Morogoro. Watu wasiofahamika wamevunja na kuondoka na misalaba iliyowekwa kwenye makaburi ya Kola, mkoani Morogoro.
Hatua hiyo imesababisha ndugu wa marehemu waliozikwa kwenye makaburi hayo kushindwa kuyatambua, huku wengine wakiingia hasara ya kuweka misalaba mingine.
Hii ni mara ya pili kutokea kwa matukio hayo ya kuvunjwa na kuibwa kwa misalaba na baadhi ya watu wanadai wanaoiba misalaba hiyo wanakwenda kuuza kama chuma chakavu.
Mwananchi limefika katika makaburi hayo na kujionea uharibifu huo uliofanywa na watu hao.
Ramadhani Libenanga, ndugu wa marehemu aliyefika makaburini hapo amesema ameshuhudia makaburi matatu ya ndugu zake yakiwa wameibwa misalaba na makaburi mengine zaidi ya 50 nayo yakiwa hayana misalaba.
“Nimefika hapa makaburi ya Kola kwa lengo la kusafisha kaburi la baba yangu na ndugu zangu niliowazika hapa, lakini cha kusikitisha nimekuta makaburi matatu ya ndugu zangu yakiwa yameibwa misalaba,” amesema Libenanga na kuongeza;
“Kwa hesabu ya harakahara hapa yapo zaidi ya makaburi 50 yameibwa misalaba, hii misalaba tunayoweka si urembo bali ni kumbukumbu ya kizazi na kizazi ili waje kujua mahala walipozikwa ndugu zao.
“Pia hii misalaba ni suala ya imani, hawa wanaoiba bila shaka hawana dini na wala hawajui kama kuna Mungu na kuna kufa, kama wangejua kuwa ipo siku nao watakufa wasingeiba misalaba hii,” amesema Libenanga.
Amesema vitendo hivyo vya wizi wa misalaba uliwahi kutokea miaka michache iliyopita, lakini kwa sasa matukio hayo yanarudi tena kwa kasi, hivyo kuliomba Jeshi la Polisi kuangalia namna ya kufuatilia biashara ya vyuma chakavu ambayo ndio chanzo cha wizi huo.
“Kabla ya biashara ya vyuma chakavu wizi huu wa misalaba haukuwepo, lakini baada ya biashara hii kushamiri ndio wizi huu nao umeshika kasi. Sio misalaba tu, tunashuhudia nguzo za taa za barabarani, kingo za daraja nazo zinakatwa na kwenda kuuzwa kama chuma chakavu.
“Lazima Serikali iwaangalie kwa hicho jingine hasa wauza vyuma chakavu, vinginevyo haya matukio yanaendelea kutokea,” amesema Libenanga.
Aidha, amesema baada ya kukuta makaburi matatu ya ndugu zake wameibwa misalaba, ameanza harakati za kutafuta pesa kwa ajili ya kununua misalaba mingine, ili makaburi hayo yasije yakasahaulika.
Akitoa ushauri wa namna ya kudhibiti, Libenanga ameiomba Halmashauri ya Manispaa Marogoro kuweka uzio kuzunguka makaburi hayo ama kuweka taa ambazo zitakuwa na mwanga mkali utakaozuia watu wenye nia mbaya kuingia kwenye makaburi hayo.
Naye Oswald Nyamoga, mkazi wa Lukobe Manispaa ya Morogoro amesema vitendo hivyo ni lazima vikomeshwe kwa nguvu zote, vinginevyo watu watayasahau makaburi ya ndugu zao.
“Polisi wafanye doria kwenye eneo hili la makaburi mara kwa mara na watakaobainika kufanya vitendo hivi sheria ichukue mkondo wake na wapewe adhabu kali, ili iwe fundisho,” amesema Nyamoga.
Mmoja wa mafundi waliokutwa makaburini hapo akifanya ukarabati wa makaburi yaliyoibwa misalaba, Luwa Said amesema vitendo hivyo vinafanywa na watu wasiokuwa na imani na hofu ya Mungu.
“Yaani hapa makaburi mengine yameibwa misalaba na vitendo hivi vitakuwa vinafanywa nyakati za usiku, maana mchana eneo hili limekuwa na watu wengi wanaokuja kuchimba makaburi, kuzika na wengine wanakuja kuzulu wapendwa wao waliowapumzisha makaburini hapa,” amesema Said.
Nao wauza misalaba kwenye maeneo mbalimbali katika Manispaa ya Morogoro wamewatuhumu mafundi wanaojengea makaburi kuwa wao ndio wamekuwa wakifanya vitendo hivyo.
Mmoja wa wauza misalaba, Ally Kitwana amedai mafundi wanaojengea makaburi ndio wanaohusika na vitendo hivyo kwa sababu wao ndio wanaokuwepo kwenye eneo hilo mara kwa mara.
“Hawa mafundi ndio tunaowatuhumu kuwa wezi wa misalaba, wanajifanya wanajengea makaburi halafu baadaye wanarudi kukata misalaba na kwenda kuuza kama chuma chakavu. Wengine wanakwenda kuuza kwa wauza misalaba, wanachofanya wanafuta jina la marehemu akija mteja wanaandika jina la marehemu mwingine,” amedai Kitwana.
Mmoja wa wauza vyuma chakavu katika Manipaaa ya Morogoro, Juma Jongo amezungumza na Mwananchi na kusema wao wanaletewa vyuma na vijana kutoka maeneo tofauti na hawawezi kujua kama huko vilikotoka vimeibwa.
“Mimi nipo hapa kwenye eneo langu la biashara, vijana wanatoka huko na vyuma vyao siwezi kujua kama wameiba ama la. Kuna wakati wanaleta vyuma ambavyo vimeshakatwakatwa siwezi kujua kama huu ni msalaba au chuma cha daraja,” amesema Jongo.
Mkurugenzi wa Manispa ya Morogoro, Emanuel Mkongo amesema taarifa za wizi wa misalaba amezipata kupitia kwa wataalamu wake na tayari ameshaanza kuzifuatilia kwa karibu, ikiwa ni pamoja na kutafuta njia ya kudhibiti wizi huo.
“Nitakaa kikao na wataalamu wangu tujadili kwa pamoja na tuone namna ya kumaliza vitendo hivyo ambavyo vimekuwa vikijirudia mara kwa mara.
“Hapa tunaangalia njia tatu, moja ni kuona uwezekano wa kuweka taa kwenye makaburi hayo na njia ya pili ni kushirikiana na Jeshi la Polisi kufanya doria za mara kwa mara katika eneo la makaburi,” amesema Mkongo.
Ametaja njia nyingine ni kuwafuatilia kwa karibu wafanyabiashara wa vyuma chakavu na kuzungumza nao, ili wajue kununua misalaba ni kosa kisheria.
“Hili suala la kujenga uzio ni zuri, lakini utekelezaji wake unahitaji mipango ya muda mrefu na fedha, kwa sasa njia ya haraka ya kudhibiti vitendo hivyo ndio hizo nilizozieleza.
“Lakini pia ipo haja kwa ndugu kujenga misalaba kwenye makaburi ya wapendwa wao kwa kutumia vifaa vingine visivyoshawishi wizi wa misalaba,” amesema Mkongo.
Mkurugenzi huyo amesema,”nimeona yapo makaburi yanayojengewa na kuwekwa misalaba ya kuchora kwa kutumia rangi badala ya kuweka misalaba ya chuma na ile ya zege ambayo ndani yake inawekwa nondo.”
Mkongo amesema ukiachilia mbali wizi wa misalaba, pia wapo watu wanaoiba vyuma kwenye madaraja na kukuta vyuma kwenye nguzo za taa za barabarani.