Tanga/Morogoro. “Nilimaliza shule mwaka 2007 (darasa la saba) tangu hapo mpaka sasa ninafanya kazi ya kuzalisha mkaa, sina shughuli nyingine. Nina mke na watoto watatu ambao maisha yao yananitegemea mimi.”
Hiyo ni kauli ya Hassan Bashiru, mzalishaji mkaa katika Kijiji cha Madebe, Kata ya Kang’ata wilayani Handeni Mkoa wa Tanga.
Bashiru anasema kwa siku anazalisha kati ya gunia 10 mpaka 15 ya mkaa anayouza Sh2,000 hadi Sh7,000. Anasema iwapo atapata ajira hata ya muda kwenye maeneo yao, yeye na wenzake wapo tayari kuacha biashara ya mkaa ambayo wanafahamu madhara yake kwa mazingira.
Kwa upande wake, Hamisi Makuya anayefanya biashara hiyo anashauri Serikali kuboresha miundombinu ya kilimo kwa wakulima wadogo, ili wapate faida na kuachana na biashara ya kuuza mkaa.
Mchoma mkaa eneo la Mafili wilayani Mvomero Mkoa wa Morogoro, Costa Mluge anasema ameanza kazi hiyo zaidi ya miaka 10 iliyopita na aliwahi kuugua kifua kikuu kutokana na vumbi la mkaa, baada ya kupona ameendelea na kazi hiyo.
“Sikusoma, sijawahi kuajiriwa popote. Hii ndiyo kazi inayonisaidia kupata riziki ya kula na familia yangu, lakini ni kazi ngumu na ya hatari. Porini tunakutana na mengi kama vile wanyama wakali lakini nitafanyaje watoto (wanne) wanataka kula na kwenda shule,” anasema.
Mluge anasema kama atawezeshwa kupata shughuli nyingine itakayomuingizia kipato yuko tayari kuacha kazi hiyo.
“Tanuri moja la mkaa naweza kupata viroba 10 hadi 12 na kiroba kimoja huku porini kwa sasa nauza kati ya Sh12,000 ha Sh15,000,” anasema.
Matha James, mfanyabiashara ya mkaa na kuni katika Manispaa ya Morogoro, anasema ana mwaka mmoja tangu aingie kwenye biashara hiyo inayomuwezesha kupata fedha ya kulipa kodi, kusomesha watoto wake wawili na kujikimu kwa mahitaji mengine muhimu.
“Kuni na mkaa naletewa na watu wanaokata porini, mara nyingi zinatoka Mvomero, nina kibali ndiyo maana nauza hapa hadharani, mara nyingi wanakuja watu wa maliasili (TFS) nawaonyesha kibali changu wananiacha,” anaeleza.
Matha anasema anafahamu kuwa misitu inateketea, lakini gharama za nishati nyingine ni kikwazo, akitoa mfano wa wateja wake wakubwa kuwa ni mama na baba lishe ambao wakinunua mkaa au kuni za Sh500 au Sh1,000 zinawaosha kwa kutwa.
Wakati ukataji misitu ukitajwa kuchochea athari za ongezeko la mabadiliko ya tabianchi, Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022-2032) unakadiria hekta 469,420 za misitu zinateketezwa kila mwaka nchini kwa shughuli za binadamu, ikiwemo uhitaji wa nishati.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa kurejesha misitu hiyo, wananchi wanatakiwa kupanda na kutunza ukubwa wa hekta 185,000 ambazo ni sawa na miti milioni 2.28 kwa mwaka ndani ya miaka 17 mfululizo tangu 2019.
Tafiti ya mwaka 2022 iliyotolewa na Mfuko wa Umoja wa Mataifa ilibaini Mkoa wa Dar es Salaam unatumia asilimia 50 ya mkaa unaozalishwa nchini ambao unatoka mikoa ya Pwani, Lindi, Morogoro, Iringa na Tanga.
Wilaya ya Handeni mkoani Tanga inatajwa kuwa miongoni mwa zinazokabiliwa na uvunaji wa mkaa kwa wingi, soko kubwa likiwa Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa uongozi wa wilaya, mwaka 2022 magunia 600 ya mkaa yalikamatwa ndani ya msitu wa hifadhi Lugala uliopo Kata ya Kwamsisi ambao una hekta 7,800, huku asilimia 50 ya hifadhi hiyo ikiwa tayari ilishaharibiwa.
Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, Mkuu wa Wilaya, Judith Nguli anaeleza mwaka 2023 hadi 2024 imetoa vibali 111 kati ya hivyo, vya mkaa ni 44, vya magogo 56 na 11 ni vibali vya kuni.
“Gharama za vibali vya uvunaji wa mazao ya misitu ambavyo vinasimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) gunia moja lenye uzito wa kilo 50 linalipiwa Sh12,500 tu, gharama hizi ni ndogo ukilinganiaha na manunuzi ya gesi ambayo mtungi mdogo tu ni zaidi ya Sh20,000,” anasema Nguli.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Madebe wilayani Handeni, Kassim Malumbi anasema, “watu wanaitumia njia ya kukata mkaa kama ajira, kwa maana utakapomkataza aache kufanya biashara hiyo, ni sawasawa na kumkatisha maisha yake.”
Malumbi anasema uvunaji upo kwa kiasi kikubwa na ukiingia msituni utakuta wapo wenye gunia 20 mpaka 100 za mkaa, ila wanaendelea kutoa elimu wapunguze biashara hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Albert Msando anasema Serikali imechukua hatua maalumu za kuhamasisha na kuelimisha wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia, kwa kupunguza kutoa vibali kwa watu wanaokata mkaa.
“Tutaendelea kupunguza utoaji wa vibali mtu akiomba kibali cha kuvuna magunia 2,000 tunampa cha gunia 1,000, lengo ni kupunguza uvunaji na baadaye kufuta kabisa utoaji vibali,” anasema.
Anasema wanatoa elimu na kubuni njia mbadala za kuwapatia ajira kwa kuandaa matamasha, makongamano na kutumia waandishi wa habari kama motisha kwa wananchi katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Nguli akizungumzia elimu anasema, “Wilaya ya Mvomero tuna kampeni ya ‘Tutunzane’ inayohamasisha kilimo rafiki cha mazingira baada ya kugundua kuwa wananchi wengi wanaoishi kwenye vijiji jirani na hifadhi wanajihusisha na ukataji mkaa.”
Kupitia kampeni hiyo anasema wanagawa mbegu za ufuta, alizeti na mazao mengine ambayo hayaathiriwi na wanyama wa misituni. Anasema halmashauri inatoa motisha kwa vikundi vinavyofanya shughuli za uhifadhi wa mazingira na misitu, lakini vinavyozalisha mkaa mbadala.
Ofisa mazingira mwandamizi kitengo cha mazingira Mvomero, Msangi Ramadhani anasema kwa uhifadhi msitu, shirika moja limepata ruzuku na kwa kutumia vikundi vilivyopo katika vijiji vya Mkindo na Bungoma, wametengeneza majiko banifu yanayotumia kiasi kidogo cha mkaa. Anasema teknolojia hiyo imesambaa katika vijiji vya jirani.
Ofisa mazingira huyo anasema wanahamasisha uundwaji wa kamati za utunzaji mazingira kwenye vijiji kutoa elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kupitia vikao na majukwaa mengine.
Mdau wa utunzaji endelelevu wa mazingira kutoka Shirika la Suhode, Frank Luvanda anasema asasi za kiraia zina mchango mkubwa katika kusaidia nchi kufikia malengo ya mkakati wa kitaifa wa miaka 10, kwani mbali ya kuharibu mazingira, nishati chafu zimekuwa zikisababisha changamoto za kiafya.
“Ndiyo maana bibi zetu vijijini kumekuwa na kesi za kuambiwa wachawi na wengine wanauawa pale wanapoonekana kuwa na macho mekundu, kumbe shida ilianzia kwenye kuni wanazopikia. Sasa kizazi hiki lazima kitoke huko,” anasema.
Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.