SERIKALI KULIPA MADENI BAADA YA UHAKIKI NA UPATIKANAJI WA FEDHA

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), alipokuwa akijibu swali bungeni jijini Dodoma la Mbunge wa Moshi Mjini, Mhe. Priscus Jacob Tarimo (Mb), aliyetaka kujua mpango wa kuwalipa Wazabuni wanaotoa huduma mbalimbali hususani chakula kwenye Shule za Serikali ambao wanadai muda mrefu. 

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) (kushoto), wakiteta jambo bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo (Mb), Katikati ni Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa (Mb).(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha-Dodoma)

Na. Asia Singano na Peter Haule, WF, Dodoma.

Serikali imesema kuwa inaendelea na utaratibu wa ulipaji wa madeni mbalimbali ikiwemo madeni ya wazabuni wa chakula waliotoa huduma katika shule mbalimbali kwa kuzingatia upatikanaji wa mapato baada ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali (IAG) kufanya uhakiki wa madeni husika.

Hayo yameelezwa bungeni, jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Moshi Mjini Mhe. Priscus Jacob Tarimo (Mb), aliyetaka kujua mpango wa kuwalipa Wazabuni wanaotoa huduma mbalimbali hususani chakula kwenye Shule za Serikali ambao wanadai kwa muda mrefu. 

Mhe. Chande alisema kuwa lengo la Serikali kufanya uhakiki ni kutekeleza azma ya usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma kulingana na sheria ya Bajeti SURA 439 na Sheria ya Fedha za umma SURA 348.

‘‘Wizara ya Fedha inazielekeza Halmashauri zote nchini kulipia huduma mbalimbali wanazopokea kutoka kwa watoa huduma kwa wakati ili kuepuka ulimbikizaji wa madeni na kuondoa usumbufu usio wa lazima kwa watoa huduma,’’alifafanua Mhe. Chande.

Kwa upande mwingine akijibu swali la Mbunge wa Chonga, Mhe. Salum Mohammed Shaafi, aliyetaka kujua iwapo Akaunti ya Pamoja ya Muungano imeshafunguliwa, Mhe. Chande alisema kuwa Serikali mbili zinaendelea na mashauriano juu ya mapendekezo yaliyowasilishwa na Tume ya Pamoja ya Fedha kuhusu utaratibu wa kudumu wa Kuchangia Matumizi na Kugawana Mapato ya Muungano.

Aliongeza kuwa uamuzi wa pamoja utakapofikiwa na pande mbili za Muungano, ndiyo utakaowezesha kufunguliwa kwa Akaunti ya Fedha ya Pamoja.

Related Posts