Safari ya mwisho ya Jenerali Musuguri ilivyokuwa Butiama

Butiama. David Musuguri (104), aliyekuwa mkuu wa majeshi ya ulinzi amehitimisha safari ya maisha yake hapa duniani kwa jeneza lenye mwili wake kuzikwa nyumbani kwake, Kijiji cha Butiama, wilayani Butiama, Mkoa wa Mara.

Safari hiyo ya mwisho ya Jenerali Musuguri aliyezaliwa Januari 4, 1920 ameihitimisha kwa mazishi ya kijeshi yaliyokwenda sambamba na mizinga 17 kupigwa. Miongoni mwa watu waliohudhuria maziko hayo ni wakuu wa majeshi wastaafu wakiwamo Robert Mboma, George Waitara na Venance Mabeyo.

Jenerali Musuguri alifariki Oktoba 29, 2024 katika Hospitali ya Bugando, Mwanza alipokuwa akipatiwa matibabu. Hadi anafariki  alikuwa na umri wa miaka 104, miezi tisa na siku 25. Alistaafu kwa heshima utumishi jeshini mwaka 1988.

Mwaka 2020, wakati Jenerali Musuguri alipoadhimisha miaka 100 ya kuzaliwa kwake alisema alikuwa na wanawake saba, watoto 32, wajukuu zaidi ya 70 na vitukuu zaidi ya 100.

Shughuli hiyo ya mwisho ya Jenerali Musuguri iliyohudhuriwa na mamia ya waombolezaji imeongozwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ambaye amesema kuwa Jenerali Musuguri ameacha funzo kubwa kwa Watanzania juu ya umuhimu wa amani na mshikamano,  hivyo kila mmoja anapaswa kuyaishi maisha hayo.

“Wote tunaofanya siasa na shughuli nyingine tukumbatie amani na kuifanya kuwa tunu ya Taifa letu, kwani katika maisha yake yote Jenerali Musuguri hakupenda vita na alikuwa akiamini na kusema vita ni mauaji hivyo tunapaswa kujua kuwa bila Taifa lenye amani hakuna maendeleo,” amesema.

Amesema Jenerali Musuguri ameacha urithi mkubwa kwa Watanzania ikiwamo uzalendo na alikuwa mwalimu wa wengi katika hilo na ni alama isiyofutika.

Amesema Jenerali Musuguri alijitolea kuhakikisha Tanzania inakuwa salama na yenye amani ili kumuenzi kwa vitendo kila mmoja anapaswa kuwa na moyo wa kizalendo na kulinda mshikamano wa nchi, ili udumu siku zote.

Alichokisema Waziri Tax, CDF

Awali, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Stergomena Tax amesema Taifa, wizara yake na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) vimepoteza mtu muhimu na kinachotakiwa ni kumuenzi kwa yale yote aliyoyatenda ikiwemo uhodari, ujasiri, uadilifu, upendo na weledi wakati wote wa utumishi na uhai wake.

Naye Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Jacob Mkunda amesema mchango wake katika suala zima la ulinzi wa nchi ni mkubwa na hauwezi kusahaulika, kwani  alitumia miaka yake 44  kulitumikia Jeshi la Wananchi (JWTZ) kwa uhodari, ushujaa, uaminifu na uadilifu mkubwa.

Amesema askari wa jeshi hilo wanayo mengi ya kujifunza kupita kwa Musuguri huku akisema kupitia ushiriki wake kwenye vita aliweza kujengeka na kuwa mahiri na kutumia uzoefu huo kwa manufaa ya JWTZ na kusaidia kuandaa mipango mbalimbali ya ya jeshi hilo ikiwemo mipango ya vita.

 “Musuguri ni miongoni mwa waanzilishi wa JWTZ na amepata kuhudumu katika nafasi mbalimbali mfano kwenye vita dhidi ya uvamizi wa nchi yetu (vita ya Kagera) kwa ujumla alitoa mchango mkubwa sana wa ushindi katika vita hivyo,” amesema Jenerali Mkunda.

Wazee wa Kizanaki wamzungumzia

Chifu wa kabila la Wazanaki, Japhet Wanzagi amesema wazee wa Kizanaki wamepoteza mtu muhimu ambaye alikuwa kimbilio la kila mtu kwa rika na jinsia zote katika jamii hiyo, ambaye alikuwa tayari kuzivaa shida za mtu aliyefika kwake kuhitaji msaada wa mali na hali.

Amesema licha ya umaarufu aliokuwa nao, Musuguri alikuwa mtu wa aina yake kwani alikuwa na kipaji, karama, uwezo na utu wema na kwa kiasi kikubwa alisaidia katika kudumisha mila na tamaduni za kabila hilo.

“Mimi binafsi alinisaidia sana katika suala zima la mila na desturi zetu, alikuwa akiwalea vijana katika misingi bora ya mila na desturi, kwa ujumla miaka yake 104 ilikuwa ni zawadi kwetu na tutamkumbuka siku zote na tutamuombea apumzike kwa amani siku zote, kwani maisha aliyoishi ni tunu adimu sana,” amesema.

Akiendesha misa ya mazishi, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma, Michael Msongazila amesema Jenerali Musuguri alipigana vita vya haki wakati wa vita vya Kagera mwaka 1978/79.

“Jenerali Musuguri ni shujaa wa vita vya kidunia lakini pia ni shujaa wa vita ya kiroho, kwani baada ya kustaafu aliamua kurudi katika imani yake na nilimbatiza pamoja na kumfungisha ndoa mwaka 2014 baada ya kumchagua mke mmoja kati ya wake zake wengi aliokuwa nao, tumuombee na tujifunze kupitia kwake,” amesema.

Amesema kwa mujibu wa kanuni za kanisa hilo, Musuguri alitakiwa kuchagua mke mmoja wa kufunga naye ndoa wengine wakibakia kuwa wasaidizi wake, huku akitakiwa kuwatunza jambo ambalo amelitekeleza hadi alipokutwa na mauti.

Askofu Msongazila amesema Musuguri ni miongoni mwa watu wenye bahati kwani hata baada ya kupigana vita vingi ikiwepo vita ya pili ya dunia, vita nje ya Tanzania kwa lengo la ukombozi wa bara la Afrika pamoja na vita vya  Kagera. “Amebahatika kuishi zaidi ya miaka 40 tangu vita vya mwisho alivyopigana.”

Related Posts