Mohamed kortini kwa madai ya kughushi wosia wa mama yake

Dar es Salaam. Mkazi wa Kawe Mzimuni, Mohamed Omar (64) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu mashitaka mawili ya jinai likiwamo la kughushi wosia wa mama yake.

Mshitakiwa huyo amefikishwa mahakamani hapo, leo Jumatatu Novemba 4, 2024 na kusomewa mashitaka na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Neema Moshi, mbele ya Hakimu Mfawidhi, Franco Kiswaga.

Hata hivyo, mshitakiwa wa pili katika kesi hiyo, Nargis Omar (70) ambaye ni dada yake Mohamed, hakuwepo mahakamani hapo, baada ya kuruka dhamana ya polisi.

Wakili Neema amedai kutokana na mshitakiwa Nargis kuruka dhamana akiwa polisi, upande wa mashtaka utamsomea siku atakapokamatwa na kufikishwa mahakamani hapo.

Baada ya kueleza hayo, wakili Neema alimsomea mashitaka Mohamed, ambaye anatetewa na wakili Steven Mosha.

Alidai katika shitaka  la kwanza, washitakiwa kwa pamoja wanadaiwa kughushi wosia, tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya Julai 29, 1997 na Oktoba 28, 1998 katika Jiji la Dar es Salaam.

Wakili Moshi alidai washitakiwa wanadaiwa katika kipindi hicho, kwa lengo la kudanganya walighushi wosia uliandikwa na marehemu Rukia Ahmed Omar, maarufu  Rukia Sheikh Ali, wakati wakijua kuwa ni uongo.

Shtaka la pili ni kuwasilisha nyaraka ya uongo mahakamani, tukio wanalodaiwa kulitenda katika ya tarehe hizo katika Jiji la Dar es Salaam.

Inadaiwa siku hiyo ya tukio, Omar na dada yake ambaye hajafikishwa mahakamani hapo, huku wakijua wanadanganya, waliwasilisha wosia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakionyesha marehemu mama yao, Rukia Ahmed Omar alitoa nyumba moja kwa Nargis iliyopo kiwanja namba 35, eneo la Kariakoo na pia alitoa nyumba kwa Mohamed iliyopo kiwanja namba 60 kitalu M, eneo la Magomeni, wakati wakijua kuwa ni uongo.

Mshitakiwa baada ya kusomewa mashitaka yake alikana na upande wa mashitaka umedai upelelezi bado unaendelea.

Wakili Moshi alidai mashitaka yanayomkabili mshitakiwa yanadhaminika ila Mahakama itoe masharti magumu yatakayomfanya mshitakiwa afike mahakamani na pia awasilishe hati ya kusafiria mahakamani hapo.

Hakimu Kiswaga alitoa masharti matatu ya dhamana dhidi ya Mohamed.

Amesema mshitakiwa huyo anatakiwa awe na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh 5 milioni kila mmoja.

Pia, wadhamini hao wanatakiwa kuwa na barua za utambulisho, kama ni wafanyakazi wanatakiwa wawe na barua ya mwajiri na kama hawana kazi basi wawe na barua kutoka Serikali za Mitaa.

Sharti ya tatu, mshtakiwa anatakiwa asitoke nje ya nchi bila ruhusa ya Mahakama.

Mshitakiwa amefanikiwa kupata dhamana na kesi yake imeahirishwa hadi Desemba 4, 2024 kwa ajili ya kutajwa.

Related Posts