Dar/Mikoani. Ukosefu wa elimu sahihi, gharama kubwa ya awali ya matumizi, uhaba wa malighafi na miundombinu kuwafikia ni baadhi ya changamoto zinazolalamikiwa na wananchi kuwa vikwazo vya kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Wanasema licha ya kuhitaji kutumia nishati hiyo, vikwazo hivyo vinawakatisha tamaa, huku baadhi wakidai ni bora kuendelea kutumia mkaa na kuni kama walivyorithi kutoka kwa babu zao, kwa kuwa upatikanaji wake ni rahisi katika mazingira wanayoishi.
Wasifu wa Msingi wa Idadi ya Watu na Hali ya Kiuchumi wa Tanzania wa Mwaka 2022 ulionyesha zaidi ya kaya nne kati ya tano nchini (asilimia 81.6) zinategemea mkaa na kuni, kama chanzo cha nishati ya kupikia.
Septemba 10 hadi 20, mwaka huu waandishi wa Mwananchi walitembelea baadhi ya maeneo katika mikoa ya Pwani, Tanga, Dar es Salaam na Morogoro ambako wananchi walieleza ugumu wa kutumia nishati rafiki kwa mazingira.
“Natumia gesi nina miaka mitatu sasa unakuta wakati mwingine inaisha ghafla na gharama za kujaza ni Sh25,000, hatuna maduka ya huduma hiyo jirani, tunalazima kwenda kujaza wilayani Bagamoyo. Ukiongeza na gharama ya bodaboda ni Sh29,000,” anasema Aisha Salum, mkazi wa Kitongoji cha Madukani.
Hoja hiyo inaungwa mkono na Ilima Othuman, anayesema walio wengi wamenunua mitungi hadi kwa Sh55,000 lakini shida wanayopitia ni kukosa fedha ya kwenda kujaza na gharama za usafiri hadi huduma zinakopatikana.
“… hizo ni fedha nyingi, hivyo bora kuweka kando na kutumia mkaa au kuni,” anasema.
Matha James, mkazi wa Manispaa ya Morogoro anasema, “mimi pale nyumbani nina jiko la gesi, lakini ni mara chache natumia tena kwa kupika vitu vyepesi kama chai na kupasha chakula kwa sababu najua ikiisha kujaza ni fedha nyingi.”
Salmin Shaaban, mkazi wa Bagamoyo anasema changamoto nyingine ni imani, akieleza wanaamini gesi haiivishi chakula vizuri na ili kiive na kiwe kizuri, mfano wali lazima uokwe kwa kupalia moto wa mkaa juu.
“Ukipika wali kwa kutumia gesi na kwa kutumia mkaa kuna tofauti kubwa. Hata ladha yake ni tofauti na kuna vyakula vingine kama kunde na maharage vinachukua muda mrefu kuiva inakuwa ngumu kutumia gesi,” anasema.
Mbali ya hilo, anasema wanaogopa gesi kwa sababu huwa inalipuka.
Anasema iwapo Serikali itafanikiwa kuwawezesha kuacha mazoea ya kutumia nishati zilizotumiwa tangu enzi za mababu itakuwa jambo zuri wao, ingawa anasema si rahisi kupata mafanikio kwa haraka. “Ukinunua mkaa wa Sh1,000 una uwezo wa kupikia hata milo mitatu kwa siku, kwa hiyo tukipiga hesabu Sh1,000 kwa mwezi unaweza kupata mkaa wa kutumia bila kuchoka tofauti na mtungi wa gesi unaweza kutubana katika matumizi,” anasema.
Mama lishem Rehema Mkomwa aliye wilayani Handeni mkoani Tanga anasema, “nimepata elimu ya matumizi ya gesi, ila kwa biashara yangu ni hasara, mtungi wa Sh23,000 natumia wiki mbili wakati mkaa wa bei hiyo unaweza kufika hadi mwezi.”
Mjasiriamali katika Mtaa wa Shauri Moyo, wilayani Bagamoyo, Subira Abdallah anasema watu wengi wanapenda kutumia nishati safi, lakini inakuwa ngumu kwa kuwa hawajawezeshwa. Anasema anafanya biashara ya kuuza chakula ambacho sahani moja ni Sh1,500, hivyo kwa mazingira hayo hawawezi kuwa na nishati safi kutokana na gharama za uendeshaji.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Madukani, Fatma Muhidin anasema anatambua athari zitokanazo na mazingira na amekuwa akijitahidi kuunga mkono mpango wa Serikali wa kupambana na uharibu.
“Tumekuwa tukifanya vikao kuhamasishana namna bora ya kutumia nishati safi, wananchi wanahamasika katika nyumba 10 unakuta walionunua mitungi ni wengi, changamoto iliyopo ni kubadilisha kwani watu hawana kipato cha uhakika.
“Bajeti zetu zimekuwa za siku, hatuwezi kupangilia nikiumwa itakuwaje? Chakula tumekuwa tukisuasua kwa sababu elimu ya bajeti ni shida. Tukikwamuka kwa mtu kujua kwa mwezi anatakiwa kutumia kiasi gani naamini jambo litakuwa rahisi,” anasema.
Fatma anaomba mamlaka husika kupitia mafunzo na warsha kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kuwa na bajeti kwa kujua mahitaji na yanapatikanaje.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Shauri Moyo, Mwanaharusi Sultani anasema katika eneo lake mwamko wa matumizi ya nishati safi hauridhishi, akieleza changamoto ni gharama za bidhaa hiyo.
“Hata wale wachache walionunua wakitumia ile gesi ya mwanzo wanashindwa kuendelea kujaza na kuanza kutumia tena nishati ya kuni na mkaa,” anasema.
Mfanyabiashara ya gesi katika Kijiji cha Mzenga wilayani Kisarawe, Alphonce Cleopa anasema hamasa ya wananchi kuingia katika matumizi ya nishati hiyo bado hairidhishi, kwani asilimia 80 ya wateja wake ni watumishi katika sekta ya umma na binafsi.
“Ili mwananchi apate mtungi lazima agharamie kuanzia Sh50,000 na kuendelea apate mtungi kamili, lakini kwa hali halisi ya uchumi wa wananchi wa Mzenga wanashindwa kumudu,” anasema.
Anapendekeza Serikali itoe ruzuku katika gesi, ili bei ishuke kuwawezesha wananchi wa kawaida kupata huduma, hasa wale wa vijijini. Pia anasema viwekwe vituo mtu akiwa na Sh2,000 apate huduma kulingana na kiwango cha fedha yake.
Mdau na Mwanaharakati wa Mazingira, Clay Mwaifwani anasema fedha ni tatizo katika matumizi ya nishati safi, hivyo ametaka mikakati iendane na kuongeza pato la Mtanzania.
“Ni wajibu wa Serikali kusimamia utajiri wa nchi na kuugawanya kwa watu wake, wengi tutaongea kuhusu nishati safi ya kupikia, lakini bosi ni hela. Maisha bora ni ongezeko la pato la mtu mmoja mmoja, awe na hela ya kuamua apikie gesi au umeme,” anasema.
Ofisa Mjiolojia kutoka Wizara ya Nishati, Ngeleja Mgejwa anasema Mei, mwaka huu Serikali ilizindua mkakati wa miaka 10 unaolenga asilimia 80 ya Watanzania watumie nishati safi hadi 2034.
“Tunachofanya sasa ni utekelezaji kwa uhamasishaji wa wananchi wafahamu vizuri nishati safi ipoje na aina ya nishati safi na unaona hadi viongozi wakubwa wanaonyesha mfano,” anasema.
Mgejwa anasema bila kuonyesha mfano Watanzania wengi hawawezi kuelewa, hivyo wabunge wamekuwa wakipewa mitungi kutoa kwenye makundi maalumu, akieleza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inafanya kazi kubwa.
“Tunaendelea kuhamasisha na kuwaambia wananchi suala la nishati ya kupikia linawezekana. Serikali inachokifanya ni kuhakikisha miundombinu inafika kwa wananchi, ili wapate huduma kwa bei nafuu,” anasema.
Akizungumzia gharama anasema, “tunatengeneza mazingira kwa kuweka miundombinu ifike hadi kwa wananchi na kupata eneo fulani wengine watatumia mitungi ya gesi, baadhi watatumia umeme na wengine mkaa mbadala,” anasema. Anasema katika aina hizo wananchi watakuwa wanatumia kulingana na eneo na teknolojia ipi inaweza kuwa rahisi kwao.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Aboubakar Kunenge, anasema walianza kutekeleza mpango huo wa miaka 10 baada ya kufunga mtungi wa tani 10 katika Shule ya Sekondari Ruvu Juu na kugawa mitungi ya gesi kwa wananchi, na kufanya kampeni za upandaji miti na kampeni ya kuzuia ukataji misitu kwa ajili ya mkaa na kuni.
Kunenge anasema wameweka msukumo kwenye elimu kwa kuwa wamebaini hata wakigawa mitungi ikiisha, waliyonunuliwa wanapata changamoto kwenda kujaza.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Albert Msando anasema Serikali imechukua hatua maalumu za kuhamasisha na kuelimisha wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia, kwa kupunguza kutoa vibali kwa watu wanaokata mkaa.
“Tutaendelea kupunguza utoaji wa vibali mtu akiomba kibali cha kuvuna magunia 2,000 ya mkaa tunampa nusu, lengo ni kupunguza uvunaji na baadaye kufuta kabisa utoaji vibali,” anasema.
Imeandikwa na Tuzo Mapunda, Rajabu Athumani na Hamida Sharrif kwa udhamini wa Bill & Melinda Gates Foundation.