Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu Baraka Mukama, kulipa faini ya Sh700,000 au kwenda jela miezi sita, baada ya kupatikana na hatia ya kufanya kazi ya uwakili bila kuwa na sifa.
Uamuzi huo umetolewa leo Jumatatu, Novemba 4, 2024 na Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo baada ya kumtia hatiani katika shtaka moja la kufanya kazi ya uwakili bila kuwa na sifa.
Mpaka sasa (ilikuwa saa 8 mchana) mshtakiwa huyo, bado hajalipa faini hiyo na atapelekwa gerezani kwenda kutumikia adhabu hiyo.
Mukama, alikuwa anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kufanya kazi ya uwakili bila kuwa na sifa na kuzuia watumishi wa umma kufanya kazi yao.
Akisoma uamuzi, Hakimu Swallo amesema mshtakiwa ametiwa hatiani katika shtaka moja la kufanya kazi ya uwakili bila kuwa na sifa.
Amesema upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi watano na vielelezo kadhaa ambavyo walitoa ushahidi wao mahakamani hapo kuthibitisha mashtaka dhidi ya mshtakiwa huyo.
Mshtakiwa kwa upande wake alikuwa na mashahidi watatu waliomtetea dhidi ya mashtaka yanayomkabili.
“Mahakama imepitia ushahidi wa upande wa mashtaka na kumtia hatiani katika shtaka moja la kufanya kazi ya uwakili bila kuwa na sifa, hivyo imempiga faini ya Sh 700,000 au kutumikia kifungo cha miezi sita gerezani iwapo atashindwa kulipa faini hiyo,” amesema Hakimu Swallo.
Amesema katika shtaka la kuzuia mtumishi wa umma kufanya kazi zake, upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha shtaka hilo kutokana na kifungu walichotumia kumshtakiwa Mukama kutokuwa sahihi, hivyo Mahakama imeshindwa kumtia hatiani katika shtaka hilo.
Awali, wakili wa Serikali, Asiat Mzamiru aliomba Mahakama itoa adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyo kwa mujibu wa sheria.
Alipopewa nafasi ya kujitetea kwanini asipewe adhabu kali, mshtakiwa huyo aliiomba Mahakama impunguzie adhabu kwa sababu ana familia inayomtegemea.
Hata hivyo, Hakimu Swallo alitupilia mbali ombi hilo na kumhukumu adhabu hiyo.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, shtaka la kwanza, alidaiwa kwa makusudi alimzuia askari polisi mwenye namba J 515 PC Mubaraka Abdallah, asimkamate Harid Rajabu maarufu Somole, aliyefutuwa kesi ya jinai namba 99/2019.
Shtaka la pili ni kufanya kazi ya uwakili bila kuwa na sifa, tukio analodaiwa kulitenda Mei 23, 2023 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Inadaiwa siku hiyo, akiwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Romuli Mbuya alijitambulisha kama wakili wa kijitegemea mwenye namba ya usajili 4696, wakati akijua ni uongo na yeye sio wakili.
Mshtakiwa huyo alijitambulisha kama wakili katika kesi ya jinai namba 99/2019 aliyokuwa akiwatetea washtakiwa wawili kati ya wanne waliokuwa wanakabiliwa na mashtaka ya kughushi nyaraka na stika mbalimbali za dawa.
Kwa mara ya kwanza, mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo Oktoba 2, 2023 na kusomewa mashtaka katika kesi ya jinai namba 177/2023.