BAADA ya kurejeshwa kikosini na kuisaidia Tanzania Prisons kushinda dhidi ya KenGold, kipa wa timu hiyo, Edward Mwakyusa amesema anataka kujihakikishia namba na kuisaidia timu kuendelea kufanya vizuri.
Mwakyusa aliyepandishwa kikosini 2022/23, anakumbukwa kuiokoa timu hiyo msimu huo kukwepa kushuka daraja alipoizuia JKT Tanzania kwenye mechi ya mchujo (play off).
Katika mchezo huo wa marudiano uliopigwa Uwanja wa Sokoine, JKT Tanzania ilihitaji ushindi, lakini Mwakyusa alikuwa imara langoni na kuzuia hatari zote ambapo kutokana na kazi nzuri aliyoifanya, alichangia ushindi wa bao 1-0 uliofanya jumla kushinda 2-1 na kubaki salama.
Tangu alipomaliza mechi hiyo, kinda huyo hakuonekana uwanjani kwani msimu uliopita Yona Amos ambaye kwa sasa anacheza Pamba Jiji ndiye alikuwa chaguo la kwanza kikosini akisaidiwa na Mussa Mbisa.
Juzi, Prisons ikicheza mechi ya Dabi ya Mbeya dhidi ya KenGold, Mwakyusa ndiye alikabidhiwa jukumu la kusimama golini na kuisaidia timu hiyo kushinda bao 1-0 akiiweka timu katika nafasi ya 11 kwa pointi 10.
Mwakyusa aliliambia Mwanaspoti kuwa kwa sasa anataka kuonyesha uwezo wake bora mazoezini ili kumshawishi Kocha Mbwana Makata amuamini kumpa uhakika wa namba.
Alisema pamoja na kusaka namba, anapambania Prisons kuhakikisha inaondokana na matokeo yasiyoridhisha akibainisha kuwa hadi sasa hawapo nafasi nzuri.
“Ni muda mrefu nilicheza, lakini nashukuru nimeanza bila kuruhusu wavu wangu (kufungwa bao), nakwenda kupambana kujihakikishia namba, lakini kubwa zaidi kuipa matokeo matokeo timu,” alisema kipa huyo ambaye pia ni askari wa Jeshi la Magereza.