Tanzania kuwasilisha COP29 maandiko ya miradi ya Dola milioni 1

Tanzania
inatarajia kuwasilisha maandiko ya miradi mikubwa tisa ya kimkakati yenye
thamani ya Dola za Marekani bilioni 1,433 katika Mkutano wa 29 wa Nchi
Wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP29) utakaofanyika Baku,
Azerbaijan kuanzia Novemba 11 hadi 22, 2024.

Lengo
la kuwasilisha maandiko hayo ni kutafuta fedha kwa ajili ya kukabiliana na
mabadiliko ya tabianchi ambayo Tanzania inapambana nayo.

Katibu Mkuu Ofisi
ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema hayo wakati akizungumza
kwenye kipindi cha Mazingira Yetu na Tanzania Ijayo kilichorushwa na Kituo cha
runinga cha TBC1 na kutayarishwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.

Amesema Ujumbe wa Tanzania
utaongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.
Philip Isdor Mpango ambaye atamwakilisha Rais wa
Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mhandisi Luhemeja amesema katika mkutano huo kutakuwa na majadiliano
yatakayohusisha viongozi pamoja na wataalamu kutoka nchini yanayolenga kuweka
msimamo wa pamoja katika masuala mbalimbali ya hifadhi ya mazingira.

Aidha, amesema Tanzania itakuwa na banda la maonesho
ambapo shughuli mbalimbali zinazofanyika nchini katika kukabiliana na athari za
mabadiliko ya tabianchi zitakuwa zikioneshwa.

Amesema, kwakuwa mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ni vita ambayo nchi inaendelea
kupambana nayo na kwamba inahitaji juhudi za pamoja ili kuhakikisha inafanikiwa
na kuwa wananchi wanapaswa kuacha kukata miti na badala yake waipande na
kuitunza.

Amesema Serikali
imewekeza katika mazingira hivyo wananchi hawana budi kuiunga mkono na ndio
maana imekuja na ajenda ya nishati safi ya kupikia kupitia kwa kinara wa Afrika
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Katika mkutano wa
COP29 tunataka kuionesha dunia namna nchi yetu inavyohamasisha matumizi ya
nishati safi ya kupikia na hivyo kutuwezesha ku
pata
wadau ambao wataongeza nguvu katika ajenda hii na hivyo tunaweza kupata nishati
kwa gharama nafuu kwa wananchi wetu,” amesema huku akisisitiza kuwa nishati
safi si tu gesi bali ni nyenzo mbalimbali zisizohusisha ukataji wa miti.

Katibu Mkuu
Luhemeja ameongeza kuwa nishati safi ya kupikia ni nyenzo muhimu ya kukabiliana
na uharibifu wa mazingira ambayo inaokoa miti ambayo ingekatwa ili kupata kuni
na mkaa vitendo ambavyo vinaweza kusababisha jangwa.

Amesema
mkutano huo utachagizwa na kaulimbiu ya kitaifa iliyopendekezwa ambayo ni
‘Kutumia Fursa za Biashara ya Kaboni katika matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia
pamoja na vyanzo vya nishati mbadala’.

 

Kaulimbiu
hii imelenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kutunza mazingira
na kujenga uwezo wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi katika kukuza uchumi
wa taifa na kuchochea maendeleo endelevu.

Related Posts