STRAIKA wa Fleetwoods United FC inayoshiriki Ligi ya Daraja la Pili UAE, Mgaya Ally amesema anarejea Tanzania wiki hii kusikilizia ofa kutoka nchi tatu.
Kinda huyo kabla ya kujiunga na timu hiyo msimu 2021/22 aliichezea Coastal Union ya vijana U-20 msimu mmoja 2020/21.
Nyota huyo alisaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia klabu hiyo ambao unatamatika katika dirisha dogo.
Nje ya Bongo ilimtafuta mshambuliaji huyo kuhusu hatma yake kikosini na alisema kuwa bado klabu hiyo haijaanza mazungumzo naye ya kusaini mkataba mpya na wakati wa dirisha dogo atarejea Tanzania kusikilizia ofa kutoka timu nyingine.
“Kwa sasa naweza kusema niko huru sina timu, klabu yangu haijafanya vizuri na hata hatujaanza mazungumzo lakini nimepata ofa kutoka Oman, Kazakhstan na Jordan ambazo inabidi nitulize akili kuangalia wapi panafaa,” alisema Mgaya.