Madeni ya makandarasi, wazabuni yawasha moto tena bungeni

Dodoma. Wabunge wameibana Serikali kuhusu madeni ya muda mrefu ya makandarasi na wazabuni wa chakula shuleni, huku yenyewe ikisema ulipaji wa madeni hayo unategemea upatikanaji wa mapato na kukamilika kwa uhakiki.

Wabunge walioibua hoja hiyo bungeni leo Jumatatu, Novemba 4, 2024 ni Priscus Tarimo (Moshi Mjini-CCM), Asia Halamga (Viti Maalumu-CCM), Grace Tendegu (Viti Maalumu), Cecilia Pareso (Viti Maalumu) na Neema Lugangira (Viti Maalumu-CCM).

Katika swali lake la msingi, Tarimo amehoji ni lini mpango wa kuwalipa wazabuni wanaotoa huduma mbalimbali, hususani chakula kwenye shule za Serikali ambao wanadai kwa muda mrefu.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande, amesema Serikali inaendelea na utaratibu wa ulipaji wa madeni mbalimbali, ikiwemo ya wazabuni wa chakula waliotoa huduma katika shule mbalimbali.

“Ulipaji huzingatia upatikanaji wa mapato na uhakiki wa madeni unaofanywa na Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali (IAG),” amesema.

Amesema lengo la Serikali kufanya uhakiki ni kutekeleza azma ya usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma kulingana na sheria ya Bajeti SURA 439 na sheria ya fedha za umma SURA 348.

Amesema Wizara ya Fedha inazielekeza halmashauri zote nchini kulipia huduma mbalimbali wanazopokea kutoka kwa watoa huduma kwa wakati, ili kuepuka ulimbikizaji wa madeni na kuondoa usumbufu usio wa lazima kwa watoa huduma. 

Katika swali la nyongeza, Asia amesema katika kipindi cha bajeti ya mwaka 2024/25, Waziri (hakumtaja) alisema zimetolewa Sh949 bilioni kwa ajili ya ulipaji wa madeni mbalimbali na kuhoji iwapo watoa huduma shuleni kama wapo kwenye fedha hizo.

“Nataka kufahamu wanatakiwa kulipa kwa muda gani ili wananchi hawa wafahamu watakaa muda gani kwa sababu watoa huduma shuleni wengi ni wajasiriamali wadogo wadogo,” amesema.

Akijibu swali la nyongeza, Chande amesema watoa huduma shuleni walikuwa ni sehemu ya fedha hizo zilizotengwa mwaka jana na kuwa zinaendelea kulipwa hadi mwaka ujao.

“Kuhusu ni lini tutalipa, inategemea upatikanaji wa mapato na kukamilika kwa uhakiki. Nimuombe mheshimiwa mbunge na wazabuni wawe na subira muda ukifika fedha zao zitalipwa,” amesema Chande.

Naye Pareso amesema miongoni mwa watu wanaodai Serikali kwa muda mrefu ni pamoja na makandarasi wa barabara hapa nchini na kuwa wapo wengi wana madai ya muda mrefu.

“Na ukumbuke watu wanaochukua kazi hizi wengi wanakwenda kukopa benki na wanatakiwa kufanya marejesho, Serikali haijawalipa. Nini kauli ya Serikali kwa makandarasi wanaodai na wapo wengine wamefilisiwa kwa sababu walikwenda kukopa,” amehoji.

Akijibu swali hilo, Chande amesema kauli ya Serikali ni kuwa madeni yote yanaendelea kuhakikiwa, uhakiki utakapokamilika na mapato yakipatikana watalipwa wazabuni wote pamoja na makandarasi.

Naye Tendega amesema wakati Chande anajibu maswali ya wabunge waliotangulia alisema wanafanya uhakiki ndipo walipe madeni hayo, lakini kuna wazabuni na makandarasi wanadai madeni ya miaka mitatu.

Amehoji uhakiki huo unachukua muda gani ili walipwe fedha zao.

Akijibu swali hilo, Chande amesema mbunge huyo amechukua eneo moja alilolizungumzia kuhusu ulipaji wa madeni hayo na kuacha eneo la kulingana na upatikanaji wa mapato.

“Kwa hiyo mapato yakipatikana watalipwa, dawa ya deni ni kulipa. Nawahakikishia waheshimiwa wabunge fedha zikipatikana wote watalipwa,” amesema.

Naye Lugangira amesema changamoto ya madeni ya wazabuni wa chakula shuleni inaathiri upatikanaji chakula na ubora wa chakula hicho, hivyo kuathiri pia uwezo wa kusoma kwa watoto.

Amesema Agosti 2024, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Zainabu Katimba amesema bungeni wamewasilisha Wizara ya Fedha madeni ya wazabuni wa chakula shuleni ya Sh21.7 bilioni.

“Je uhakiki huo utakamilika lini na kwa mfano jimbo la Bukoba Mjini kuna shule sita za sekondari ambazo ni za Serikali zinadai Sh936 milioni na madeni hayo ni kati ya mwaka hadi miaka sita,” amesema.

Ameomba waziri kuwapa majibu ya uhakika na ya kueleweka.

Akijibu swali hilo, Chande amesema ni kweli baadhi ya wazabuni malipo yao hayajakamilika na kuwafikia, lakini kadri mapato yatakavyokuwa yanapatikana ndivyo watakavyolipwa wazabuni wetu.

Bajeti ya kuyalipa iwekwe wazi

Suala la madeni lilizungumziwa pia Novemba mosi, 2024 na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, kuhusu mapendekezo wa maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2025/26 pamoja mapendekezo ya mwongozo wa maandalizi mpango na bajeti ya Serikali kwa mwaka 2025/26.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Oran Njeza alisema uchambuzi wa kamati yake umebaini madeni hadi Juni, 2023 jumla ya madeni yaliyohakikiwa yalikuwa ni Sh3.30 trilioni na kiasi cha madeni ambayo hayajahakikiwa ni Sh64.72 bilioni.

Alisema sekta ya barabara, maji, kilimo na mifugo imekuwa vigumu kutekeleza miradi mipya kwa sababu ya madeni hayo.

Alisema mwaka 2023 Serikali kupitia Katibu Mkuu Hazina ilitoa waraka ujulikanao kama The Treasury Circular No. 2 of 2022/23 on Government Domestic Expenditure Arrears and Other Outstanding Obligations kwa lengo la kuendelea kusimamia na kutekeleza mkakati wa kudhibiti na kuzuia malimbikizo ya madeni.

Hata hivyo, alisema kamati imebaini kwamba waraka huo haujaweza kudhibiti malimbikizo ya madeni.

“Kati ya maeneo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa na Maafisa masuuli wakati wa upangaji wa bajeti ni pamoja kutenga bajeti ya ulipaji wa madeni kwa kuzingatia umri wa madeni na kutoa kipaumbele kwenye madeni yenye riba na adhabu,”alisema.

Alitaka mwongozo wa bajeti kuweka wazi kiasi ambacho kitatengwa na Serikali kwa ajili ya ulipaji wa madeni ya wakandarasi na wazabuni wa ndani.

Related Posts