LIGI Kuu Bara inaendelea tena leo Jumatatu kwa timu nane kusaka pointi tatu na michezo minne itapigwa viwanja mbalimbali.
Mchezo wa mapema saa 8:00 mchana utazikutanisha Ihefu iliyokuwa nafasi ya 12 na pointi 25 kwenye Uwanja wa Liti, Singida dhidi ya Namungo ya Lindi iliyopo nafasi ya 11 na pointi 27 baada ya zote kucheza michezo 24.
Mchezo huu ni wa kuwania nafasi kutokana na jinsi timu hizo zilivyopishana pointi ingawa pia itakuwa ni mechi ya kisasi kwa Ihefu kwani ilichapwa mabao 2-0 mzunguko wa kwanza Uwanja wa Majaliwa Novemba 23, mwaka jana.
Hata hivyo rekodi zinaikataa zaidi Ihefu kwani tangu ilipoanza kukutana na Namungo Ligi Kuu Bara zimeshakutana mara tano na kati ya hizo haijawahi kushinda kwa sababu imefungwa michezo mitatu huku miwili iliyobaki ikiisha kwa sare.
Kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro utapigwa mchezo mwingine na Mtibwa Sugar inayopigania janga la kutoshuka daraja itakuwa na kibarua dhidi ya matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam kuanzia saa 10:00 jioni.
Mtibwa ipo mkiani na pointi 17 wakati Azam ni ya pili na pointi 54 baada ya zote kucheza michezo 24.
Ushindi pekee kwa Mtibwa utaweka hai matumaini ya kusalia Ligi Kuu ingawa ikitokea ikapoteza itakuwa na mlima mrefu zaidi huku ikiingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kuchapwa 5-0, mzunguko wa kwanza Novemba 24, mwaka jana.
Mchezo wa mwisho kwa timu hizi kukutana mkoani Morogoro uliopigwa Uwanja wa Manungu Complex, Mtibwa ilifungwa pia mabao 4-3, Novemba 12, 2022.
Saa 12:15 jioni utapigwa mchezo mwingine na Simba iliyopo nafasi ya tatu na pointi zake 50 baada ya kucheza michezo 23 itakuwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi dhidi ya Tabora United inayoshika nafasi ya 15 na pointi 23.
Tabora United iliyokuwa chini ya kocha wa zamani wa Simba, Masoud Djuma inapigania kubaki Ligi Kuu kutokana na kutokuwa na mwenendo mzuri kwani katika michezo 24 iliyocheza imeshinda minne tu, sare 11 na kuchezea vichapo mara tisa.
Huu utakuwa ni mchezo wa pili Ligi Kuu timu hizi kukutana kwani mara ya kwanza zilikutana mzunguko wa kwanza na Simba ilishinda mabao 4-0, kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora, Februari 6, mwaka huu.
Katika rekodi bora ambayo Simba imeiweka msimu huu licha ya kutofanya vizuri ni mwendelezo wa matokeo mazuri pindi inapocheza ugenini tofauti na ilivyokuwa kwa wapinzani wao Azam FC na vinara wa ligi Yanga tangu msimu umeanza.
Rekodi zinaonyesha Simba katika michezo 12 ugenini imeshinda minane, sare mitatu na kupoteza mmoja na kati ya hiyo imefunga jumla ya mabao 24 na kuruhusu 12, sawa na kukusanya pointi 27.
Yanga pia imecheza michezo 12 ugenini ukiachilia mbali wa jana dhidi ya Mashujaa ambao ni wa 13, na imeshinda minane, sare miwili na kupoteza miwili ikifunga mabao 23 na kuruhusu saba ikikusanya pointi 26.
Azam iliyopo nafasi ya tatu imecheza michezo 11 ugenini na wa leo dhidi ya Mtibwa Sugar utakuwa ni wa 12 na kati ya hiyo imeshinda sita, sare minne na kupoteza mmoja ikifunga mabao 18 na kuruhusu sita sawa na kukusanya pointi zake 22.
Mchezo wa mwisho wa kukamilisha siku ya leo utapigwa huko Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga na wenyeji ‘Wagosi wa Kaya’ Coastal Union iloiyo nafasi ya nne na pointi 33 itacheza na Tanzania Prisons saa 2:30 usiku. Pointi hizo ni sawa na ilizokuwa nazo KMC zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa huku Prisons ikiwa ya sita na pointi 31.
Timu hizi zinakutana wakati Prisons ikiwa na kumbukumbu ya kuchapwa mechi ya mzunguko wa kwanza bao 1-0, kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya Novemba 23, mwaka jana huku pia haijashinda katika michezo mitano mfululizo ya Ligi Kuu Bara.
Kocha wa Simba, Juma Mgunda alisema bado wana nafasi nzuri ya kufanya vizuri zaidi katika michezo iliyobaki huku Kocha wa Tabora United, Masoud Djuma akiwataka wachezaji wa timu hiyo kucheza kwa nidhamu ili wapate matokeo yaliyokuwa bora.
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zubery Katwila alisema mchezo na Azam utakuwa mgumu kutokana na ubora wa wapinzani wao ingawa kwa nafasi waliyopo michezo sita iliyobaki watapambana kadri ya uwezo wao ili kuinusuru timu hiyo.