lakini Masra amekuwa akivutia umati mkubwa kwenye mikutano yake ya kampeni.

Baadhi ya wafuasi wa upinzani na makundi ya kiraia yametoa mwito wa kususiwa uchaguzi wa lreo wakitoa sababu ya wasiwasi wa kutoea wizi wa kura. Mwito huo umepandisha joto la kisiasa na mashaka ya kutokea machafuko.

Related Posts