Wamarekani leo kuamua ni Trump au Kamala

Washington. Wamarekani wanatarajia kupiga kura leo kukamilisha mbio za uchaguzi mkuu wa Taifa hilo lenye nguvu duniani zilizotanguliwa na kampeni za wagombea, Rais wa zamani, Donald Trump na Makamu wa Rais, Kamala Harris.

Mshindi katika uchaguzi huo, atatangazwa kuwa Rais wa 47 wa Marekani, akichukua nafasi ya Rais Joe Biden aliyekuwa madarakani kwa muhula mmoja wa miaka minne.

Jana, Trump na Kamala waliendelea na kampeni katika majimbo yasiyo ngome ya chama chochote, wakitafuta kuungwa mkono na wananchi katika majimbo hayo ili kujihakikishia ushindi.

Kampeni hizo zilitawaliwa na mbwembwe zao katika majimbo ya Georgia, Michigan na Carolina Kaskazini, huku wakishinikiza kuungwa mkono katika siku za mwisho za kampeni.

Kamala alijaribu kuwavutia Wamarekani huko Michigan kwa kusisitiza hali mbaya ya vita vya Israeli huko Gaza na Lebanon, lakini watetezi wa jamii wanasema kuwa, maneno pekee hayatoshi.

Kwa upande wake, Trump anakabiliwa na ukosoaji mpya kuhusu mashambulizi yake dhidi ya waandishi wa habari baada ya kusema wakati wa mkutano wa kampeni huko Pennsylvania kwamba, hatajali sana ikiwa muuaji anaweza kurusha habari za uwongo ili kumfikia.

Takribani Wamarekani milioni 78 tayari wamepiga kura za awali, kwa mujibu wa chumba cha kuhesabia kura katika Chuo Kikuu cha Florida.

Kabla ya siku ya uchaguzi, wafuasi wa Trump wanadai kuwa, mwaka 2020 mfanyakazi wa ngazi ya juu wa mfumo wa kupigia kura wa Dominion aliwaambia wanachama wa Antifa alihakikisha Trump hatashinda.

“Usijali kuhusu uchaguzi, Trump hatashinda. Nilihakikisha kuwa hatashinda,” linasema chapisho la Novemba mosi kwenye mtandao wa Instagram. Chapisho hilo linahusisha nukuu hiyo kwa Eric Coomer, aliyetambuliwa kama mkurugenzi wa mikakati na usalama wa Dominion. Chapisho hilo pia linasema Coomer alitoa taarifa hiyo wakati “akizungumza kwenye simu ya mkutano wa Antifa.”

Kwa sasa, hali ya kura za maoni ni ngumu sana katika majimbo saba ya mapambano ambayo ni majimbo yenye umuhimu mkubwa katika uchaguzi huu.

 Hali hii inafanya iwe vigumu sana kwa wachambuzi na wapigakura kujua ni nani anayeshikilia nafasi ya kuongoza katika mbio hizi za urais.

Kura za maoni za hivi karibuni zinaonyesha kuna tofauti ndogo sana, chini ya asilimia moja, inayotenganisha wagombea wawili katika majimbo kadhaa muhimu.

Hii inajumuisha Jimbo la Pennsylvania, ambalo ni muhimu sana kwa sababu lina idadi kubwa ya kura za uchaguzi.

Kwa hiyo, jimbo hili linaweza kuwa na athari kubwa kwa mshindi kufikia lengo la kura 270 zinazohitajika ili kushinda urais.

Pennsylvania, pamoja na majimbo ya Michigan na Wisconsin, yalikuwa ngome imara za Chama cha Democrats kabla ya Rais Trump kuzigeuza kuwa ngome za Chama cha Republican katika uchaguzi wa mwaka 2016.

Katika uchaguzi wa mwaka 2020, Rais Biden alifanikiwa kurejesha majimbo haya kuwa ngome za Democrats.

 Ikiwa Kamala atafanikiwa kufanya hivyo mwaka huu, itamuwezesha kuwa kwenye njia sahihi ya kushinda uchaguzi na kuingia katika nafasi ya urais.

Hali hii inaonyesha kwamba, mbio za uchaguzi zinaendelea kuwa ngumu na zinazoshikilia nafasi ya kushinda kutegemea na  wagombea wanavyoendelea kupambana katika majimbo hayo.

Kura za maoni zitakuwa na muhimu wa kuelewa mwelekeo wa mwisho wa uchaguzi na matokeo yatategemea sana hali ya majimbo haya muhimu.

Related Posts