Faida, vikwazo nishati safi ya kupikia

Morogoro/Pwani. Dhima kuu ya Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034) uliozinduliwa Mei mwaka huu inalenga kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia iliyo nafuu, endelevu, salama na rahisi kutumika.

Mkakati huo uliozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, unalenga kutoa mwongozo wa namna ya kupunguza athari za kiafya, mazingira na kuboresha maisha ya wananchi, huku ukipunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Licha ya ukweli kwamba mpango huo unawataja zaidi ya robo tatu ya wananchi wanatumia nishati zisizo rafiki kwa mazingira za kuni na mkaa, wapo wanaotumia nishati safi na wanaeleza walivyopunguza gharama za nishati na kuimarisha maisha yao baada ya kutumia nishati safi.

Frank Joseph, baba lishe katika Kijiji cha Dakawa wilayani Mvomero, anasema awali alitumia mkaa kupikia, lakini wateja waliongezeka na chakula kilihitajika kingi na kwa haraka, ndipo aliamua kuchanganya matumizi ya gesi na mkaa.

“Hapa napika kuanzia asubuhi chai, supu na vitafunwa; mchana napika chakula na jioni pia. Si kwamba mapishi yote natumia gesi, hapana! Isipokuwa nimepunguza matumizi ya mkaa na imeniongezea ufanisi,” anasema Joseph.

Anasema awali gunia moja la mkaa alitumia kwa siku tatu, lakini tangu ameanza matumizi ya gesi sasa anatumia gunia hilo kwa siku kati ya 10 hadi 14.

Kwa mujibu wa Joseph, mkaa huo hununua kwa Sh60,000 kwa gunia na gesi anabadilisha kwa kati ya Sh100,000 na Sh120,000 kwa mtungi wa kilo 38 anaotumia kwa siku hadi 15. Hii ina maana Joseph anatumia wastani wa Sh160,000 kwa siku saba na Sh260,000 kwa siku 15, tofauti na wastani wa Sh350,000 kabla hajaanza matumizi ya nishati hiyo.

Hadija Hamisi, mama lishe eneo la Jamhuri, Morogoro Mjini anasema anatumia gesi kupikia na kwa kiasi kikubwa imefanya eneo lake la biashara kuwa safi wakati wote, tofauti na awali, jambo lililomuongezea wateja.

Licha ya ufanisi wa gesi, anasema analazimika kuchanganya na mkaa akitaja ukubwa wa gharama ya bidhaa hizo kama kikwazo.

“Tunaomba Serikali ifanyie kazi gharama za gesi zipungue, vinginevyo haya majiko ya gesi yatabaki majumbani kama mapambo. Mimi kwenye mgahawa natumia Sh105,000 hadi Sh115,000 kununua gesi ambayo napikia kwa siku tatu hadi nne,” anasema.

Kutokana na gharama kubwa za gesi, anasema huitumia kupikia chai, maziwa, mboga za majani na vyakula vingine vyepesi, akieleza hawezi kupikia maharage au makande kwenye gesi na kwamba hulazimika kununua mkaa.

Mfanyabiashara wa chipsi, eneo la Morogoro Mjini, James Fabian anasema ameachana na mkaa na kuni baada ya kuona anapoteza muda mwingi kuwasha moto, kupoteza wateja kutokana na moshi na uhaba wa bidhaa hiyo wakati wa masika.

Hili lilimlazimisha Fabian kutumia mabaki ya mbao (maranda) ambayo amekuwa akinunua kiroba kimoja kwa Sh1,000.

“Kuni na mkaa niliona ni changamoto kwangu, kuna wakati hasa kipindi cha masika vinaadimika na kuna wakati natumia gharama kununua mkaa ambao hauwaki vizuri, ndiyo maana nikaona nitumie maranda, viroba vyangu vinne napikia siku nzima,” anasema.

Anasema kwa kutumia maranda anapunguza gharama mara mbili kama angetumia gesi na mkaa.

Anasema anatamani kutumia gesi, lakini gharama kubwa ni kikwazo, akieleza iwapo itashuka atatumia. Hali si tofauti mkoani Pwani, kwani mkazi wa Kitongoji cha Bwawani Mzenga wilayani Kisarawe, Lina Joseph anasema huchanganya matumizi ya gesi na mkaa.

“Gesi ni gharama lakini inanisaidia, hasa wakati wa usiku nikiamka kupasha maziwa ya watoto na asubuhi pia. Mkaa mpaka uwashe ukolee si leo. Kupika mara nyingi natumia mkaa,” anasema.

Lina ambaye ni mwalimu wa shule ya awali anasema gharama za mkaa zipo chini, akieleza akinunua wa Sh1,500 anapika kutwa nzima.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Bwawani Mzenga, Omary Othman anasema watu hawataki kutumia nishati safi kwa kuwa inapika vyakula laini pekee na kuivisha haraka. “Gharama kuwa juu ni sababu ya watu kuendelea kutumia kuni na mkaa, watu wanafikiria wanunue gesi Sh26,000 wakati kiroba cha mkaa Sh7,000 atatumia wiki nzima,” anasema.

Omary anasema sababu nyingine ni kuwa kaya zina watu wengi, hivyo wanaona matumizi ya gesi hayawezi kutosheleza bali watajiongezea gharama za maisha.

Mikakati kupunguza gharama ya nishati

Dhima ya mkakati wa kitaifa wa miaka 10 imelenga kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia iliyo nafuu, endelevu, salama na rahisi kutumika.

Ofisa Mjiolojia kutoka Wizara ya Nishati, Ngeleja Mgejwa anasema baada ya tafiti maeneo mbalimbali nchini, Serikali iliona umuhimu wa kuweka mkakati utakaohakikisha upatikanaji wa urahisi na gharama nafuu wa nishati safi kwenye maeneo ya watu.

“Tunatengeneza mazingira kwa kuweka miundombinu ifike hadi kwa wananchi na kupata eneo fulani, wengine watatumia mitungi ya gesi na baadhi watatumia umeme na wengine watatumia mkaa mbadala,” anasema.

Anasema kwa kufanya hivyo wananchi watakuwa wanatumia nishati kulingana na eneo na teknolojia inayoweza kuwa rahisi kwao, akieleza bado wanaendelea kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa nishati safi.

Ili kukabiliana na gharama kubwa, Mgejwa anasema maelekezo yameshatolewa kuangaliwe namna kama ni gesi wananchi wawe na uwezo wa kununua kulingana na fedha waliyonayo.

“Gharama za gesi ni suala linaloendelea kufanyiwa kazi, kwanza lazima nishati ipatikane mahali popote kwa kuwa na miundombinu rafiki na kwa bei nafuu kulingana na maeneo husika,” anasema.

Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Judith Nguli anaeleza, “licha ya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi, pia tunafanya ushirikishaji wa wadau na taasisi nyingine za mazingira zinazotoa elimu juu ya uhifadhi na matumizi ya nishati safi.”

Nguli anasema halmashauri imekuwa ikitoa motisha kwa vikundi vinavyofanya shughuli za uhifadhi wa mazingira, misitu lakini vinavyozalisha mkaa mbadala.

Pia wapo wanawake wamepewa mitungi ya gesi, ili kuwahamisisha juu ya matumizi. “Tayari tumeanza kutoa elimu kwenye shule zetu za bweni kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia na zipo baadhi ya shule zimeanza kutumia nishati mbadala. Bado tutaendelea kutoa elimu kwenye taasisi nyingine kama vyuo, viwanda na hospitali,” anasema.

Katibu Tawala Mkoa wa Pwani, Rashid Mchatta anasema changamoto inayowakabili wanahitaji fedha nyingi za kufanya uwekezaji unaohitajika.

“Tumeanza na taasisi zenye watu wengi na kuwaandikia mikakati ya kwenda kwenye nishati mbadala, mikakati ni endelevu na inahitaji uwekezaji mkubwa. Tumekuwa tukishirikiana na taasisi binafsi kufanya tathimini kujua ni kiasi gani kinahitajika,” anasema.

Anasema baada ya kufanya tathimini wametoa maelekezo kwa kila mkurugenzi wa wilaya kuweka mipango katika maeneo yao, ili kuunga mkono juhudi za Serikali.

Anaeleza kuna mradi wilayani Bagamoyo unaotoa elimu kwa wananchi kuingia kwenye nishati mbadala kwa ngazi ya vijiji, pia wapo wadau wanaounga mkono juhudi hizo.

Mbali ya hayo, anasema wanaendelea kutoa mafunzo kwa wakuu wa shule kutambua umuhimu wa nishati mbadala na waachane na matumizi ya kuni na mkaa.

“Tuna taasisi tunazoshirikiana nazo zinatoa semina kwa wadau tofauti kuhusu nishati mbadala kwa kubadilisha takataka,” anasema.

Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation

 Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts