Kinana: Hatukubali kushutumiwa kwa uongo

Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana amesema viongozi wa chama hicho hawakatai kukosolewa, kusahihishwa, lakini hawakubali kuzushiwa wala kushutumiwa kwa mambo ambayo hayapo au ya uwongo.

Pia amewataka Watanzania kutokubali kufarakanishwa, kupandikizwa chuki dhidi ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwa hana nia njema na Bara. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Kinana ametoa kauli hiyo jana Jumapili wakati akizungumza na wananchi wa Dodoma, kwa kujibu hoja mbalimbali zilizoibuliwa na Chadema katika mikutano yake ya hadhara inayoendelea nchini.

Kinana amesema kwa muda wa wiki kadhaa Chadema walipata uhuru mkubwa kufanya maandamano, kufanya mikutano ya hadhara, kuzunguka sehemu mbalimbali nchini, na katika mizunguko yao wamezungumza mambo mengi, wameituhumu wanachama wa CCM.

“Wameituhumu serikali ya CCM, wamemtuhumu Rais kwa mambo ya uwongo, hatukatai kukosolewa, hatukatai kusahihishwa, lakini hatukubali kuzushiwa wala kushutumiwa kwa mambo ambayo hayapo au ya uwongo” amesema Kinana

Akizungumzia kuhusu sheria za uchaguzi zilizopitishwa na Bunge hivi karibuni, Kinana amesema sheria hizo ni nzuri na bora kuliko sheria zilizopita.

“Ni muhimu watambue kuwa sheria ya uchaguzi siyo njia pekee ya kushinda, ni lazima uwe na sera nzuri, kukubalika kwa chama na wagombea wanaoteuliwa na kujipanga vizuri kwa ajili ya uchaguzi huo ndio mtaji wa ushindi.

“Sheria hizi zilizotengenezwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni sheria bora kuliko ile iliyotumika 2015 na 2020, kwa namna yoyote ile. Sheria hii nawahakikishia kwamba; Tume itakua huru, itafanya kazi kwa uwadilifu,” amesema Kinana.

Aidha, Kinana amekemea mjadala ulioibuliwa kuhusu muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kusisiza kuwa muungano huo ni mfano wa kuigwa duniani na hautovunjika kamwe.

Amewataka Watanzania kutokubali kufarakanishwa, kupandikizwa chuki dhidi ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwa hana nia njema na Bara.

“Kilichofanya Muungano huu ukadumu ni historia, Bara na Visiwani tuna historia moja, utamaduni, lugha, undugu na mapambano wakati TANU na ASP vinapambana vyama vilishikamana kukomboa nchi zetu, hakuna atakayetufarakanisha,”amesema Kinana.

Amesema hoja za upinzani ni kwamba Zanzibar ni ndogo sana wanakuaje na wabunge wengi wakati wao ni milioni 1.4 pili wanasema Rais Samia Mzanzibar hana nia njema na sisi na kwamba maneno hayo hayana ukweli hata kidogo.

“Rais kaingia madarakani kwa katiba ya Tanzania amekula kiapo eti ana dhamira mbaya na upande wa pili wa muungano uongo ukirudiwa rudiwa usiposahihishwa itafanywa kuwa kweli, watanzania kataeni sumu inayopandikizwa mioyoni mwenu.

“Baba wa Taifa angesema tuimeze Zanzibar sasa hivi tungekuwa tunagombana, aliona mbali, Karume alitaka nchi iwe moja. Chadema wanataka kutufarakanisha, kutukoroga, nchi imetulia wanataka watanzania kutugawanya msikubali, tusikubali. Tupo tayari kukosolewa na kikundi chochote, lakini hatupo tayari kukubali umoja wa kitaifa ukavurugwa,” amesema.

Aidha, amesema Rais Samia ana nia na dhamira ya dhati na Bara hivyo hoja za wapinzani kuwa hana huruma wala. Nia jema na Bara, ni hoja mfu.

“Kampuni binafsi ya kimataifa ya kuhudumia makontena Tanzania (TICTS), imekuwepo tangu Serikali ya awamu ya tatu, awamu ya nne, awamu tano, awamu ya sita imeiondoa na kuweka DP Word imekuwa tatizo.

“Nani kakataa Rais Samia kuwa sio mzanzibari katoka Zanzibar katiba inasema mgombea akitoka upande wa Muungano mgombea mwenza atatoka upande wa pili ndivyo tulivyokubaliana, kitu gani cha ajabu na mgombea mwenza ana umuhimu sawa sawa na mgombea

“Mkapa (Benjamin Mkapa Rais wa awamu ya tatu) amebinafsisha mashirika zaidi ya 200 alikuwa Mzanzibari? Benki ya NBC (iliyokuwa Benki ya Biashara-NBC), Shirika la Reli lilibinafsishwa kwa Kampuni Hodhi ya Mali za Reli (Rahco) na ATC (Shirika la Ndege Tanzania), yalibinafsishwa, alikuwa Mzanzibari?” amehoji Kinana.

Akizungumzia suala la Katiba mpya, Kinana amesema  CCM ilikubali kwa kuwekwa utaratibu, lakini Chadema wamekuwa kikwazo na wameshawahi kujitoa kwenye mazungumzo na CCM.

“Tulipokua tunazungumza juu ya Katiba Chadema walikuja na hoja ndio iliyotufanya tukashindwa kuelewana, walikuja na hoja kwamba; suala la katiba liwe suala la CCM na Chadema basi. Kwanini? CCM Chama tawala na Chadema – Chama Kikuu cha upinzani, Duniani kuna vyama vya upinzani hakuna chama kikuu wala kidogo, hakipo,” amesema Kinana.

Related Posts