· Stanbic Bank yatoa TZS milioni 80 kwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Heart Team Africa Foundation kusaidia kugharamia matibabu muhimu kwa watoto.
· Hafla ya kuchangisha fedha, iliyoongozwa na Rais Mstaafu Mh. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, imewaleta pamoja wadau kutoka sekta za umma na binafsi kwa lengo la kusaidia watoto wenye magonjwa yanayotishia maisha.
· Mchango huu unaonyesha dhamira ya Stanbic Bank katika kuwekeza kwa jamii kwa vitendo kupitia sekta ya afya na ustawi wa jamii kote Tanzania.
Benki ya Stanbic Tanzania imetoa TZS milioni 80 kwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Heart Team Africa Foundation kusaidia matibabu muhimu kwa watoto wanaokabiliwa na magonjwa ya moyo na mishipa ya damu. Mchango huu ulitangazwa katika hafla ya kuchangisha fedha iliyofanyika katika Hoteli ya Johari Rotana, Dar es Salaam, ambapo Rais Mstaafu Mh. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliongoza kama Mgeni Rasmi, akisisitiza umuhimu wa juhudi za pamoja za jamii kusaidia watoto wanaohitaji.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Stanbic Tanzania, Bw. Manzi Rwegasira, alieleza fahari ya benki hiyo kuwa mshirika wa JKCI na Heart Team Africa Foundation. “Tunajivunia kuunga mkono juhudi hizi muhimu za kuwasaidia watoto kupata matibabu ya kuokoa maisha na kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa familia zinazokabili changamoto hii,” alisema Rwegasira. “Stanbic Bank tunaamini katika kurudisha kwa jamii tunayoihudumia, na ushirikiano huu unaonyesha dhamira yetu ya kuleta mabadiliko chanya kwenye sekta ya afya hapa Tanzania.”
Inakadiriwa kuwa watoto 1,500 nchini Tanzania hugundulika na matatizo ya moyo ya kuzaliwa kila mwaka, ambapo gharama za matibabu mara nyingi ni mzigo mkubwa kwa familia nyingi. JKCI na Heart Team Africa Foundation husaidia kwa kutoa ruzuku ya matibabu na kusaidia kupunguza gharama hizo. Fedha zinazokusanywa kupitia hafla hii zitaelekezwa moja kwa moja kusaidia familia hizi, ambapo TZS milioni 4 zinahitajika kusaidia matibabu ya kila mtoto mmoja.
Mchango huu unaendeleza jitihada za Uwekezaji wa Kijamii wa Stanbic Bank nchini Tanzania. Mbali na kusaidia sekta ya afya, Stanbic hivi karibuni imejihusisha na miradi ya maendeleo ya elimu kupitia uboreshaji wa shule mkoani Dodoma, Geita, na Bunda, ikijumuisha michango ya madawati, kampeni za kupanda miti, na programu za elimu ya kifedha kwa wanafunzi. Miradi hii ni sehemu ya dhamira ya Stanbic ya kuinua jamii za Kitanzania na kukuza maendeleo endelevu.
Stanbic Bank inatoa wito kwa sekta zote za jamii kuunga mkono miradi inayotoa matumaini kwa watoto wa kesho. Kama alivyohitimisha Rwegasira, “Pamoja, huruma na ukarimu wetu unaweza kuleta mabadiliko makubwa.”
Rais Mstaafu wa awamu ya nne wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete akimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Stanbic Tanzania, Bw. Manzi Rwegasira Tuzo ya kuthamini mchango wa Benki ya Stanbic kwa ajili ya kuchangia kusaidia gharama za matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo na mishipa ya damu nchini. Benki ya Stanbic Tanzania ilichangia shilingi milioni 80 kwenye harambee hiyo iliyoandaliwa na JKCI na Heart Team Africa Foundation iliyofanyika jijini Dar es salaam mwishoni mwa wiki.