Mifumo 17 yaunganishwa taasisi za Serikali kuwezesha ununuzi kielektroniki Tanzania

Dar es Salaam. Taasisi zaidi ya 17 za Serikali nchini Tanzania zimeunganishwa na mfumo mpya wa manunuzi wa kielekroniki (NeST) ili kuongeza ufanisi, uwazi na kurahisisha manunuzi ya umma.

Kuunganishwa na kuzifanya taasisi hizo zisomane, pia kumetajwa kutapunguza mianya ya utoaji rushwa kwa kuondoa muingiliano wa watu katika ushughulikiaji wa zabuni mbalimbali za manunuzi.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu Novemba 4, 2024 jijini Dar es Salaam katika mkutano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) na waandishi na wahariri wa vyombo vya habari ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Akizungumza katika mkutano huo, Meneja wa PPRA Kanda ya Pwani, Vicky Mollel amesema kuunganishwa kwa mifumo hiyo kunasaidia kurahisisha kupunguza muda ambao wazabuni wangetumia katika utumaji wa maombi pindi wanapohitaji kuambatanisha baadhi ya vielelezo.

“Kuunganishwa kwa mifumo mingine zaidi ya 17 ni kwa ajili ya kuwezesha suala la ununuzi kufanyika kwa ufanisi na wakati, hii pia inasaidia taarifa zinazotumiwa kuwa sahihi ndani ya mfumo ambazo haziwezi kubadilika,” amesema.

Kwa mujibu wa Mollel, hilo pia litasaidia kuondoa mkanganyiko wa taarifa ambao kabla ya kuwapo kwa mfumo huo ungefanyika kwa mtu kuwa na uwezo wa kubadili taarifa zake kulingana na aina ya zabuni anayoomba.

“Mbali na kutuma maombi pia wazabuni wataweza kufanya ufuatiliaji wa zabuni kujua iko hatua gani baada ya kutangazwa au tathmini,” amesema Mollel.

Kuhusu rushwa, amesema matumizi ya mifumo huo pia umesaidia kupunguza mianya hiyo kwa kuondoa muingiliano kati ya mtangaza zabuni na anayeomba, kwani kila kitu kinafanyika kwa njia ya mtandao.

Ametaja baadhi ya mifumo ambayo imeunganishwa na NeST ni Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), mfumo wa kidijitali (Tausi), Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfumo wa Malipo ya Serikali (GePG), Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (Osha), Bodi ya Usajili wa Wahandisi nchini (ERB), Bodi ya Usajili wa Makandarasi Tanzania (CRB).

Wengine waliounishwa ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira), Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na Mfumo Shirikishi wa Kusimamia Shughuli na Rasilimali za Taasisi (ERMS).

Mfumo huo umetengenezwa ili kuongeza uwazi kwenye ununuzi wa umma, uwepo wa vitendo vya rushwa kwenye ununuzi wa umma, michakato ya zabuni kuchukua muda mrefu na kuhakikisha masharti ya mikataba yanazingatiwa kikamilifu.

Pia mabadiliko hayo yamelenga kushughulikia suala la ubora usioridhisha wa bidhaa, huduma na kazi za ujenzi, gharama kubwa katika kununua bidhaa na huduma mbalimbali ukilinganisha na bei za soko, uchaguzi mbovu wa njia za ununuzi na matumizi yasiyoridhisha ya sheria na taratibu za ununuzi umma.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Denis Simba amesema kupitia matumizi ya mfumo huo wamefanikia kuokoa jumla ya Sh14.94 bilioni kupitia ukaguzi na Sh2.7 trilioni kupitia ufuatiliaji tangu mfumo uanze kutumika Julai mosi 2023 hadi Oktoba 2024.

“Si hilo tu, hadi kufikia Oktoba 31, 2024, jumla ya taasisi nunuzi 21,851 zilikuwa zimesajiliwa na zinatumia mfumo wa NeST, wazabuni zaidi ya 28,590 wamejisajili na mikataba ya zabuni 62,267 yenye thamani ya zaidi ya Sh10.2 trilioni zikiwa zimetolewa kwa wazabuni kupitia mfumo huu,” amesema Simba.

Katika zabuni zilizotolewa hadi mwisho wa mwaka wa fedha 2023/24 kwa mujibu wake, asilimia 99.6 zilikwenda kwa Watanzania zikifuatiwa na China iliyochukua zabuni 28 na nchi ya Kenya zabuni 21, Afrika Kusini 18, nchi za Umoja wa Jumuiya za Kiarabu zabuni 10.

Amesema katika kuwaongezea nguvu wazawa, sheria mpya ya ununuzi wa umma imeweka fursa ya wazabuni wa ndani kuingia ubia na wazabuni wa nje na katika ushiriki huo, kampuni ya ndani ndiyo itakayokuwa kiongozi na itapokea malipo.

“Pia zabuni zenye thamani isiyozidi Sh50 bilioni zimetengwa kwa ajili ya wazabuni wa ndani ya nchi pekee. Mfumo wa NeST unaisaidia PPRA katika kulisimamia hilo kwa ufanisi zaidi,” amesema Simba.

Related Posts