DKT.MPANGO KUFUNGUA MICHEZO YA SHIMMUTA 2024 JIJINI TANGA

NA ANDREW CHALE.

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango anatarajia kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Mashindano ya Mashirika ya Umma, Makampuni na Taasisi Binafsi (SHIMMUTA) Novemba 16, 2024 jijini Tanga.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Shirikisho hilo, Dkt.Maswet Masinda wakati wa zoezi la kupanga droo ya makundi ya timu zitakazokutana katika michezo zaidi ya 12 ambayo itashindaniwa na timu zaidi ya 91 zilizojitokeza mwaka huu.

“Maandalizi yote yamekamilika na tayari mlezi wetu ambaye ni Makamu wa Rais Dkt. Mpango anatarajiwa kufungua rasmi Novemba 16, 2024. Uwanja wa ufunguzi tutautangaza rasmi hapo baadae.

Kwa sasa timu zote zipo hapa kushuhudia droo ya wazi kabisa kuona timu zao zitakuwa kwenye kundi lipi tayari kwa michezo rasmi itakayoanza Novemba 10 hadi 24, Jijini Tanga.”Amesema Dkt. Masinda

Aidha, Dkt. Masinda ametoa wito kwa timu zote 91 kufika Jijini Tanga Novemba 8, ambapo Novemba 9 watakuwa na kikao cha pamoja kisha michezo kuanza kutimua vumbi Novemba 10.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa SHIMMUTA Taifa, Roselyne Massam amesema mwaka huu Shirikisho hilo limevunja rekodi kwa kupata timu nyingi zilizojitokeza hali ambayo inaleta mwamko na hamasa katika kuimarisha afya kwenye michezo pamoja na kuleta umoja hapa nchini kupitia michezo hiyo.

Amesema rekodi hiyo inatokana na kuongezeka kwa idadi ya timu na sasa kufiki 91 zitakazochuana katika kuwasaka mabingwa kupitia michezo watakayoshindaniwa.

Aidha, katika zoezi hilo wamejipanga hakuna mamluki atakayechezeshwa kwenye timu zitakazoshiriki mashindano hayo kwani watahakikisha wanasimamia sheria, kanuni na taratibu zinazowaongoza katika michezo yote.

Michezo hiyo 12 itakayochezwa katika mashindano hayo ni pamoja na michezo ya mpira wa miguu kwa wanaume, mpira wa pete, wavu, kikapu, dats, pool table, vishale, drafti, kukimbia kwa magunia, riadha, kuvuta kamba, bao na mingineyo, lengo kuu likiwa kuimarisha uhusiano na kuimarisha afya za wafanyakazi kupitia michezo.



Related Posts